Cheki Hamis anavyowakimbiza hadi Wakenya
Muktasari:
Tangu ametua katika Ligi Kuu Kenya, Hamis amekuwa na mafanikio ndani na nje ya uwanja, tayari amecheza katika klabu za Sony Sugar na msimu huu amejiunga na Bandari FC pia amepata nafasi ya kuichezea Taifa Stars.
ACHANA na yale maisha ya kuharibu kwake mipango ya wapinzani kwa ukabaji wake wa kibabe ndani ya uwanja, nyota wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Kenya Abdallah Hamis sio mtu wa mchezo mchezo kabisa.
Kiungo huyo aliyepo klabu ya Bandari FC ya Kenya ni mtu mwingine kabisa nje ya uwanja kwani upole na kujichanganya kwake mitaani kulimfanya aonekane ni Mkenya na alipoanza kufanya vizuri akiwa Sony Sugar walimpigia debe aitwe Harambee Stars.
Mei mwaka huu, Hamis alipata shavu la kujiunga na Bandari aliyoisaidia kumaliza nafasi ya pili katika Msimamo wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) na kubeba ndoo yenye thamani ya million 1.5 za Kenya, nyuma ya mabingwa Gor Mahia ya Dylan Kerr.
Mwanaspoti imefanya mahojiano ya kina na kiungo huyo mkabaji aliyeanika maisha yake kwa ujumla nchini Kenya na mipango yake mingine ya kimaisha na soka, ambapo katika msimu uliomalizika alihusika na mabao saba katika mechi nane alizocheza akiwa na klabu yake ya Bandari FC.
AITEKA MOMBASA
Asikuambie mtu, Mtanzania huyo katika mji wa Mombasa, Kenya ni kama ameuteka kwa jinsi anavyokubalika tangu alipotua kwa mara ya kwanza mwaka 2016 alipoanza kuichezea Muhoroni Youth FC na baadaye Sony Sugar kabla ya kutua Bandari kwa sasa.
Hamis anasema amejizolea umaarufu kwenye mji huo kutokana na kiwango ambacho amekuwa akikionyesha toka amejiunga na wazee wa Bandari Mei mwaka huu.
"Sina tabia ya kujiona staa ndio maana nimekuwa mtu wa kujichanganya, watu wa Mombasa wamekuwa wakinipa sapoti ya kutosha pengine ni kutokana na kujituma kwangu uwanjani," anasema kiungo huyo aliyewahi kuitwa mara kadhaa katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Salum Mayanga.
WAKENYA WALIMTAKA
Wakenya wengi walikuwa wakihisi, Hamis ni Mkenya alipoonyesha kiwango cha juu ndani ya msimu wake wa kwanza wadau wengi wa soka walianza kumpigia chapuo la kuitwa timu yao ya taifa ya Harambee Stars.
Hamis aligoma kuichezea Harambee Stars na alikutana na changamoto ya kuwaelekeza watu kuwa yeye ni Mtanzania na ndoto yake ni kuitumikia Taifa Stars.
"Walijisikia vibaya Wakenya lakini sikuwa na jinsi, bahati nzuri haikuchukua muda kwa mara ya kwanza chini ya Salum Mayanga nilipata nafasi ya kuitwa Taifa Stars mwaka 2017 na kucheza michezo tisa.
"Nakumbuka mechi ya kwanza kuichezea Taifa Stars ilikuwa dhidi ya Botswana na ya mwisho ni dhidi ya Uganda kwenye mashindano ya Cecafa," anasema.
ALIHISI KUTENGWA
Alipotua Kenya, Hamis anasema alihisi kutengwa na Wakenya kutokana na namna ambavyo walikuwa wakipenda kuzungumza lugha zao hata wakati wa mazoezi.
"Nilikuwa najiona mpweke maana kuna kipindi nilikuwa nikihisi kuwa wananisema ili ilifika muda nikazoea mazingira hayo na kuona kawaida. Labda nikujulishe kuwa, huku Kenya ni tofauti na Tanzania, watu wanathamini sana makabila yao," anasema.
YEYE NA STAREHE
Kwa mchezaji yanki kama yeye na anayemwagiwa sifa ni rahisi kujitosa kwenye starehe na kujirusha kwa sana ili kula ujana, lakini kwa Hamis mambo ni tofauti kabisa.
Ukitaka ugombane na kiungo huyo we mletee ishu za starehe, kwani anasema starehe kiukweli zimempitia kushoto toka akiwa mdogo alilelewa kwenye misingi mizuri ya dini na maisha, hivyo anathamini zaidi kazi kuliko mambo hayo ambayo anaamini ni mwanzo wa kupoteza watu hasa wale wasioweza kujidhibiti.
"Mfano naenda klabu kwanza hata kucheza kwenyewe sijui siwatanicheka maana hata pombe pia situmii, kidogo nachokipata nakitumia kwenye mambo ya msingi na sio starehe," anasema.
ANAPENDA MUVI BALAA
Anasema kitu pekee anachokipenda zaidi ni kuangalia muvi hasa anapokuwa kwenye mapumziko. "Napenda muvi balaa," anasema Hamis na kuendelea kuwa amekuwa akitumia muda wake mwingi pindi anapomaliza purukushani za uwanjani kupumzika huku akitupia macho yake kwenye muvi.
"Sifichi bwana, mi napenda muvi yoyote ile nzuri, nyumbani tumeshuka kwenye utengenezaji wa muvi, lakini huwa natumia muda wangu kwenye vichekesho naona upande huo kuna nguvu bado licha ya kuondokewa na Mzee King Majuto."
