Biashara za chakula zimenoga Uhuru
Muktasari:
- Hali hiyo imefanya maeneo mbalimbali ya uwanja huo kunakofanyika tamasha la Simba Day hii leo, kuonekana yakiwa na shughuli nyingi, huku wafanyabiashara wakihangaika kuhakikisha wanawafikia wateja wao kwa wakati.
UWANJA wa Uhuru umeendelea kuwa na shamrashamra huku wafanyabiashara wa chakula wakionekana kutawala eneo hilo kutokana na idadi kubwa ya watu wanaofika na kuhitaji huduma za vyakula na vinywaji.
Hali hiyo imefanya maeneo mbalimbali ya uwanja huo kunakofanyika tamasha la Simba Day hii leo, kuonekana yakiwa na shughuli nyingi, huku wafanyabiashara wakihangaika kuhakikisha wanawafikia wateja wao kwa wakati.
Wafanyabiashara hao wamekuwa wakitoa huduma za aina mbalimbali, ikiwemo vyakula na vinywaji, jambo linalowafanya mashabiki wa soka waliofika kutopata wakati mgumu wa huduma hiyo.
Baadhi yao wameonekana wakihudumia wateja kwa kasi, hasa nyakati ambazo idadi ya watu uwanjani inaongezeka. Foleni za wateja zimeonekana kwenye baadhi ya maeneo, hali inayoonyesha kuwa biashara ya chakula imekuwa na mwitikio mkubwa.
Kwa upande mwingine, uwepo wa wafanyabiashara hao umeongeza uhai katika uwanja huo, kwani watu waliofika kushuhudia kilele cha Simba Day hawalazimiki kuondoka eneo hilo kutafuta chakula maeneo ya mbali. Huduma zinapatikana uwanjani hapa na kwa urahisi zaidi.