Dalali ampa tano Mo Dewji
SIMBA inafanya maadhimisho ya miaka 90 Agosti 8, 2026 tangu ilipoanzishwa 1936. Katika safari ya mafanikio ya klabu hiyo kuna viongozi mbalimbali waliojenga misingi imara ya maendeleo yake.
Mwanaspoti lilifanya safari kutoka makao makuu ya Tabata Relini hadi Nyumba Nyeupe, Mbagala, Dar es Salaam yalipo makazi ya mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali ‘Field Marshal’. Huko lilifanya mahojiano na kiongozi huyo ambaye kwa sehemu kubwa anazungumzia historia yake ndani ya klabu hiyo na mambo anayotamani yafanyike.
Anaanza kwa kufafanua kwa nini alipewa jina la Field Marshal. “Nilipewa jina hilo kwa sababu maalumu kutokana na kazi niliyoifanya Simba. Kwa Kiingereza lina maana ya cheo kikubwa jeshini chenye mamlaka ya kufanya uamuzi na kuongoza jeshi. Mashabiki na wanachama walinipa jina hilo baada ya kuona nafanya mambo makubwa bila kuogopa.”
Mbali na hilo, ikumbukwe Dalali ndiye mwasisi wa tamasha la Simba Day. Pia anaelezea hatua mbalimbali za maendeleo ya klabu hiyo.
HUYU NDIYE MO DEWJI
Dalali anazungumzia jinsi anavyomfahamu bilionea Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ambaye pia ni mwekezaji wa Simba na namna anavyoisaidia kuhakikisha inapata mahitaji ya msingi, akisisitiza mpira wa miguu bila fedha ni vigumu kuuendesha.
“Kwanza sina shaka na Usimba wa Mo Dewji. Namfahamu tangu akiwa mdogo sana. Nakumbuka mjomba wake Kassim Dewji ndiye aliyeanza kuwa mdhamini wa Simba. Tulipokuwa na matukio ya klabu alikuwa akiongozana na Mo mara nyingi,” anasema Dalali.
“Baadaye Mo Dewji alianza kuwa mdhamini wa Simba na sasa ni mwekezaji mkubwa. Mchango wake ni mkubwa kwa sababu ili mambo yaende lazima kuwepo na fedha. Ni vigumu viongozi kuwalipa wachezaji bila kuwa na fedha.
“Soka kwa sasa ni biashara kubwa, hivyo linahitaji wawekezaji. Ndiyo maana uwepo wa watu kama Mo Dewji ni muhimu katika mpira wa miguu nchini. Kama kila kitu kingefanywa na viongozi kwa fedha zao binafsi wasingeweza. Ukiangalia usajili yanatumika mamilioni ya fedha pamoja na mishahara mikubwa. Ni kiongozi gani angeweza kufanya hayo bila wawekezaji?”
Anasema japokuwa hawezi kusema kwa sasa Mo Dewji anatoa kiasi gani kuendesha shughuli za timu kwa kuwa hayupo tena kwenye uongozi, anatambua mchango wake ni mkubwa. Anamtaka aendelee kuiunga mkono Simba ili siku moja itwae ubingwa wa Afrika.
“Inawezekana Simba ikanyakua ubingwa wa Afrika kwa sababu wawekezaji wanapoweka fedha unaweza kusajili mchezaji kutoka sehemu yoyote duniani. Hilo ndilo analotamani kuona likitokea kwa klabu ya Simba,” anasema.
Anasema jambo kubwa viongozi wa Simba kwa kushirikiana na Mo Dewji ni kuhakikisha klabu inakuwa na umoja na mshikamano, hasa kuhakikisha ubingwa unarejea Msimbazi msimu unaoanza Agosti 14, 2026.
“Kwa sasa tunatakiwa kufanya mambo yanayoendana na wakati. Kusiwe na watu wanaoanza kufikiria uchaguzi ambao bado haujafika. Wakati wake ukifika, hayo yatafanyika,” anasema Dalali.
