Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzimu mpya wa soka Nyanda za Juu Kusini

Muktasari:

  • Hii ni kutokana na idadi ya timu za Ligi Kuu na zile za madaraja ya chini yake kuendelea kupungua katika Kanda hiyo yenye mikoa saba, ambapo Mbeya ilikuwa tegemeo kwa kuwa na kituo cha kuziona Yanga na Simba.

KUSHUKA daraja kwa Tanzania Prisons kumewashtua wadau na mashabiki wa soka Nyanda za Juu Kusini, huku wengi wakijawa na hofu huenda kanda hiyo kwa miaka ijayo kukosa uhondo wa Ligi Kuu.

Hii ni kutokana na idadi ya timu za Ligi Kuu na zile za madaraja ya chini yake kuendelea kupungua katika Kanda hiyo yenye mikoa saba, ambapo Mbeya ilikuwa tegemeo kwa kuwa na kituo cha kuziona Yanga na Simba.

Kwa historia ya miaka takribani saba nyuma, Kanda hiyo ilikuwa ikijivunia kuwa na idadi kubwa ya timu Ligi Kuu, Championship na First League, lakini kwa sasa hali inazidi kuwa ngumu kwa kuporomoka kwa soka.

Kwa sasa ni Mbeya City pekee iliyobaki Ligi Kuu, ambapo kwa msimu ujao wa 2026-2027, mashabiki na wadau wa soka watasafiri kutoka Iringa, Njombe, Songwe, Katavi na Rukwa kuja jijini Mbeya kuziona Yanga na Simba.

Makala hii inakuletea orodha na timu zilizowahi kutamba Ligi Kuu, ambapo baadhi zimepotea na kubaki historia, huku nyingine zikiendelea kujikongoja bila mwelekeo wowote na kuibua sintofahamu ya vipaji vya vijana katika ukanda huo.


VIPAJI VIPO

Ukitaja Nyanda za Juu Kusini kwa timu za Ligi Kuu tangu miaka ya nyuma wachezaji kutoka Kanda hiyo walikuwa wengi na ndio walitangaza mikoa yao kupitia vipaji mguuni.

Wachezaji kama Shadrack Nsajigwa, Wily Martin ‘Garikubwa’, Antony Mwamlima, Tais Mwalyoga, Suleiman Mwakenya, Godwine Aswile, Ivo Mapunda, John Mwansasu, John Joseph ‘JJ’ na Fred Mwailenge.

Nyota hao licha ya kungâ’ara na timu za mikoa hiyo, pia walizichezea timu kadhaa nchini zikiwamo Simba, Yanga na timu za Taifa kwa nyakati tofauti na kufanya Kanda hiyo kusifika kwa vipaji.

Ukiachana na mastaa wa zamani, baadaye walichipukia nyota wengine walifanya vizuri na wapo wanaoendelea kutesa Ligi Kuu hadi sasa katika timu tofauti, ikiwa ni Beno Kakolanya, Ditram Nchimbi, Peter Mwangosi, Deus Kaseke, David Kameta ‘Duchu’, Mpoki Mwakinyuke, Peter Mapunda, Marcel Kaheza na Mpoki Mwakinyuke.

Pia wapo ambao wanaendelea kujitafuta kusaka ndoto zao kupitia soka kutoka mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini japokuwa sehemu ya kutokea imeonekana kuwa ngumu kutokana na timu kushuka daraja.


TUKUYU STARS

Timu hii kongwe ya mkoani Mbeya kwa sasa imebaki historia kutokana na kushuka kwao daraja na kupoteana katika medani za soka na waliokuwa wakiitegemea kuzima ndoto zao.

Tukuyu Stars iliyopanda Ligi Kuu mwaka 1985 (zamani Ligi Daraja la Kwanza) imepotea kwa rekodi ya ubingwa wa mwaka 1986, kwa sasa haijulikani inacheza ligi gani na si tegemeo tena kwa wadau na mashabiki wa mpira.

