Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bilionea huyu kuingoza CAF kuanzia Ijumaa

Muktasari:

Labda itokee miujiza! Kama mambo yatabakia kama yalivyo, bilionea wa Afrika Kusini kesho Ijumaa atachukua kiti cha urais wa mpira wa miguu barani Afrika, akianzisha safari mpya ya mageuzi ya uendeshaji mchezo huo maarufu.

Labda itokee miujiza! Kama mambo yatabakia kama yalivyo, bilionea wa Afrika Kusini kesho Ijumaa atachukua kiti cha urais wa mpira wa miguu barani Afrika, akianzisha safari mpya ya mageuzi ya uendeshaji mchezo huo maarufu.
Tajiri huyo, Patrice Tlhopane Motsepe, anatarajiwa kuchaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kushika nafasi hiyo baada ya mgombea aliyetarajiwa kuweka upinzani mkubwa, Ahmad Yahya Ahmad kufungiwa kujihusisha na soka kwa miaka miwili, ikiwa ni punguzo la adhabu aliyopewa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) ya miaka mitano.
Punguzo hilo la adhabu lilifanywa na Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) baada ya Ahmad kukata rufaa kupinga adhabu ya Fifa iliyotokana na kutiwa hatiani kwa makosa kadhaa yakiwemo ya kutumia madaraka vibaya na kujihusisha katika mkataba na kampuni ya vifaa vya michezo.
Wagombea wengine wa urais wa CAF, Jacque Anouma wa Ivory Coast na ambaye amewahi kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Fifa, na Augustin Senghor wa Senegal, walifikia makubaliano ya kumuachia Motsepe kiti hicho kilichokuwa kinashikiliwa na Ahmad, ambaye alimuangusha kiongozi wa muda mrefu barani Afrika, Issa Hayatou katika uchaguzi uliofanyika miaka minne iliyopita.
Motsepe ni mfanyabiashara anayejihusisha na madini akitokea kabila la Tswana nchini Afrika Kusini, akiwa muasisi wa kampuni ya African Rainbow Minerals, ambayo inajihusisha na madini ya dhahabu, chuma na platinum.
Mgombea huyo anatarajiwa kulichukua shirikisho likiwa hoi, likielezewa kuwa ni jalala la rushwa na taasisi isiyofanya kazi yenye watu wenye maslahi binafsi.
Motsepe atakuwa raia wa kwanza wa Afrika Kusini kuiongoza CAF, akifuata nyayo za viongozi kutoka Misri, Sudan, Ethiopia, Cameroon na Madagascar.
Tofauti na viongozi wengine walitokea katika vyama vya soka vya nchi, Motsepe amejihusisha na soka kwa kumiliki klabu ya Mamelodi Sundowns, ambayo ilitwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2016.
Kama si mabadiliko ya sheria ya hivi karibuni, shabiki huyo wa klabu ya Barcelona asingeweza kugombea urais kwa kuwa angelazimika kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya CAF kama moja ya masharti ya kuwa rais wa shirikisho hilo.
Bilionea huyo mwenye mafanikio katika biashara ni mtu ambaye soka la Afrika linaweza kumtegemea katika kulifanyia mabadiliko makubwa, akitumia uzoefu wake katika biashara.
Ni mtu mwenye maono na ambaye anaamini Afrika ina uwezo mkubwa na ana mapenzi nayo, akiwa ameshatumia rasilimali zake kuinua mchezo huo nyumbani kwao Afrika Kusini.
“Hakuna mtu barani Afrika ambaye amepoteza fedha nyingi kunizidi. Ni mapenzi ya kipumbavu. Soka barani Afrika lazima liwe bora duniani. Hilo haliwezi kutokea siku moja, lakini hicho ni kipimo cha kile ambacho tutaenda kukifanya kwa miaka michache ijayo. Kwangu kipimo na jinsi matokeo yatakavyokuwa. Huna budi kushinda ndani ya dakika 90,” alisema Motsepe katika hafla ya kuzindua kampeni zake katika ukumbi wa mikutano wa Sandton jijini Johannesburg.
Pamoja na kujulikana zaidi kutokana na kuimiliki klabu ya Mamelodi, Motsepe amejihusisha sana kukuza mpira wa miguu nchini Afrika Kusini, akidhamini ligi daraja la tatu inayoitwa ABC Motsepe.
Kwa maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini, ligi ya ABC-- ambayo ni ya kulipwa kwa kiwango fulani kwa sababu klabu nyingi zinalipa mishahara -- ni mlango wa kutokea kwenda ligi kamilifu ya kulipwa- Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Kuu.
Inahusisha ligi tisa za majimbo zikiwa na klabu 144, ikigusa karibu kila eneo la nchi.
Motsepe amekuwa akiifadhili ligi hiyo iliyopewa jina la baba yake anayeitwa Augustine Butana Chaane Motsepe, bila ya kutegemea kunufaika nayo kifedha tangu aichukue mwaka 2014 kutoka kampuni ya Vodacom.
Pia kuna mashindano muhimu ya shule yanayoitwa Kay Motsepe, ambayo yanahusisha soka na netiboli huku bilionea huyo akiwa ameweka mamilioni ya fedha.