"Wamarekani niseme ndio watu ambao wameliteka soko la muvi duniani, wajua kuuvaa uhusika wa muvi pamoja na kuzitengeneza tatizo letu nyumbani hatuwekezi kwenye kazi," anasema.
Hamis anamini kinachobomoa ubora wa kazi nyingi za Bongo muvi ni mtu mmoja kubeba zaidi ya majukumu matatu hadi manne kwenye muvi moja.
"Huwezi mtu mmoja ukawa ndiye mtunzi, muigizaji, mtayarishaji, muongozaji na sijui kusimamia nini, wenzetu wanawapa majukumu wenye kumudu kazi husia, ndio maana unakuta Van Damme anaigiza, lakini hadithi imetungwa na mwingine na hata mwandishi wa mswada ni mtu mwingine, ndio maana kazi zao zina ubora," anasema.
MADEMU WA KENYA
Hamis anakiri kwamba kama mwanaume, amekuwa akipata usumbufu kwa wasichana wa Kenya, lakini amekuwa makini mno.
Unaambiwa hana mpango na mademu wa Kenya kabisa na anasema nyota huyo wa Kitanzania kuwa ameshajichagulia mchumba nyumbani Tanzania anasubiri muda ufike ili afunge naye pingu za maisha.
Hamis aliyezaliwa Novemba 16, 1997 anasema sio kwamba mademu wa Kenya ni wabaya lakini hapendelei kuoa nje ya nchi yake ya Tanzania.
"Sipendi kumweka wazi mchumba wangu kwa sasa kwa sababu kuna mambo tunayaweka sawa kwanza, muda sahihi ukifika nitamweka wazi na kumwoa kabisa," anasema.
AZIPOTEZEA SIMBA NA YANGA
Kiungo huyo mwenye urefu wa futi sita kasoro inchi moja, anasema hana mawazo ya kuzichezea Simba na Yanga kwa sasa na badala yake ameelekeza nguvu zake kupigania nafasi za kucheza soka la kulipwa kwenye mataifa yaliyoendelea zaidi ya Kenya.
Hamis anasema kutoka Kenya kurudi Tanzania ni sawa na kutoa fedha kwenye suruali au nguo yoyote kutoka mfuko wa kushoto kwenda wa kulia.
"Kenya na Tanzania utofauti wa soka lake ni mdogo, nataka kuendele kuonyesha uwezo wangu huku ili nisonge mbele na sio kurudi nyuma au kusalia hapa hapa, hizi Simba na Yanga hazitofautiani na klabu zilizopo Kenya," anasema.
Hamis anasema anachopigana kwa sasa ni kujitangaza vyema kabla ya kuanza safari ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi za Afrika Mashariki na ikiwezekana Ulaya akiamini uwezo na kipaji cha kufanya hivyo anavyo.
AWATAJA SAMATTA, MSUVA
Hamis anasema hakuna anachowaza kichwani mwake zaidi ya kupiga hatua kama ilivyo kwa nyota wengine wa Kitanzania wanaocheza kwenye ligi kubwa zaidi Afrika na hata Ulaya.
Washambuliaji Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Saimon Msuva wa Difaa El Jadida ya Morocco aliwataja kama mifano mizuri kwake ambayo imekuwa ikimfanya kuongeza ufanisi kwenye uchezaji wake soka.
"Nina mahusiano mazuri na wachezaji hao huwa ninapata muda wa kuongea nao kwa lengo la kubadikishana mawazo, niwachangafu na wepesi kutoa moyo," anasema Hamis.
Nyota huyo wa Kitanzania anasema moja ya Ligi ambayo anatamani kupata nafasi ya kucheza ni Ligi Kuu ya Afrika Kusini 'PSL' ambayo pia anaichezea Abdi Banda akiwa kama nahodha msaidizi wa Baroka FC.
AMPIGIA SALUTI MIENO
Hamis ambaye ana uzito wa 79 Kg anasema moja ya wachezaji anaowakubali Kenya ni Hamphrey Mieno aliyekuwa Tusker kabla ya sasa kuichezea Gor Mahia. Anasema nyota huyo aliyewahi kukipiga pia Azam FC ni mkali na anayemkuna kwa soka lake.
"Viungo kibao ambao nimekutana nao huku Kenya huyo jamaa ni balaa anauweza sana mpira, huwa nakuwa naye makini pindi timu zetu zikikutana," anasema.
ANA MJENGO MATATA
Hamis mwenye umri wa miaka 21, ni mjanja kinoma, kwani licha ya kuwazidi nyota wengine nchini kwa kukimbili kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania, lakini hata katika masuala ya kimaisha hayupo nyuma bwana!
Tofauti na umri alionao ama muonekano wake wa kibishoo, jamaa ana akili na hivi unavyomsoma, anaendelea na ujenzi wake wa nyumba ya kisasa mkoani Mwanza ambako amepanga iwe na bwawa la kuogelea (Swimming Pool).
"Swimming ni muhimu kwa wachezaji maana kuna uhitaji wa muda mwingine kukaa kwenye maji kwa muda mrefu ili kurejesha utimamu wa mwili wao wanaita kurecover," anasema.
Anafichua kuwa, japo hapendi kuaminika mambo yake hadharani, lakini mjengo huo matata mpaka sasa umemgharimu zaidi ya Shilingi 50 milioni ambazo zimetokana na jasho lake linalopatikana kwenye kazi yake ya soka.
"Katika maisha ya sasa usipojipanga mapema, unaweza kuja kuumbuka mbele ya safari, ndio maana nimeanza kujipanga ili hata nikiachana na soka niwe na mahali pa kuegesha ubavu," anasema kiungo huyo.