Katika kipindi chake, timu hiyo ilitesa na mastaa wengi ambao baadaye walijiunga na timu nyingine wakiwamo Mbwana Makata, Suleiman Mwankenja, Kelvin Haule, Ally Kimwaga, Salum Kusi, Hussein Zito na Simon Mwasakyeni.


MAJIMAJI

Kwa miaka ya zamani ilifahamika kuwa ‘Wanalizombe’ ambapo mwaka 1977 ndio ilianzishwa rasmi na mwaka 1980 ikapanda Ligi Kuu (Ligi Daraja la Kwanza), ambapo ilikuwa yenye mageuzi makubwa kwenye soka nchini.

Kwa muda mfupi, timu hiyo ya mkoani Ruvuma iliyokuwa chini ya mwanzilishi, Dk Raulence Gama, ilifanya makubwa na kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano kwa miaka miwili mfululizo, mwaka 1985 na 1986, kisha kufanya hivyo tena mwaka 1998.

Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, mwaka 2007 ilishuka daraja baada ya serikali ya Mkoa wa Ruvuma kujitoa kwenye uendeshaji na kuwaachia wanachama, ambapo 2009 ikarejea Ligi Kuu na kudumu misimu miwili hadi 2011 iliposhuka tena.

Baadaye timu hiyo ilirejea Ligi Kuu msimu wa 2014-2015 ikionesha soka la ushindani lakini haikuwa na safari ndefu baada ya kujikuta ikirudi tena Championship msimu wa 2017-2018.

Hadi sasa timu hiyo imepoteana licha ya uwepo wa juhudi za baadhi ya wadau wa soka huko Songea kupambana kuirejesha huku suala la ukata likitajwa kukwamisha baadhi ya mipango yao.


NJOMBE MJI

Timu hiyo iliyopanda kwa mzuka mwingi na kuwapa raha mashabiki mkoani Njombe, hawakuwa na muda mrefu wa kucheza Ligi Kuu baada ya kushuka daraja msimu mmoja tu waliodumu kwenye michuano hiyo.

Njombe Mji ilipanda Ligi Kuu msimu wa 2016-2017 na kuamsha matumaini kwa wakazi mkoani humo wakiamini burudani za Simba na Yanga kuziona kwa macho, lakini raha hiyo haikudumu zaidi.

Hata vijana waliokuwa wakijiandaa kuonekana kupitia vipaji vyao ili kuitumikia timu hiyo na baadaye kutoka, mambo hayakwenda vizuri kutokana na matokeo ya kushuka kwa chama hilo na hadi sasa haijulikani itarejea lini.


LIPULI

‘Wanapaluhengo’ hao walikuwa moto sana kwani hata timu kubwa za Yanga na Simba haziwezi kusahau makali yao kutokana na upinzani walioupata kwa timu hiyo ya mkoani Iringa.

Lipuli iliyokuwa na baadhi ya mastaa wakiwamo Seif Karihe, Paul Nonga, Daruwesh Saliboko, Wiliam Lucian ‘Gallas’, Novatus Lufunga, Miraji Athuman na Zawadi Mauya, ilikuwa ya moto wa kuotea mbali.

Ikicheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu, ilifanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho (kwa sasa CRDB) ilipoifumua Yanga mabao 2-0 kabla ya kufungwa na Azam iliyoingia nayo fainali.

Kwa sasa ‘Wanapaluhengo’ hao hawajulikani walipo licha ya mara kadhaa wadau na baadhi ya viongozi kuitaja kwenye matukio tofauti wakitamba watairudisha kwa njia nyingine.


TANZANIA PRISONS

Baada ya kudumu Ligi Kuu kwa miaka 15, timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza nchini ilishuka daraja msimu uliopita 2025-2026 kupitia play off baada ya kupoteza kwa jumla ya mabao 4-1 dhidi ya Polisi Tanzania.