“Simba iwe kitu kimoja. Isiwepo tena timu za viongozi. Wengine wanajiita timu ya Murtaza Ally Mangungu na wengine timu ya Crescentius Magori. Wote hao wapo kwa ajili ya kuitumikia Simba na Wanasimba.”
Jambo lingine analosisitiza Dalali ni Simba kukamilisha mchakato wa mabadiliko ili kuifanya klabu iwe imara.
“Ninaunga mkono mabadiliko kwa sababu yana manufaa. Klabu zimepitia hatua nyingi za maendeleo. Kinachotakiwa ni kuhakikisha mabadiliko hayo yanazingatia masilahi ya klabu.”
Anaongeza: “Nimewahi kuwa kiongozi, tena katika kipindi kigumu. Hatukuwa na mdhamini, tulitegemea mapato ya langoni kuwalipa mishahara wachezaji. Wakati mwingine tulilazimika kuuza baadhi ya mali za klabu ili mambo yaende. Ndiyo maana naona kuna umuhimu mkubwa wa wawekezaji kuwepo kwenye timu.”
“Kwa sasa naona wachezaji wanachukua maji ya chupa na kujimwagia kichwani. Tumetoka mbali; enzi zetu maji yalikuwa kwenye mifuko. Wakati mwingine tulibeba ndoo mazoezini wachezaji wakachota kwa kikombe ndipo wanywe. Maendeleo yaliyopo yanapaswa kuungwa mkono.”
KULINDA WAWEKEZAJI
Anasema Wanasimba wana jukumu la kuhakikisha wanawalinda wawekezaji ikiwa wanataka klabu hiyo iwe mfano wa kuigwa Afrika. Anasisitiza yapo mambo ambayo hayapaswi kuachwa kwa viongozi pekee.
“Mfano mzuri ni suala la jezi feki. Wanachama na mashabiki wa Simba wana uwezo wa kulidhibiti. Ili mwekezaji afaidike na klabu ipate mapato wanapaswa kuacha kununua jezi feki. Ikiwezekana wakiwabaini watu wanaozitengeneza au kuziuza watoe taarifa kwa polisi,” anasema Dalali.
“Mfano, kuna Kampuni ya Jayrutty chini ya CPA Joseph Rwegasira ambayo inasimamia utengenezaji na usambazaji wa jezi na vifaa vyenye nembo ya Simba. Kampuni hiyo inapaswa kuungwa mkono. Mashabiki wa Simba wakiacha kununua jezi feki faida itaongezeka. Pia aliahidi kujenga uwanja wenye uwezo wa kubeba mashabiki kati ya 10,000 na 12,000 kule Bunju, hivyo ni vyema akalitekeleza hilo.”
WAZO LA SIMBA DAY
Anasema wazo la kuanzisha tamasha la Simba Day alilipata baada ya kutembelea matawi mbalimbali ya klabu, ambako alibaini wanachama walikuwa na kiu ya kuwa na uwanja wao.
“Nilipopata wazo hilo niliwashirikisha viongozi wenzangu. Baadhi yao walilipinga, lakini kwa kuwa nilikuwa mwenyekiti nikasimamia msimamo wangu. Hata hivyo, siku moja kabla ya kufanyika kwa Simba Day na tuliialika Sports Club Villa ya Uganda mmoja wa viongozi aliita vyombo vya habari na kutangaza Simba Day haitafanyika,” anasema.
“Nakumbuka wakati huo nilikuwa Bagamoyo. Nilipoona taarifa hizo kwenye vyombo vya habari ilikuwa jioni nikarejea Dar es Salaam. Asubuhi yake nikaenda redioni na kuwaeleza watu Simba Day ingefanyika kama ilivyopangwa kwa sababu timu tuliyoialika ilikuwa tayari imewasili.
“Ingawa kulikuwa na mkanganyiko miongoni mwa viongozi na tukaitwa kupatanishwa. bBaadaye wale walionipinga walikuja kuona lilikuwa wazo zuri. Leo linaendelea kuishi na kuingizia Simba mapato makubwa. Timu nyingine pia zimeiga na zinafaidika nalo. Mimi huiita Yanga Day siyo Wiki ya Wananchi kwa sababu wote ni wananchi wa Tanzania. Nakumbuka hata nilimshauri aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga wakati huo, Imani Madega, lakini alidharau wazo hilo. Wakati huo utani wa jadi haukuwa ugomvi wala uhasama.”
