Bakari Shime ataja sababu kichapo
Muktasari:
- Shime amesemsa Tanzania ilikuwa imeanza kuonyesha kiwango kizuri na kupata ujasiri baada ya kusawazisha mchezo, lakini bao la pili la Brazil lilibadilisha kabisa hali ya kikosi hicho na kuanza kuathiri namna wachezaji walivyotekeleza majukumu yao uwanjani.
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 20, Bakari Shime amesema sababu zilizoifanya timu hiyo kukubali kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Brazil katika mchezo wa kwanza wa Kundi B wa Kombe la Dunia U-20 ni pamoja na kuruhusu bao la pili liliwatoa mchezoni baada ya awali kuwa na hali nzuri ya kujiamini.
Shime amesemsa Tanzania ilikuwa imeanza kuonyesha kiwango kizuri na kupata ujasiri baada ya kusawazisha mchezo, lakini bao la pili la Brazil lilibadilisha kabisa hali ya kikosi hicho na kuanza kuathiri namna wachezaji walivyotekeleza majukumu yao uwanjani.
“Goli la pili lilianza kuifanya timu itikisike kwa sababu timu ilikuwa tayari imeanza kujiamini nzuri, lakini lile goli la pili kidogo likaanza kuturudisha nyuma,” amesemsa Shime.
Kocha huyo pia amekiri kuwa kulikuwa na makosa ya kiufundi katika safu ya ulinzi, hasa kwenye bao la tatu, akieleza kuwa Tanzania ilipoteza mpangilio baada ya kipa kuanzisha mpira ambao ulirudi kwa Brazil kutokana na mabeki kuchelewa kusogea mbele.
“Tulikuwa na huo mpira sisi, golikipa akapiga mpira lakini safu ya ulinzi ilibakia chini, wamechelewa kwenye kuondoka na matokeo yake mpira umerudi na tumeruhusu goli.”
Shime aliongeza kuwa pamoja na kichapo hicho, Tanzania haipaswi kukata tamaa, badala yake wanapaswa kutumia mchezo huo kama somo la kurekebisha makosa yaliyobainika kabla ya michezo miwili iliyobaki.
Mfungaji wa bao la Tanzania, Winifrida Gerald amesemsa kichapo hicho hakiwezi kuwa sababu ya Tanzania kukata tamaa, akisisitiza kuwa bado wana michezo miwili ya kuwania pointi katika hatua ya makundi.
“Pia hii sio mwisho. Tutaendelea kupambana, michezo yetu bado ipo miwili. Tutaendelea kupambana michezo inayokuja tuweze kupata pointi,” amesemsa Winifrida.
“Kila mmoja hapo atamsikiliza mwalimu kwenye nafasi yake anamwelekezaje. Pia tutakuja kiukubwa kuja kucheza mchezo wetu mechi na England,” amesema.
Baada ya mechi hiyo kesho Septemba 08, Tanzania itaminyana na England kwenye mechi ya pili ya kundi B itakayopigwa Uwanja wa Stadion Miejski saa 1 kamili usiku.