Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kisa mwalimu mashabiki Simba waja juu

Muktasari:

  • Alfajiri ya leo, Yanga imetangaza rasmi kupitia mitandao yake ya kijamii kukamilisha usajili wa Mwalimu kwa mkopo kutoka Wydad Casablanca ya Morocco.

Baada ya Yanga kumtambulisha mshambuliaji Selemani Mwalimu kuwa mchezaji wake mpya, baadhi ya mashabiki wa Simba wameulalamikia uongozi wa klabu hiyo, wakidai umekuwa ukifanya mambo ya ajabu.

Alfajiri ya leo, Yanga imetangaza rasmi kupitia mitandao yake ya kijamii kukamilisha usajili wa Mwalimu kwa mkopo kutoka Wydad Casablanca ya Morocco.

Hatua hiyo imeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka, kutokana na ukweli kwamba kabla ya Yanga kutangaza usajili huo, mahasimu wao Simba walikuwa tayari wametangaza kumalizana na mshambuliaji huyo.

Usajili wa Mwalimu kwa Simba ulitangazwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, wakati wa tamasha la Simba Day lililofanyika Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Shabiki maarufu anayefahamika kwa jina la Mchome Mapovu amesema kitendo hicho kimewaacha mashabiki wa Simba wakiwa wamevunjika moyo, akidai taarifa zinazotolewa na uongozi zimekuwa zikiwapotosha.

“Ahmed anatoa habari za uongozi, anawadanganya Wanasimba. Yanga wametupiga panapouma.

“Ukiangalia hata usajili wetu hauzingatii mahitaji. Tumesajili mawinga watano, mshambuliaji mmoja. Sio sawa,” amesema Mchome.

Naye shabiki anayefahamika kwa jina la Mzee Said amedai uongozi wa Simba haujui unachokifanya, tofauti na Yanga ambao amesema wanafanya mambo yao kwa uhakika.

“Huyu anayetubeba naye ameenda Yanga, halafu mtu anatangaza fedha ziko kwenye akaunti.

“Asubuhi bosi wangu kanipigia simu ananiambia Selemani Mwalimu kaenda Yanga. Nikamwambia hiyo ni AI. Haya, kesho tunaenda kukutana na Yanga, tunaenda kufeli.

“Mimi namwomba Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, atusaidie akiwa kama kiongozi, awaambie viongozi wa Simba wasitufanyie haya mambo,” amesema Mzee Said.

Kwa upande wake, shabiki mwingine anayefahamika kwa jina la Kisugu amesema aliwahi kutoa taarifa kwamba viongozi wa Yanga walikwenda Morocco kumfuatilia Mwalimu, lakini hakueleweka na baadhi ya mashabiki.

“Nilishasema viongozi wa Yanga walienda Wydad kumfuata Sele, lakini hamkunielewa," amesema shabiki huyo na kuongeza:

“Kwanza niwapongeze Dar es Salaam Yanga Africans kwa kumpata mchezaji mzuri. Pia niwapongeze viongozi wa Simba kwa kutofuata siasa za mpira. Unapoenda kusajili washambuliaji nane, hizi sasa ndiyo siasa za mpira.”

Ameongeza: “Sisi tulishaacha siasa za mpira. Mnamkumbuka Victor Costa? Alifanya mazoezi Yanga, akasajiliwa Simba. Simba tumeacha siasa za mpira.”

Msimu uliopita, Mwalimu aliichezea Simba kwa mkopo kutoka Wydad Casablanca na kufanikiwa kufunga mabao 10.