Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CAF yaipongeza Zanzibar maandalizi ya AFCON 2027

ZANZI Pict

Muktasari:

  • Pongezi hizo zimetolewa na timu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) iliyofanya ziara ya kukagua huduma za afya Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya maandalizi ya nchi zitakazokuwa wenyeji wa mashindano hayo.

ZANZIBAR imepongezwa katika kuimarisha huduma za afya na huduma za dharura kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Pongezi hizo zimetolewa na timu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) iliyofanya ziara ya kukagua huduma za afya Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya maandalizi ya nchi zitakazokuwa wenyeji wa mashindano hayo.

Mwakilishi wa CAF, Dk Boubakar Sidiki, amesema ziara hiyo imelenga kutathmini uwezo wa vituo vya afya, huduma za dharura na upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya wachezaji, viongozi na watazamaji wakati wa mashindano.

Amesema CAF imeridhishwa na maandalizi yaliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikiwemo uwepo wa magari ya wagonjwa mapya (ambulance), kitengo maalum cha masuala ya michezo, huduma za dharura, MRI pamoja na huduma nyingine zinazokidhi viwango vinavyohitajika kimataifa.

ZANZ 01

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Mgereza Mzee Miraji, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu ya vifaa tiba, huduma za dharura na uwezo wa vituo vya afya, hatua inayoiweka Zanzibar katika utayari wa kutoa huduma wakati wa AFCON 2027.

"Zanzibar iko tayari kuwapokea wachezaji, viongozi, mashabiki na wageni watakaofika kwa ajili ya mashindano hayo, hadi sasa zipo ambulance 10 ambazo zitatumika kuimarisha huduma za dharura kwa maeneo mbalimbali yatakayohusika na mashindano," amesema Dk Mgereza.

Naye Dk Zainab Kheri Hassan ambaye ni Mjumbe wa Wizara ya Afya katika Timu ya Maandalizi ya AFCON, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi wakati wa mashindano hayo na kutumia fursa mbalimbali zitakazotokana na ujio wa wageni, hususani katika sekta ya utalii.

Amesema Wizara ya Afya imeandaa mfumo maalum wa utoaji wa huduma za matibabu kwa wachezaji, watazamaji na wageni katika kipindi chote cha mashindano, ambapo Hospitali ya Rufaa ya Lumumba na Hospitali ya Ampola zitakuwa sehemu muhimu ya mpango huo.

ZANZ 02

Fainali hizo zinatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027 ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Kwa Tanzania, mechi zinatarajiwa kuchezwa Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Arusha (Uwanja wa Samia Suluhu Hassan) na Zanzibar (Uwanja wa New Amaan Complex na Fumba vilivyopo Unguja).

Timu ya ukaguzi ya CAF, ipo Tanzania kuanzia Septemba 1, 2026 hadi 3, 2026, kwa ajili ya kukagua maandalizi na miundombinu kuelekea AFCON 2027. 

Ukaguzi huo ni mwendelezo wa mchakato wa CAF kutathmini utayari wa nchi wenyeji, ambapo hivi karibuni timu hiyo ilikuwa nchini Kenya kufanya ukaguzi wa viwanja na vifaa vingine muhimu.