Tanzanite yajipanga Kombe la Dunia
Muktasari:
- Tanzanite Queens itaanza safari ya kihistoria Jumamosi, Septemba 5, 2026 kwa kuvaana na Brazil katika mchezo wa Kundi B utakaochezwa Uwanja wa Miejski Bielsko-Biaa, huku Shime akisisitiza maandalizi na utayari wa kikosi chake.
KOCHA Mkuu wa Tanzanite Queens, Bakari Shime amesema kikosi kipo tayari kuandika historia katika Fainali za Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 20 nchini Poland, huku akitambua ukubwa wa kazi iliyo mbele yao dhidi ya Brazil.
Tanzanite Queens itaanza safari ya kihistoria Jumamosi, Septemba 5, 2026 kwa kuvaana na Brazil katika mchezo wa Kundi B utakaochezwa Uwanja wa Miejski Bielsko-Biaa, huku Shime akisisitiza maandalizi na utayari wa kikosi chake.
Shime alisema safari ya kuelekea Poland ilikuwa ndefu, lakini kubwa zaidi ni kuhakikisha wachezaji wanafika salama, wanapata muda wa kujiandaa na kuingia uwanjani wakiwa tayari kwa vita ya kwanza.
“Safari itachukua zaidi ya saa 15. Ninatarajia tutafika salama na mara moja kuanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu wa kwanza utakaochezwa Jumamosi,” alisema Shime.
Tanzania ipo Kundi B pamoja na Brazil, England na Canada, ikiwa ni kundi lenye changamoto kubwa kwa timu hiyo inayoshiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, nahodha Diana Mnally, alisema Tanzanite Queens haijaenda Poland kwa ajili ya kutimiza idadi ya washiriki, bali kupambana na kutafuta matokeo mazuri.
“Tunafahamu ukubwa na umuhimu wa mashindano haya. Makocha wetu wametuandaa vizuri kisaikolojia na kimwili kwenda kushindana kwa ushindi,” alisema Mnally.
Tanzanite Queens inakwenda Poland ikiwa na kumbukumbu tamu ya namna ilivyopata tiketi ya fainali hizo baada ya kuifanya mabadiliko makubwa kwenye hatua ya mwisho ya kufuzu dhidi ya Cameroon.
Timu hiyo ilipoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 3-1 ikiwa Younde nchini Cameroon, lakini ilipindua meza katika mchezo wa marudiano uliochezwa New Amaan Complex, Zanzibar, kwa kushinda 2-0 na kusawazisha jumla ya mabao 3-3, matokeo yaliyowapa tiketi ya kucheza Kombe la Dunia kwa bao la ugenini.
Baada ya kumalizana na Brazil, Tanzanite Queens itakutana na England Septemba 8, 2026 na kumaliza mechi za Kundi B dhidi ya Canada Septemba 11, 2026. Mechi zote za Tanzanite Queens katika hatua hiyo zimepangwa kuchezwa saa 3:00 usiku kwa saa za Tanzania. Fainali za Dunia U-20 zinafanyika Poland kuanzia Septemba 5, 2026 hadi Septemba 27, 2026.