Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Doumbia, Ibenge presha yawavaa mapema Ligi Kuu

LIGI KUU PIct

Muktasari:

  • Katika ushindani huo mapema tu kumeanza kuchangamka kwa baadhi ya wachezaji na hata makocha kukumbana na presha ya kuonyesha uwezo katika mwanzo wa msimu mpya, kutokana na matarajio ambayo mashabiki walikuwa nayo juu yao, sasa hebu tuwangalie wale waliouanza msimu huu kwa presha.

LIGI Kuu Bara msimu wa 2026/27 inaendelea kwa kasi na wiki hii timu nyingi zitakuwa zinacheza mechi zake za sita huku ushindani ukiendelea kuwa mkubwa kuanzia timu, wachezaji na hata makocha wakionyeshana ubabe wa mbinu uwanjani.


Katika ushindani huo mapema tu kumeanza kuchangamka kwa baadhi ya wachezaji na hata makocha kukumbana na presha ya kuonyesha uwezo katika mwanzo wa msimu mpya, kutokana na matarajio ambayo mashabiki walikuwa nayo juu yao, sasa hebu tuwangalie wale waliouanza msimu huu kwa presha.

IBRAHIM DOUMBIA (SIMBA)

Pengine ndiye mchezaji mwenye presha kubwa zaidi kwa sasa nchini, Simba ilimsajili Doumbia msimu huu akitokea AS Korofina ya Mali ambako alikuwa mfungaji bora wa ligi ya taifa hilo la kisoka Afrika akifunga mabao 17 kwenye msimu wake wa mwisho.

Doumbia alitua Simba na mapema akakutana na mashindano ya Cecafa ambako katika mechi zake tatu alifunga bao moja, aliporudi nchini akakutana na mechi mbili ya kilele cha Simba na ile ya dabi ya Kariakoo, akapata nafasi lakini hakufunga bao lolote na hapo ndipo presha ilipoanzia kutoka mitandaoni.

Katika ligi, ameshacheza mechi nne kati ya tano za wekundu hao na hajafunga bao lolote huku kiwango chake kikiwagawa wadau wa soka, wengine wengi wakiona kama jamaa hakuna kitu lakini baadhi wakizidi kumpa imani ni mapema na atafanya vizuri.

Mashabiki wa Simba kuna wakati wamekuwa wakimzomea uwanjani hali ambayo imekuwa ikimfanya kuwa na presha kubwa, lakini wakati mwingine wamekuwa wakionekana kumuunga mkono kama ilivyokuwa kwenye mchezo dhidi ya Geita Gold ambao shabiki mmoja alimletea kuku.

FLORENT IBENGE (AZAM)

Kocha Mkuu wa Azam, Florent Ibenge yupo kwenye msimu wake wa pili na matajiri hao na baada ya kufanya mambo tofauti ule wa kwanza ambao aliifikisha timu hiyo hatua ya makundi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ilitarajiwa msimu huu mambo makubwa yataanza kuchomoza zaidi lakini imekuwa tofauti.

Azam imeanza msimu kwa gia ya chini sana ikishinda mechi za nyumbani dhidi ya TRA United na Pamba Jiji zote kwa ushindi wa mabao 2-1 kila moja, lakini imeonyesha kukwama ugenini ikipata sare dhidi ya Polisi Tanzania na Geita Gold na kuibuka na ushindi dhidi ya Kagera wa mabao 2-0.

Matokeo hayo siyo kitu ambacho wengi walikitarajia hususan mashabiki na viongozi wa klabu hiyo hasa kutokana na usajili uliofanywa dirisha kubwa lililopita, ulioaminisha Azam ingekuja msimu huu na moto mkubwa.

Kama Ibenge ataendelea kuangusha pointi, hilo siyo rahisi sana kuendelea kuvumiliwa na mashabiki na viongozi wa klabu hiyo na mapema tu presha imeanza kumuingia kocha huyo Mkongomani mwenye jina kubwa Afrika.

Ibenge mechi inayofuata atakuwa uwanjani kwa timu yake kucheza mechi ya tano itakapokuwa mgeni wa Simba inayoweza kuwa na maswali mengi.

