Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TAEC, IAEA wakabiliana na mianya ya uhalifu wa nyuklia AFCON 2027

SAMIA Pict

Muktasari:

  • Muhtasari:Katika kukabiliana na hatari za kiusalama kwenye mikusanyiko mikubwa hasa kwenye michuano ya AFCON inayotarajiwa kufanyika hapa nchini mwaka 2027, Tume ya Nguvu za Atomu nchini (TAEC) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA), wamezindua mkakati wa kiusalama unaolenga kudhibiti nyenzo za nyuklia na vifaa vyenye mionzi visitumike kwa madhumuni ya kihalifu .

Tume ya Nguvu za Atomu nchini (TAEC) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA), wamezindua mkakati wa kiusalama unaolenga kudhibiti nyenzo za nyuklia na vifaa vyenye mionzi visitumike kwa madhumuni ya kihalifu wakati wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika nchini mwaka 2027.


Hayo yamesemwa  Jumatatu, Agosti 31,2026 na Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Najat Kassim Mohammed, wakati wa ufunguzi wa warsha ya kitaifa ya siku tano inayolenga kuandaa na kutekeleza hatua za usalama wa nyuklia kwa matukio makubwa ya umma.

Profesa Najat amesema kuwa ingawa uwezekano wa kutokea kwa dharura au shambulio la kiusalama linalohusisha nyuklia ni mdogo, madhara yake yanapotokea huwa ni makubwa mno yakiwemo hofu kubwa kwa umma, kuvurugika kwa huduma za kijamii pamoja na mdororo mkubwa wa kiuchumi.


Ameongeza kuwa michuano hiyo ya AFCON 2027 itakayofanyika hapa nchini na nchi za Kenya na Uganda itawaleta pamoja  wachezaji, viongozi, mashabiki na waandishi wa habari duniani, jambo linalohitaji mipango thabiti ya usalama inayozingatia tathmini ya kina ya viashiria vya hatari.


"Usalama wa nyuklia kwenye matukio makubwa kama hili hauwezi kuwa jukumu la taasisi moja pekee. Unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Jeshi la Polisi, mamlaka za forodha, uhamiaji, zimamoto, sekta ya afya na uongozi wa viwanja vya michezo," amesema Profesa Najat.


Tanzania imeelezwa kupiga hatua kubwa kwa kuweka vifaa vya kisasa vya kugundua mionzi kwenye mipaka na maeneo ya kimkakati pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa wa mipakani, hata hivyo, mapungufu madogo yaliyopo yatafanyiwa kazi ili kuendana na vigezo vya kimataifa vya IAEA.

Kwa upande wake, Mtaalamu kutoka IAEA, Lacina Saro amesema kuwa maandalizi ya usalama wa nyuklia ya kiwango hiki yanapaswa kufanywa kwa umakini mkubwa, kufanyiwa majaribio ya kutosha na kutekelezwa kwa kujiamini na timu za kitaifa zilizofundishwa vizuri.


Saro aliongeza kuwa warsha hiyo ni muendelezo wa msaada wa IAEA ambapo mnamo Aprili 2025 watalaamu kutoka shirika hilo walifanya tathmini ya mahitaji ya Tanzania na Julai mwaka jana ujumbe wa wataalamu wa Tanzania ulitembelea nchi ya Morocco kujifunza kwa vitendo namna mifumo hiyo inavyofanya kazi.

Alifafanua kuwa katika kipindi cha mafunzo hayo,washiriki hawatasikiliza mihadhara tu, bali wataingia viwanjani kufanya mazoezi ya vitendo ya ugunduzi wa mionzi, upekuzi, utambuzi wa kengele za hatari  na jinsi ya kukabili vifaa hatarishi kwenye uwanja wa michezo.

Warsha hiyo inatarajiwa kuhitimishwa kwa zoezi kubwa la uwanjani litakalofuatiwa na uandaaji wa mpango kazi wa kitaifa wa utekelezaji utakaokabidhiwa kwa serikali ya Tanzania kwa usimamizi wa karibu wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Usalama wa Nyuklia cha IAEA, Elena Bubo.


Naye Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia na Huduma za Ufundi wa TAEC,Dk.Remigius Kawala amesema kitaalamu teknolojia ya nyuklia ina uwezo wa kutumika kwa manufaa makubwa sana lakini pia inaweza kutumika katika njia zisizo za manufaa na kusababisha hatari,hofu na kutishia usalama.

Mifano michache inaonesha matukio ya kigaidi yamekuwa yakilenga michezo duniani ili kupata umaarufu wa kimataifa na kusababisha hofu kubwa kwa jamii.

Mwaka 1972,  kulitokea mauaji ya Munich, Ujerumani ambapo kikundi cha kigaidi cha Black September kiliwateka na kuwaua wanamichezo 11 wa timu ya taifa ya Israel wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Joto mjini Munich, Ujerumani.

Mwaka 1996, bomu lilitegwa katika bustani ya umma wakati wa michezo ya Olimpiki ya Atlanta, Marekani, na kusababisha vifo na majeruhi kwa watu zaidi ya 100.

Mwaka 2013, wanandoa wa kigaidi walilipua mabomu mawili karibu na eneo la kumalizia la Boston Marathon, Marekani na kuua watu watatu huku wengine zaidi ya 260 wakijeruhiwa.

Pia kuna historia ya mashambulizi ya Paris 2015 ambapo  washambuliaji wa kujitoa mhanga walilenga nje ya uwanja wa mpira wa Stade de France nchini Ufaransa wakati mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Ufaransa na Ujerumani ikiendelea.

Viwanja vya michezo sasa vinatumia teknolojia za kisasa za ukaguzi kwa lengo la kuthibiti matukio ya uhalifu michezoni.


Mwisho