Kabla ya timu hiyo kushuka daraja, iliifanya Mbeya kuwa na timu mbili za Ligi Kuu ikiungana na Mbeya City ambayo ndio imebaki kwa sasa katika mashindano hayo na sasa ndio inatazamwa na mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini.

Kwa miaka mitano nyuma, Mkoa wa Mbeya ulifikisha timu tano Ligi Kuu ikiwa ni Prisons, Mbeya City, Ihefu (kwa sasa Singida Black Stars), Mbeya Kwanza na KenGold ambayo ipo Championship.


KILIO MIKOA HII

Wakati timu zikiendelea kupungua Ligi Kuu, ipo baadhi ya mikoa haijaonja ladha ya michuano na kufifisha ndoto za vijana wanaotegemea kufikia malengo yao kupitia soka.

Mikoa ya Songwe, Katavi na Rukwa bado giza limetanda na hadi kuziona Simba na Yanga lazima wajazane kwenye vibanda umiza, tofauti na hapo watabaki kusikia uhondo huo.

Songwe tangu ilipoundwa mwaka 2012, haijawahi kupata japo timu ya First League, huku Katavi iliyofanya hivyo kwa kuwa na Malimao FC haikudumu baada ya mmiliki wake kuipiga bei na sasa ni Magenet ya Dar es Salaam.

Rukwa tangu iliposhuka daraja Ujenzi FC miaka ya 1994, haijawahi kuwa na timu nyingine yenye kuamsha na kuchangamsha soka ikisubiri timu kutoka mikoa ya jirani iweze kutumia uwanja wa Nelson Mandela.


KAULI ZA WADAU

Jafari Haule mkazi wa Songea, anasema kwa mwenendo ulivyo kwenye soka kipindi hiki huenda miaka mitatu ijayo kanda hiyo ikapoteana kwenye medani za soka nchini kwani hali si shwari.

“Zamani kulikuwa na wadau wenye kujitolea kuzisapoti timu, lakini kwa sasa haionekani hiyo nguvu wala ushawishi kutoka kwa viongozi, kimsingi inahitaji nguvu ya pamoja kurejesha soka letu,” anasema Haule.

Naye Uhuru Mwampashi mkazi wa Songwe anasema kwa sasa ni kilio sana kwa mkoa huo wenye uchumi na lango la SADC kukosa timu ya Ligi Kuu akieleza kuwa si suala la mtu mmoja bali wadau wote kushirikiana. “Tumepakana na nchi jirani kama Zambia, Malawi na Congo, tungeweza kufanya vizuri hata katika shughuli zetu za uchumi kuweza kupiga hatua kupitia michezo kama tungekuwa na timu ya Ligi Kuu,” anasema Mwampashi.


FA NA MIKAKATI

Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani Songwe (Sorefa), Jacob Mwangosi anasema ndoto zao ni kuwa na timu ya Ligi Kuu na haijalishi itapatikanaje aidha kwa kunuanua au kupandisha wenyewe.

“Ni kitu kinatuumiza sana kichwa kama wadau na chama kwa ujumla, tunaendelea kuwasiliana na watu kadhaa wapenda soka na maendeleo kuona tunakamilishaje, lakini mkakati ulishaanza,”  anasema Mwangosi.

Naye Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Katavi, Alfred Basu, anasema kiu yao ni kuwa na timu za madaraja ya juu ili kuhamasisha vijana na kuamsha uchumi kupitia sekta ya michezo.

“Tatizo Katavi siyo kuwa na timu kwakuwa wadau wapo na wanatamani kuona soka, lakini changamoto kubwa ni viwanja, tulipata mdau akanunua timu ya Tunduru Korosho lakini akawaza ataiweka wapi?

“Tumesikia mpango mkakati wa Manispaa ya Mpanda kutenga bajeti kwa ajili ya uwanja wa Halmashauri, huenda tukikamilisha hilo, mpira utaanza kuonekana rasmi hapa Katavi,”  anasema Basu.