Prime
Bangala: Huku Azam raha sana
KIUNGO mpya wa Azam FC, Yannick Bangala Litombo muda mwingi ameonekana kuwa na furaha na wachezaji wenzake kisha akafunguka Azam kuna raha sana.
Bangala ambaye amesajiliwa na Azam FC akitokea Yanga alisema kama kuna kitu kimempa faraja ni mapokezi mazuri ambayo amepewa na wachezaji wenzake, benchi la ufundi na hata viongozi wa klabu.
Bangala alisema mapokezi hayo yamempa furaha ya moyo wake wakati wote amejikuta na kiu ya kutamani kucheza haraka ili aisaidie timu hiyo.
“Nina furaha ndio kama unavyoona nimepokelewa vizuri na wachezaji wenzangu na hata makocha naona kila kitu kipo sawa kabisa,” alisema Bangala na kuongeza;
“Maisha yamekuwa rahisi hapa kwa kuwa pia nimekutana na marafiki zangu Feisal (Salum) tulikuwa naye Yanga na sasa tuko hapa lakini pia ndugu yangu Mbombo (Idris) naye tunajuana vizuri amefurahi kuona najiunga na Azam.
“Kila kitu kipo sawa kiu yangu ni kuona naanza kucheza nataka nianze kucheza ili niisaidie timu yangu mpya hii ni klabu yenye kila kitu sisi wachezaji ni jukumu letu sasa kulipa mazuri kwa ajili ya uwekezaji kama huu.”
Bangla alitua Azam baada ya kuuzwa na Yanga aliyoitumikia kwa misimu miwili mfululizo na kutwaa nayo mataji saba tofauti ikiwamo mawili ya Ligi Kuu Bara, ASFC na Ngao ya Jamii sambamba na Kombe la Mapinduzi.
Awali kabla ya kupata dili hilol Yanga ilipanga kumtoa kwa mkopo kwenye kwenye Ligi Kuu kutokana na kukamilisha idadi ya wachezaji 12 wanaohitajika kwa mujibu wa kanuni, ndipo Azam itamnyakua kuchukua nafasi ya Isah Ndala.