Mambo matano yaliyoiangusha Twiga Stars WAFCON
Muktasari:
- Mashindano hayo yanayoendelea kufanyika jijini Rabat nchini Morocco, Tanzania imekusanya pointi tatu na kumaliza nafasi ya nne huku Ivory Coast ikimaliza kinara kwa pointi saba na Afrika Kusini iliyofuzu ikiwa nafasi ya pili kwa pointi sita.
SAFARI ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Twiga Stars katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 imefikia tamati baada ya kucheza mechi tatu za Kundi B ikiwa mkiani.
Mashindano hayo yanayoendelea kufanyika jijini Rabat nchini Morocco, Tanzania imekusanya pointi tatu na kumaliza nafasi ya nne huku Ivory Coast ikimaliza kinara kwa pointi saba na Afrika Kusini iliyofuzu ikiwa nafasi ya pili kwa pointi sita.
Ni matokeo yanayoacha maumivu kwa mashabiki, hasa ukizingatia kwamba kabla ya mchezo wa mwisho dhidi ya Ivory Coast, Twiga Stars ilikuwa na nafasi ya kuandika historia kwa kutinga robo fainali kwa mara ya kwanza.
Lakini, nini hasa kimeiangusha Twiga Stars? Mwanaspoti imekuchambulia mambo matano yaliyoigharimu timu hiyo kushindwa kufanya vizuri WAFCON.
NIDHAMU ILIGHARIMU
Moja ya eneo lililoigharimu Twiga Stars kwenye michuano hii ni nidhamu.Kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Afrika Kusini Tanzania ilicheza kwa kuwaheshimu mabingwa watetezi ambalo lilikuwa faida kubwa.
Lakini mbili mfululizo dhidi ya Burkina Faso na Ivory Coast, Tanzania ni kama hakukuwa na nidhamu nzuri ya kuzuia na kushambulia.
Hata kadi nyekundu aliyopewa winga, Hasnath Ubamba kwenye mechi ya pili dhidi ya Burkina Faso iliathiri kwa kiasi kikubwa kwenye mchezo wa mwisho kutokana na ubora wake.
Adhabu hiyo haikuathiri mechi hiyo pekee, bali ilimnyima nafasi ya kucheza dhidi ya Ivory Coast katika mchezo wa mwisho wa kundi. Kutokuwepo kwake kulionekana wazi kwenye safu ya ushambuliaji.
Ni pigo ambalo lilipunguza chaguo la benchi la ufundi katika mechi ya muhimu zaidi ya mashindano.
MORALI
Baada ya kuifunga Afrika Kusini na kuandika historia ya ushindi wa kwanza wa Tanzania katika WAFCON, wengi waliamini Twiga Stars ilikuwa imepata morali kubwa.
Hata hivyo, ushindi kuwa chanzo cha mwendelezo wa matokeo. Timu ilishindwa kutumia ari hiyo dhidi ya Ivory Coast na kujikuta ikiruhusu wapinzani kutawala sehemu kubwa ya mchezo.
Mashindano mafupi kama WAFCON yanahitaji uwezo wa kushinda au kupata matokeo mfululizo. Hilo ndilo lililofanywa na Ivory Coast, huku Tanzania ikishindwa kuendeleza kasi yake.
MAKOSA YA KIULINZI
Ivory Coast haikutengeneza nafasi nyingi kuliko Tanzania, lakini ilionyesha tofauti kubwa katika kuzitumia.
Bao la kwanza la Nsira Ouedraogo lilitokana na uzembe wa kuacha nafasi katikati ya ulinzi dakika chache kabla ya mapumziko. Bao hilo lilibadili mpango mzima wa mchezo.
Baadaye, penalti iliyofungwa na Ines Konan iliipa Ivory Coast utulivu wa kucheza kwa kujiamini zaidi na hilo ndilo lilitokea kwa Stars.
UMALIZIAJI WA NAFASI
Ingawa Twiga Stars ilifanikiwa kufunga bao katika kila mchezo wa hatua ya makundi, bado ilionyesha mapungufu makubwa kwenye eneo la mwisho.
Washambuliaji walishindwa kutumia baadhi ya nafasi walizozipata, hasa kipindi cha pili dhidi ya Ivory Coast walipokuwa wakitafuta bao la kusawazisha.
