Azam FC yaruka kihuzi kimoja Kombe la Shirikisho
Muktasari:
- Badala yake, wawakilishi hao wa Tanzania wataanza safari yao moja kwa moja katika hatua ya kwanza, hatua inayowapa nafasi ya kupata muda wa ziada wa kujiandaa kabla ya kuingia kwenye vita ya kusaka tiketi ya hatua ya makundi.
Azam FC itaanzia hatua ya kwanza katika kampeni yake ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuthibitisha kuwa haitaanzia hatua ya awali ya mashindano hayo.
Badala yake, wawakilishi hao wa Tanzania wataanza safari yao moja kwa moja katika hatua ya kwanza, hatua inayowapa nafasi ya kupata muda wa ziada wa kujiandaa kabla ya kuingia kwenye vita ya kusaka tiketi ya hatua ya makundi.
Uamuzi huo unazipa faida kubwa Wana Lambalamba, ambazo sasa watakuwa wanasubiri washindi wa mechi za hatua ya awali ili kujua wapinzani wao.
Mbali na Azam FC, klabu nyingine zilizopewa nafasi ya kuanzia hatua hiyo ni Al Ahly (Misri), USM Alger (Algeria), CR Belouizdad (Algeria), AS FAR (Moroko), Raja Casablanca (Moroko), AS Maniema Union (DR Congo) na AS Otohô (Congo).
Hatua hiyo inaonyesha hadhi ya Azam FC katika viwango vya CAF, huku ikitarajiwa kutumia muda huo wa ziada kujiandaa vizuri kwa lengo la kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya msimu huu na kufuzu hatua ya makundi.