Anasema katika tamasha la kwanza la Simba Day walikusanya Sh70 milioni na Sh20 milioni zilipelekwa kwenye mradi wa uwanja wa Bunju. Pia anamshukuru aliyekuwa katibu wake Mwina Kaduguda kwa mchango mkubwa alioutoa kufanikisha tamasha hilo.
“Kaduguda ana uwezo mkubwa wa ubunifu. Ukizungumzia Simba Day huwezi kumtenga. Ni msomi na bado anaendelea na masomo. Pia anaandaa kitabu kuhusu mpira wa miguu.”
Anasema baada ya Simba kuanzisha tamasha hilo, timu ya kwanza kuiga ilikuwa Ndanda mwaka 2014, ilipoialika Simba kucheza nayo mechi ya kirafiki, ingawa baadaye ilishuka daraja.
“Kuiga si jambo baya. Niliwashauri mara nyingi Yanga wawe na Yanga Day, ambayo leo inawaingizia mamilioni ya fedha. Kiukweli, ningekuwa katika nchi nyingine, huenda ningekuwa bilionea kwa kuanzisha jambo linaloendelea kuishi na kuingiza mabilioni ya fedha. Bahati mbaya haijawa hivyo.”
“Ninachojivunia ni kuona wakati wa matamasha hayo huduma kwa jamii zinafanyika, ajira za muda zinapatikana, na watu wengi hupata zabuni za kufanya kazi mbalimbali. Hilo linanithibitishia sikutumia muda wangu wa uongozi bure.”
Anasema kinachomfurahisha zaidi ni Simba Day ya mwaka huu wakati klabu ikitimiza miaka 90 itafanyika Uwanja wa Uhuru ambako tamasha hilo lilifanyika mara ya kwanza Agosti 8, 2009.
“Naamini historia nyingine itaandikwa. Tunarejea kwenye uwanja tuliouzindulia Simba Day. Hata hivyo, nina jambo moja la kuwaomba viongozi wa Simba.”
“Wakati Simba inatimiza miaka 90, mzee Hamis Kilomoni naye anatimiza miaka 90. Viongozi wampe mwaliko maalumu kwa sababu ametoa jasho kubwa kuitumikia klabu. Baraka nyingine hutokana na kuwathamini waliotutangulia.
“Pia, Simba inapokwenda kutoa misaada kabla ya Simba Day, iwakumbuke Wanasimba waliopo vitandani kwa kuwafikishia misaada. Mfano ni Stambuli Mponda, ambaye alikuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu kwenda kwenye mfumo wa kisasa. Nimekuwa nikisisitiza jambo hilo kwa viongozi, lakini sijaliona likitekelezwa. Natamani naye awe miongoni mwa watakaonufaika na misaada hiyo.”
ALAMA ALIZOACHA
Anasema anaamini mambo aliyoyafanya akiwa Simba yataendelea kubaki kwenye kumbukumbu za mashabiki na viongozi watakaokuja kuiongoza klabu hiyo.
“Katika kipindi changu cha uongozi nilianzisha Simba B, Simba Queens, Simba Day, mradi wa uwanja wa Mo Arena, matawi, kadi za kisasa za uanachama, nikaboresha ada za uanachama na kufanikisha upatikanaji wa wadhamini wa timu,” anasema na kuongeza:
“Siku moja kiongozi mmoja mkubwa serikalini aliniona nikipanda daladala. Akawatuma watu waniite Dodoma. Nilipofika ofisini kwake, aliniambia, ‘Wewe ni mtu mkubwa sana, kwa nini unapanda daladala?’
“Kisha akaniambia nitaje gari ninayopenda. Nikamjibu sitaki gari. Akaniambia nitoke nje nikafikirie tena. Alinifanyia hivyo mara tatu. Mwishowe akaniuliza ninataka nini. Nikamwambia ninachohitaji ni udhamini kwa timu yangu. Jibu hilo lilimshangaza, ndipo akaniandikia barua ya utambulisho kwenda kwa viongozi wa Kiwanda cha Bia.”