FAROUK KOUMARA (YANGA)

Yanga kwenye usajili wa dirisha lililopita, ilishtua kwa kumsajili beki wa kati Farouk Koumara raia wa Ivory Coast ambaye alikuwa akiitumikia klabu moja ya Afrika Kusini, ukitajwa ni usajili uliotokana na ushauri wa kocha wa timu hiyo, Manqoba Mngqithi.

Bahati mbaya Koumara hakuanza na mguu wa baraka na kwenye mechi yake ya kwanza kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi, kosa lake likasababisha Yanga kuruhusu bao hatua ambayo ni wazi itakuwa imemharibia.

Kuanzia hapo Koumara hakupata nafasi ya kurejea kwenye mechi dhidi ya Fountain Gate ambayo alionyesha kiwango cha wastani na kuendelea kuwagawa mashabiki.

Koumara anaweza kuja kucheza vizuri lakini presha itakuwa kwake kama ubora wake utaweza kuwashawishi mashabiki wa timu hiyo ambao watataka kuona kiwango tofauti na kile walichokiona dhidi ya Eigles du Congo ambao Yanga ililala kwa mabao 2-1.

JUMA KASEJA (KAGERA SUGAR)

Kocha wa Kagera Sugar, Juma Kaseja naye ana presha yake, alikuwa hapo wakati timu hiyo inashuka daraja, akawapa heshima ya kusalia hapo na kuirudisha tena ligi kuu lakini bahati mbaya akauanza msimu vibaya.

Kagera kwenye mechi zake tano za ligi imepoteza nne, ikifungwa dhidi ya Simba nyumbani (0-2) , ikapigwa tena na Geita Gold (6-2), kisha Mashujaa (2-1) na mechi hizo mbili zikipigwa ugenini na ikatoa sare moja pekee nyumbani ilipokutana na Singida Black Stars (1-1), pia ililala mabao 2-0 dhidi ya Azam.

Bahati mbaya zaidi hadi sasa Kagera Sugar ndiyo timu iliyopokea kipigo kikali zaidi cha mabao 6-2 kutoka kwa Geita, matokeo ambayo yataongeza presha kubwa kwa kocha huyo aliyekuwa kipa mwenye jina kubwa na uwezo mkubwa nchini.

MARCEL KANADI (SINGIDA BLACK STARS)

Ligi Kuu Bara kuna raia mmoja tu kutoka Ulaya ambaye ni mchezaji, Marcel Kanadi ambaye ni raia wa Austria, ujio wake uliwashtua wengi kuona kama jamaa atawezaje kumudu ligi ya hapa kwa asili yake kutoka Uzunguni.

Kanadi bado hajaanza ligi kwa kasi ambayo watu wanatamani kuona vitu kwake, mechi nyingi mpaka sasa amekuwa akitokea benchi zaidi akipewa dakika chache na Kocha Mkongomani Pappy Kimoto, presha itakuwa kwake kuthibitisha ubora wake.

JOHN MANO (AZAM)

Baada ya Azam kuwatema washambuliaji wake wawili Japhte Kitambala na Jacque Ngita wote raia wa DR Congo wengi walitarajia kushsuhwa mshambuliaji mwenye ubora mkubwa ambaye atakuja kufanya makubwa kuwazidi wawili hao.

Matajiri hao wa Chamazi wakamleta mshambuliaji John Mano raia wa Sudan kuja kuchukua nafasi lakini bahati mbaya mpaka sasa hajafanikiwa kuonyesha makali yake akikosa mechi karibu zote, hatua ambayo imeanza kuleta mashaka.

Taarifa zaidi zinasema Mano ambaye aliwahi kufanya kazi na kocha Ibenge Al Hilal ya kwao Sudan, ametua kwa matajiri hao akiwa na ongezeko la uzito wa mwili ambapo kuna kazi inafanyika ya kumpunguza kilo zake za mwili.

Kama mshambuliaji huyo atashindwa kufanya makubwa, inawezekana akajikweka kwenye wakati mgumu lakini pia akamuongezea presha kocha wake Ibenge ambaye atakuwa anaangaliwa yeye kutokana na ujio wa mshambuliaji huyo mrefu.