Makata afichua jambo Polisi Tanzania
Muktasari:
- Polisi iliyorejea Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, ilikumbana na kichapo hicho katika mechi iliyopigwa Agosti 29, 2026, kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida, licha ya mwanzo mzuri tangu imepanda daraja.
LICHA ya Polisi Tanzania kupoteza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2026-2027, baada ya kuchapwa mabao 4-2, na Singida Black Stars, ila kocha mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makata amesifu kiwango cha wachezaji wake.
Polisi iliyorejea Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, ilikumbana na kichapo hicho katika mechi iliyopigwa Agosti 29, 2026, kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida, licha ya mwanzo mzuri tangu imepanda daraja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makata amesema mechi nne zimetoa taswira halisi ya mwenendo wa timu hiyo katika Ligi Kuu kwa msimu huu, licha ya baadhi ya mashabiki kutokuwa na imani nao tangu mwanzoni, kutokana na aina ya usajili uliofanyika.
“Wengi waliona usajili tulioufanya ni wa kawaida kutokana na baadhi ya majina kuonekana yameshaisha, ila walisahau kitu kimoja kwamba timu inajengwa na muunganiko mzuri na sio kutegemea mtu, nashukuru wameanza kuliona hilo,” amesema Makata.
Aidha, Makata amesema kichapo hicho cha mabao 4-2, kilitokana na makosa madogo ya wachezaji wa timu hiyo, ambayo hutokea kwa mtu yeyote, ingawa ni sehemu ya mchezo na ameyachukulia kwa uzito mkubwa na kwenda kuyafanyia kazi kwa haraka zaidi.
“Ukicheza na timu yenye wachezaji bora na ukafanya makosa ya kujirudia katika eneo la kujilinda ni lazima yatakugharimu, hili limekuwa ni funzo kwetu na tunaenda tena uwanja wa mazoezi kulifanyia kazi kwa uharaka ili lisijirudie,” amesema.
Kabla ya kichapo hicho, timu hiyo ilianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC, Agosti 15, 2026, kisha ikaifunga JKT Tanzania mabao 2-0, Agosti 20, 2026 na kuitembezea kichapo cha bao 1-0 Dodoma Jiji, Agosti 25, 2026.