“Kwa kuwa ilikuwa jioni na hakukuwa na usafiri wa kawaida, nilipanda lori kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam usiku. Safari yote mkono wangu haukutoka mfukoni kwa kuhofia barua ile isidondoke. Nilifika saa 12:00 asubuhi katika ofisi za Breweries, lakini mlinzi akaniambia nisubiri hadi saa 2:00 ndipo ofisi zitakapofunguliwa.”
“Saa 2:00 viongozi walipoanza kuwasili, niliwakabidhi barua ile. Walipoona muhuri wa Serikali hawakuniuliza maswali mengi. Walikubali kutoa udhamini, lakini wakaniomba nizungumze na viongozi wa Yanga ili udhamini utolewe kwa klabu zote mbili. Nikampigia simu Madega, akafika, tukasaini mikataba. Miongoni mwa walivyofanikisha ni kupatikana kwa mabasi ya timu, kulipwa mishahara ya wachezaji na mambo mengine mengi.”
Mbali na hilo, anasema wakati wa uongozi wake, tawi la Friends of Simba lilifanya kazi kubwa ya kusaka na kusajili wachezaji wenye vipaji, huku wanachama wake wakitumia fedha zao binafsi.
“Japokuwa nilitokea tawi la Ngurumo za Simba, baadaye gazeti la klabu lilipewa jina hilo. Kwa sasa tawi hilo linajulikana kama Mpira Pesa,” anasema na kuongeza:
“Baadhi ya viongozi waliokuwa Friends of Simba na waliofanya kazi kubwa ya kusaka vipaji ni marehemu Zacharia Hanspope, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ na Evans Aveva.”
“Viongozi hao ndio waliounda Simba B iliyozalisha wachezaji kama Jonas Mkude, Christopher Edward, Ibrahim Ajibu, Abdallah Seseme, Said Ndemla, Haruna Chanongo na wengine wengi.”
Anasema, mbali na viongozi hao, aliyekuwa meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alitoa mchango mkubwa katika kulea vijana hao kwa kutumia muda wake na hata fedha zake binafsi. Anaamini uongozi wa sasa unapaswa kumthamini kutokana na kujitoa kwake kwa masilahi ya klabu.
“Katika mafanikio ya Simba B, Patrick Rweyemamu amehusika kwa kiwango kikubwa. Ukiwauliza kina Mkude, Ajibu na Ndemla watakuambia jinsi alivyowalea kama watoto wake. Kipindi hicho tuliishi kama familia moja yenye upendo,” anasema.
Jambo lingine analojivunia ni kuiongoza Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2009/10 bila kupoteza mchezo hata mmoja.
ISHU YA MASHABIKI
Anapoulizwa: “Unalizungumziaje tukio la baadhi ya mashabiki wa Simba, baada ya klabu hiyo kutwaa taji la CRDB, kwenda katika makao ya Yanga na kujisaidia?”
Anajibu: “Sidhani kama kuna mtu alivua nguo na kuanza kujisaidia kweli. Nafikiri ilikuwa ni utani. Ndiyo maana sikuamini hata taarifa zilizosema kwamba mashabiki wa Yanga, baada ya kutwaa ubingwa, walipita Msimbazi na kurusha chupa zenye mikojo. Naamini hayo yalikuwa ni matukio ya utani tu.”
Hata hivyo, anasema hajawahi kusahau tukio la mwaka 2008, alilofanyiwa na mashabiki wa Simba baada ya timu kufungwa mabao 2-0 na Azam FC huku ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
“Zilifika kosta tatu zilizojaa mashabiki nyumbani kwangu kwa lengo la kufanya vurugu. Kwa bahati nzuri, kuna mtu alinipenyezea taarifa mapema. Waliposhuka kwenye magari, wakaanza kuipiga nyumba mawe. Nikaiweka familia yangu mahali salama, kisha nikatoka nje kwenda kuzungumza nao,” anasema na kuongeza:
“Nikawauliza ‘mnataka nini?’ Wakanijibu ‘ujiuzulu kwa sababu umefungwa na Azam.’ Nikawaambia bado kulikuwa na mechi nyingi na tulikuwa nafasi ya pili. Wakasisitiza hawakunitaka. Nikawauliza tena ‘mnataka nini kingine?’ Wakasema wanataka kujisaidia ndani ya nyumba yangu. Nikawafungulia milango.”
