Alikiba asindikizwa na bao la Chama
Muktasari:
- Alikiba, ambaye ni msanii mkuu aliyetumbuiza kwenye tamasha hilo, amekonga nyoyo za mashabiki kwa kuimba nyimbo mbalimbali ikiwemo 'Finale', 'Mnyama' na nyinginezo.
Wakati msanii nyota wa Bongofleva, Alikiba akitumbuiza katika kilele cha tamasha la Simba Day, mkali huyo amesindikizwa na bao la Clatous Chama lililoonyeshwa kwenye runinga iliyokuwa karibu na steji aliyopanda.
Alikiba, ambaye ni msanii mkuu aliyetumbuiza kwenye tamasha hilo, amekonga nyoyo za mashabiki kwa kuimba nyimbo mbalimbali ikiwemo 'Finale', 'Mnyama' na nyinginezo.
Sasa wakati Alikiba akiimba wimbo wa 'Mnyama', screen kubwa ya uwanja ilionyesha picha ya bao la kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama, alilofunga dhidi ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Mei 3 kwenye Uwanja wa Mej Gen Isamuhyo.
Bao hilo la Chama lilikuwa la aina yake, baada ya mchezaji huyo kutumia ustadi wa acrobatic kufunga katika mazingira yaliyowafanya mashabiki wa soka nchini kulizungumzia kwa muda mrefu. Goli hilo lilikuwa miongoni mwa matukio yaliyoifanya dabi hiyo kuwa gumzo, huku picha na video zake zikisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.
Ubora wa bao hilo haukuishia Tanzania, kwani liliingia pia kwenye mijadala ya kimataifa baada ya kuhusishwa na tuzo ya FIFA Puskás Award, tuzo inayotolewa kwa bao bora zaidi kwa kuzingatia ubora na mvuto wake.
Hivyo, kuonyeshwa kwake kwenye screen wakati wa kuliongeza uzito wa burudani hiyo na kuwafanya mashabiki kukumbushwa moja ya matukio yaliyowahi kuwapa furaha katika dabi.
Kwa upande wa Alikiba, ujio wake Simba Day umelipa tamasha hilo sura nyingine kutokana na ukubwa wa jina lake katika muziki wa Tanzania. King Kiba ametumia jukwaa hilo kuwapagawisha mashabiki kwa mfululizo wa nyimbo zake, huku 'Mnyama' ikiwa miongoni mwa nyimbo zilizobeba ujumbe maalumu kwa mashabiki wa Simba kutokana na namna ilivyotumika katika shughuli mbalimbali za klabu.