Alianzia kazi ya uanasheria
Mgombea huyo mwenye miaka 59 alianza maisha akiwa mwanasheria, baadaye akahamia katika madini, na sasa yuko katika biashara nyingi.
Jarida la Forbes linakadiria utajiri wake kufikia dola 2.9 bilioni za Kimarekani (sawa na Sh6.68 za Kitanzania).

Maisha ya utotoni
Motsepe alizaliwa Januari 28, 1962 na kukulia Soweto karibu na jiji la Johannesburg.
Baba yae alikuwa mwalimu na baadaye akawa anamiliki duka, ambalo wateja wake wengi walikuwa wafanyakazi katika migodi.
Patrice alimsaidia baba yake katika duka hilo wakati wa likizo, na ilikuwa katika duka hilo ndiko alikojifunza kanuni za biashara.
Baada ya kumaliza elimu ya juu ya sekondari, alihamia nchi jirani ya Swaziland (sasa eSwatini) kuchukua shahada ya sanaa katika chuo kikuu cha taifa hilo dogo.
Baadaye alijiunga na chuo maarufu duniani cha Witwatersrand (au Wits) kilicho katika wilaya maarufu kwa biashara jijini Johannesburg ambako alichukua sheria.
Mwaka 1994, Patrice akawa mtu wa kwanza mweusi kuingia ubia katika kampuni ya sheria ambayo pia ina matawi katika nchi za Kenya, Malawi, Mauritius, Tanzania, Uganda na Zambia.

Katika biashara
Wakati bei ya dhahabu ikipaa mwaka 1997, Motsepe alinunua migodi kadhaa kwa bei ya makubaliano, akijenga msingi wa mafanikio yake.
Katika miaka iliyofuata, alinunua migodo zaidi, kuajiri maelfu ya wafanyakazi katika maeneo ya vijijini ambako kulikuwa na fursa chache za ajira.
Baadaye alijiingiza katika biashara nyingine, ikiwemo bima na huduma za kifedha, majengo, benki na mawasiliano.

Alivyoibadili Mamelodi
Motsepe aliifanyia mageuzi Sundowns, klabu kutoka jiji la Pretoria, hadi kuwa moja ya klabu kumi bora barani Afrika, ikitwaa kombe la Ligi ya Mabingwa na CAF Super Cuo mwaka uliofuata.
Akiutwaa urais, Motsepe atalazimika kukata mawasiliano na klabu hiyo, na hivyo mwanawe wa kiume, Tlhopie, atambadili na kuwa rais wa Sundowns, ambayo imeshatwaa ubingwa wa Afrika Kusini mara kumi.
Patrice pia ni mwanahisa wa klabu ya rugby ya Bulls, akiwa na asilimia 37.

Ana watoto watatu
Ameoana na Precious Moloi-Motsepe, daktari na mfanyabiashara ya mitindo, na ni shemeji wa Rais Cyril Ramaphosa na waziri wa zamani, Jeff Radebe.
Wawili hao wana watoto watatu wa kiume -- Tlhopie, Kgosi na Kabelo -- ingawa habari zao hazijulikani sana kwa kuwa Motsepes anakwepa vyombo vya habari.
Familia hiyo imeunda taasisi ya Motsepe, ambayo hutoa msaada wa kifedha ili kuinua kiwango cha maisha ya maskini nchini Afrika Kusini.