“Waliingia ndani na kujisaidia sehemu mbalimbali. Nadhani walikuwa wametoka Kariakoo kula mapera. Baada ya kumaliza, nikawaambia waende wakajisafishe uwanjani ambako kulikuwa na jaba la maji. Wengine walijisafisha hapo, lakini wengine walienda mbali zaidi na kujisaidia hadi sehemu ambayo nilikuwa naswalia, na wengine hata juu ya bati.”
Anasema baada ya tukio hilo mashabiki hao waliondoka, na siku iliyofuata alienda makao makuu ya Simba, ambako aliwakuta mashabiki na kutangaza kujiuzulu.
“Kuna waziri mmoja aliona tukio hilo, akanipigia simu na kuniomba nirejee kazini. Pia alinisaidia kuwafikisha mashabiki hao polisi. Walipobanwa, walimtaja mmoja wa viongozi wenzangu kuwa ndiye aliyewakodisha kwa Sh300,000. Baadaye waliniomba msamaha, nami nikawasamehe kwa sababu kiongozi huyo alikuwa miongoni mwa wale niliowaondoa madarakani wakati wa mabadiliko ya uongozi,” anasema.
Anaongeza kuwa baada ya wiki mbili alirejea tena klabuni na kufuta uamuzi wake wa kujiuzulu, akisema hakuwahi kuwasilisha barua rasmi ya kuachia nafasi hiyo, hivyo aliendelea kuhudumu hadi alipostaafu mwaka 2010.
“Baadhi ya wale waliojisaidia sehemu ambayo nilikuwa naswalia walifariki baadaye. Wengine walikuja kuniomba msamaha. Nikawaambia wamwombe Mwenyezi Mungu. Hayo ni miongoni mwa matukio magumu niliyowahi kukutana nayo,” anasema.
Anapoulizwa ni nani aliyefanya usafi baada ya nyumba yake kuchafuliwa na mashabiki hao.
“Nilimuomba mke wangu anisamehe na anivumilie kutokana na kazi niliyokuwa nafanya. Yeye ndiye aliyefanya usafi, ingawa familia yangu ilinisisitiza niache kazi hiyo, lakini haikuwezekana,” anasema.
WAKIMBIZA WADHAMINI
Anasema mwaka 2006 alipata udhamini kutoka benki moja ya Afrika Kusini, ambao ungewezesha kujengwa ghorofa 25 kwa ajili ya Simba, lakini mpango huo ulivunjika kutokana na upinzani wa baadhi ya mashabiki.
“Walikubali kutujengea gorofa 25 eneo la Msimbazi. Makubaliano yalikuwa kwamba kwa miaka 10 wangetumia gorofa tano za chini, huku 20 zikiwa za Simba. Baada ya kipindi hicho, majengo yote yangekuwa mali ya Simba. Pia walikuwa wameahidi kujenga hospitali. Mzungu mmoja alikuja kupiga picha za eneo, lakini baadhi ya wanachama wakamshambulia na kuvunja kamera yake wakidhani tunataka kuuza mali za klabu,” anasema na kuongeza:
“Walianza kueneza taarifa kwamba mimi na tawi la Friends of Simba tulitaka kuuza mali za klabu, jambo ambalo halikuwa kweli. Nisingeweza kufanya uamuzi wa aina hiyo bila kuwashirikisha wanachama. Baada ya kuwaeleza ukweli walielewa, lakini niliporudi tena kwa wale wawekezaji, walikataa kuendelea na mradi wakisema sisi ni watu wa vurugu.”
ITAENDELEA KESHO