Tofauti ya timu kubwa na zinazojifunza mara nyingi huonekana kwenye uwezo wa kutumia nafasi chache zinazopatikana. Ivory Coast ilitumia nafasi zake mbili muhimu kupata mabao mawili, wakati Tanzania ililazimika kusubiri hadi dakika za nyongeza kupata bao lake kupitia penalti ya Diana Msewa.
UZOEFU UMEWAANGUSHA
Twiga Stars imeendelea kukua, lakini bado ipo katika hatua ya kujifunza kucheza mashindano makubwa kama Wafcon
Ivory Coast ilionyesha utulivu mkubwa ilipokuwa inaongoza, ikadhibiti tempo ya mchezo, ikapunguza kasi pale ilipohitajika na ikawalazimisha Tanzania kutumia nguvu nyingi bila mafanikio.
Ikumbukwe hii ni mara ya tatu Tanzania inacheza mashindano ya WAFCON, mara mbili mfululizo iliishia makundi ikiwa haijachshinda mchezo wowote.
Mwaka 2010 ilishia makundi ikiwa haina pointi hata moja ikipoteza mechi zote tatu dhidi ya Afrika Kusini kwa mabao 2-1, Mali 3-1 na dhidi ya Nigeria ikipokea kichapo cha mabao 3-0.
Mwaka 2024 ikamaliza kundi C ikiwa mkiani na pointi moja, Ilianza kwa kupoteza bao 1-0 dhdi ya Mali kisha ikatoka sare ya 1-1 dhidi ya Afrika Kusini na kumaliza makundi ikipokea kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Ghana.
Ukiangalia matoleo yaliyopita utagundua mwaka huu timu hiyo imeimarika zaidi tofauti na miaka iliyopita lakini uzoefu kwenye mashindano hayo ndio uliwaangusha.
Licha ya kuaga mapema, Twiga Stars imeondoka Morocco ikiwa imeandika historia. Ushindi dhidi ya Afrika Kusini umeonyesha kwamba Tanzania inaweza kushindana na vigogo wa soka la wanawake barani Afrika.
Timu pia imefunga mabao katika mechi zote tatu za hatua ya makundi, jambo linaloonyesha maendeleo kwenye safu ya ushambuliaji ukilinganisha na ushiriki uliopita.
Mafanikio hayo yanapaswa kuwa msingi wa kujenga kikosi kitakachokuwa na ushindani zaidi katika mashindano yajayo.
Benchi la ufundi lina kazi ya kuboresha maeneo yaliyodhihirika kuwa na udhaifu. Ulinzi unahitaji kuwa makini zaidi, safu ya ushambuliaji inapaswa kuongeza makali ya kutumia nafasi, huku nidhamu ya wachezaji ikiwa eneo lisilopaswa kuangalia kwa jicho la pili.
Pia, kuongezeka kwa idadi ya mechi za kimataifa za kirafiki kutawasaidia wachezaji kupata uzoefu wa kukabiliana na presha ya mashindano makubwa.
Ingawa ndoto ya robo fainali imeyeyuka, safari ya Twiga Stars nchini Morocco imeonyesha wazi kuwa Tanzania haipo tena katika kundi la timu zinazokwenda kushiriki tu. Sasa inaweza kushindana na kushinda dhidi ya mataifa makubwa.
Kinachohitajika ni kujifunza kutokana na makosa yaliyojitokeza mwaka huu na kuyaweka sawa kabla ya mashindano yajayo. Ikiwa hilo litafanyika, basi kuondolewa kwa WAFCON 2026 kutabaki kuwa somo muhimu lililoweka msingi wa mafanikio makubwa zaidi katika siku zijazo.
MSIKIE KOCHA
Kocha wa Stars, Bakari Shime anasema “Hali ya wachezaji ilikuwa mbaya baada ya kuruhusu bao na imeonekana mshambuliaji kiongozi Opah alishindwa kupafomu, tulipungua uwezo na kumpeleka Enekia acheze pale, tulifanya mabadiliko ya lazima lakini yalishindwa kutupa faida, wachezaji wamefanya kazi kubwa kwa sababu walicheza kwenye sehemu ngumu,”
“Tutakwenda kujifunza kulingana na makosa, namna gani tumeweza kujiweka kwenye hali ngumu ni kosa tulilifanya lakini ushindani wa mechi hadi mechi ulikuwa mzuri kikubwa tumejifunza na tuwape pole mashabiki wetu.”