Dah! Yanga watamu sana
Donald Ngoma, Mshambuliaji wa PLatnum Fc ya Zimbabwe
Muktasari:
Ngoma ambaye anahitajiwa na kocha wa Yanga, Mholanzi Hans Pluijm, ambaye alithubutu kusema Didier Kavumbagu wa nini wakati unaweza kuwa na mtu kama huyu (Ngoma).
MSHAMBULIAJI wa kimataifa Zimbabwe anayeichezea FC Platnum ya kwao, Donald Ngoma, anayehusishwa na mipango ya kutua Jangwani, amefungua kinywa chake na kutamka maneno machache tu akisema: “Yanga ni watamu sana.”
Ngoma ambaye anahitajiwa na kocha wa Yanga, Mholanzi Hans Pluijm, ambaye alithubutu kusema Didier Kavumbagu wa nini wakati unaweza kuwa na mtu kama huyu (Ngoma).
Itakumbukwa Mwanaspoti pekee lenye uwezo wa kusafiri popote zinapokwenda timu za soka za hapa nchini ndiyo lilifichua harakati za Yanga kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo.
Kufuatia taarifa nyingi Mwanaspoti liliamua kumsaka mshambuliaji huyo na kufanya mazungumzo naye kwa njia ya simu ya mkononi na akaeleza kila kitu kuhusu kinachomchelewesha kutua kwake kwa Mabingwa hao wa Tanzania;
Mwanaspoti: Habari yako Donald Ngoma
Ngoma: Salama. Nazungumza na nani?
Mwanaspoti: Unaongea na mwandishi wa gazeti bora la michezo Tanzania la Mwanaspoti.
Ngoma: Nashukuru, niambie.
Mwanaspoti: Vipi maendeleo yako na hapo ulipo FC Platinum?
Ngoma:Kila kitu kinaendelea vyema tunaendelea na ligi, japo leo (jana Jumapili) tupo mapumziko kidogo.
Mwanaspoti: Ngoma, hapa Tanzania kuna taarifa nyingi juu yako kuhusu kuja huku likoje hili?
Ngoma: Kuna uwezekano wa hilo kama kila kitu kitakwenda sawa.
Mwanaspoti: Gazeti hili lingependa kujua ni timu ipi unafanya nayo mazungumzo ya kuja hapa Tanzania?
Ngoma: (Anacheka kidogo) Nipo katika mazungumzo na Yanga, lakini nasisitiza bado kila kitu hakijamalizika.
Mwanaspoti: Kila kitu hakijamalizika, mashabiki wa Yanga wangependa kujua nini kinachelewesha safari yako ya kuja hapa?
Ngoma: Bado nawasubiri Yanga wakamilishe kila kitu tulichokubaliana ili nije.
Mwanaspoti: Unapozungumza nao unafikiri hilo linaweza kukamilika lini, na ukaja hapa Tanzania?
Ngoma: Nafikiri kila kitu kitakuwa tayari itakapofika wiki ijayo (wiki hii), unaweza ukawauliza wao hapo watakueleza.
Mwanaspoti: Tungependa kufahamu unaijuaje Yanga?
Ngoma: Kwangu Yanga niliwajua wakati tulipocheza nao wakatutoa ni kama miezi miwili iliyopita, timu nzuri nafurahi kusikia wananihitaji.
Mwanaspoti: Kipi kimekuvutia katika timu yao wewe ukaamua kukubali kuja?
Ngoma: Napenda wanavyocheza soka la kushambulia, hiyo ni aina ambayo mchezaji yeyote angependa kuona timu yake inacheza hivyo. Kifupi Yanga ni watamu sana kisoka.
Mwanaspoti: Mkataba wako na FC Platinum ukoje?
Ngoma: Bado nina mkataba na Platinum, na bado tunaendelea na ligi kwa hiyo kwa sasa hakuna ninachopoteza kwa kuwa naendelea kuitumikia timu yangu mpaka hapo Yanga watakapomaliza kila kitu kuhusu mimi kuja huko, nataka kubadilisha mazingira kidogo.
Mwanaspoti: Tunaamini mambo yanaweza kuwa sawa, Yanga ni timu yenye mashabiki wengi hapa nini kauli yako kwao?
Ngoma: Wanatakiwa kusubiri nije huko, lakini kwangu najua kufanya kazi yangu ndiyo maana wakanihitaji, tusubiri
Mwanaspoti: Ahsante Ngoma kwa kushirikianna nasi, karibu sana Tanzania na Yanga
Ngoma:Ahsante kazi njema
Baada ya mazungumzo hayo na Ngoma Mwanaspoti lilimtafuta Katibu wa Yanga Dk Jonas Tiboroha ambaye licha ya kugoma kuelezea walipofikia kwa mchezaji huyo, lakini aligusiua kwamba mshambuliaji huyo ni mmoja ya watu waliosalia katika usajili wao.
“Tunaendelea kufanya mambo yetu kwa utulivu, sitaki kuliongelea sana jambo ambalo bado hatujalikamilisha lakini lolote linaweza kutokea kwa huyo mchezaji kuja hapa nchini.
Mkwasa alonga
Mpaka jana Yanga ilikuwa imesajili wachezaji watano ambao ni viungo washambuliaji Deus Kaseke na Malimi Busungu ambao wanatarajiwa kuziba pengo la Mrisho Ngassa aliyetimkia Afrika Kusini. Wengine waliosajiliwa ni winga chipukizi, Geofrey Mwashiuya aliyenyakuliwa mapema, kipa Benedict Tinoco na beki Haji Mwinyi Ngwali.
Kusajili kwa akina Kaseke na Busungu kumeelezwa kutaongeza ushindani Jangwani kwani tayari Yanga ilikuwa na wakali kama Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Salum Telela na Amissi Tambwe ambao ni tishio kwa vikosi vingine.
Wachezaji hao ndiyo wanatarajiwa kuiboresha safu hiyo msimu ujao ambapo Jerry Tegete, Danny Mrwanda, Hussein Javu, Said Bahanuzi, Nizar Kharfan wanadaiwa kuachwa, wakati Mliberia Kpar Sherman na Mbrazili Andrey Coutinho wamewekwa sokoni.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa ameliambia Mwanaspoti: “Kama benchi la ufundi, tulipeleka mapendekezo yetu kwa uongozi na ndivyo wanavyofanyia kazi.
“Mpaka hapo palipofikia sasa ni mahali pazuri mambo bado yanaendelea kiujumla naweza kusema ni kazi nzuri. Kuhusu uwezo wao uwanjani, wachezaji hao ni wazuri mambo mengine itategemea na namna tutakavyoanza maandalizi yetu na ushindani ndiyo mafanikio ya timu.”
Kaseke, Busungu waliwindwa sana na Simba ambayo iliwahitaji kwa nguvu lakini watani wao hao wa jadi waliwazidi ujanja na kunasa sahihji za wawili hao kwa ajili ya msimu ujao.
Wachezaji hao, wana uwezo wa juu wa kucheza nafasi ya ushambuliaji wa pembeni yaani winga, watafanya ushindani wa juu ya Mwashiuya, Msuva na Niyonzima ambaye ana uwezo wa kucheza pembeni na katikati.