Barker anataka taji la Ngao ya Jamii 2026
Muktasari:
- Barker amesema maandalizi yao yamefanyika kwa kiwango cha kiwango cha kutosha na kwamba kikosi chake kimejiandaa kuchukua taji hilo ili waanze vizuri hesabu za msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Kocha wa Simba Steve Barker amesema kikosi chake kipo tayari kuelekea mechi ya ngao ya Jamii dhidi ya Yanga akisema wanalitaka taji hilo la mapema.
Barker amesema maandalizi yao yamefanyika kwa kiwango cha kiwango cha kutosha na kwamba kikosi chake kimejiandaa kuchukua taji hilo ili waanze vizuri hesabu za msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
"Mpango wetu ni kushinda,ni wazi tulitengeneza nafasi hii baada ya kushinda ubingwa wa Shirikisho CRDB, kama timu tumepata haki hii ya kushiriki mchezo huu wa Ngao ya jamii, tumefanya maandalizi mazuri na kujiweka tayari kuanza msimu kwa hesabu chanya," amesema Barker.
"Tuna nafasi ya kupata mafanikio ya mapema kwa kuchukua taji hili, Simba SC ni timu ambayo wakati wote ina hesabu za kuchukua mataji, tupo tayari kuanza kulichukua hili la kesho."
Akizungumzia uwepo wa kocha Manqoba Mngqithi ambaye ni raia mwenzake wa Afrika Kusini Barker amesema, anamjua vizuri kocha huyo na kwamba anaamini itakuwa mechi nzuri kwa wao kukutana tena.
"Ndio, kocha Manqoba tunajuana vizuri ni kocha mwenye uwezo mkubwa, amepata mafanikio makubwa wakati akifundisha pale nyumbani, ni furaha kwangu kumuona yupo hapa," amesema.
"Utakuwa mchezo mzuri tunaamini kwamba itakuwa mechi ambayo itakwenda kutupa nafasi ya kuziongoza timu hizi mbili kubwa wote tukitoka taifa moja."
Beki wa Simba, Nickson Kibabage amesema wao kama wachezaji wako tayari kwa mchezo huo wakitambua umuhimu wa kupata matokeo mazuri yatakayowapa taji lingine.
"Tumefanya maandalizi mazuri na Leo tutamalizia, wachezaji tupo tayari kwa mechi hii, haitakuwa rahisi kwa kuwa tunakutana na timu ngumu lakini tumejipanga kushinda," amesema.