Ally Mwazoa; promota wa Mwakinyo mwenye simulizi tamu, chungu za ndondi-2

KATIKA sehemu iliyopita, Mwazoa alizungumza mengi kuhusu upromota wa ngumi na safari ya Mwakinyo kuitwa Ikulu, hapa anashuka mambo mengine mengi... endelea.
Pambano la Tinampay
Mwazoa anasema pambano la Mwakinyo dhidi ya bondia wa Ufilipino, Arnel Tinampay alishirikiana na bondioa huyo staa wa Tanzania, ingawa yeye alipata safari na wakamchagua Jay Msangi kuwa msemaji wa pambano.
“Niliporudi nilikuta Msangi ndiye amejipa nafasi ya upromota, lakini kwa kuwa Mwakinyo ni mwanangu ilikuwa lazima nisimame upande wake na mimi ndiye nilimshauri afanye kazi na Msangi.
Anasema alimchagua Msangi kwa kuwa ni promota ambaye anaweza kujenga hoja, hahofii kupatana kwa maslahi mazuri, lakini pia anajua promosheni ya ngumi.
“Nilimwambia Mwakinyo, kwa Msangi shikilia upande huu na huu jihadhari, kwani kwenye ngumi kuna mapromota wa aina mbili, kuna promota wa kumtoa bondia kutoa mchangani hadi kuuzika kimataifa na promota mfanyabiashara.
Anasema kwenye pambano lile, Mwakinyo aliongoza raundi sita za mwanzo na sita za mwisho waligawana na Tinampay, hakupigwa kama baadhi ya watu walivyozungumza.
“Mwakinyo angeweza kushinda pambano lile kwa KO, lakini alikuwa bize na promosheni kuliko maandalizi, hakutulia kujiandaa, lakini pia siku ya pambano, watu wengi waliibuka kuwa wasaidizi wake wa ulingo (second).
Anasema ilibidi kocha wake kutulia pembeni kuwaangalia watu waliojidai kuwa ni wataalamu zaidi ya kocha wake.
“Nilikuwepo nikakaa pembeni kabisa, kuna watu wengi waliibuka kumsecond, pale ulingoni mtu anamwambia piga right, utasema anafahamu kama Hassan ‘ametrain’ right, ila angeachiwa kocha wake akawa huru, angefanya vizuri sana kwani ndiye amemfundisha hadi akashinda Uingereza, anamfahamu vilivyo bondia.”
Udhamini Sportpesa
Mwanzoa anasema kabla ya Mwakinyo kushinda Uingereza, aliunganishwa na mwandishi wa habari Majuto Omary kuhusu kuomba udhamini SportPesa.
“Tulizungumza muda mrefu sana suala hilo na Majuto, Hassan aliposhinda Uingereza mchakato huo ukaanza ukiratibiwa na Majuto mwandishi nguli wa gazeti la The Citizen,” anasema.
Anasema japo yeye Mwanzoa anafahamiana na Tarimba (Abbas), lakini kila kitu kilifanywa na Majuto na wakamshirikisha Mwakinyo.
“Tulipanga kuondoka wote Tanga siku inayofuata baada ya mchakato wa udhamini kukamilika ili akasaini mkataba, sikuwa natarajia hata mia yake, lengo langu nilitaka vipaji nilivyoviibua vifike hatua vina majumba, magari mjini, nikaona ndiyo wakati wa Mwakinyo.”
Anasema wakati wanapanga siku inayofuata kwenda Dar es Salaam ili amsaidie katika masuala hayo ya kimkataba, kumbe Mwakinyo naye alikuwa na mipango yake.
“Nimempigia simu jioni kuhusu hiyo safari, akasema tayari ameondoka na rafiki yake, basi nikamuacha, sikushiriki kwa lolote katika mkataba ule,” anasema.
Anasema anachoshukuru bado wana uhusiano mkubwa na Mwakinyo mpaka sasa.
“Kuna siku anakuja ofisini kwangu ananiambia mzee dola 100 hii chukua, elfu 40 hii, japo nakuwa na pesa nyingi kushinda hizo, lakini sikatai asijekuona nimedharau, naichukua nanunua umeme wa chuo ili naye apate thawabu,” anasema.
Alikataa pambano la Tshibangu wa DRC
Miezi kadhaa iliyopita, Mwakinyo alizichapa na Tshibangu Kayembe wa DR Congo kuwania ubingwa wa dunia wa WBF lililopigwa kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam..
“Lile pambano sikulipenda, nililikataa, kwani jamaa alikuwa hatunufaishi, hakuwa ‘active’ lakini kila bondia ambaye alilengwa hakupatikana kwa kuwa kilikuwa kipindi cha corona na nchi nyingi zilikuwa kwenye ‘lockdown’, hivyo ikabidi tu aje Kayembe ambaye naye alikuja kibishi.
Anasema pambano lile liliacha alama, kwani kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi kupita watu walikesha kulisubiri kama ilivyokuwa miaka ya 1990 walipokuwa wakisubiri pambano la Mike ‘Iron’ Tyson.
“Mwakinyo amerejesha morali ya ngumi nchini, ni nembo ya ngumi hivi sasa lazima alindwe, tumsapoti huyu ndiye Mbwana Samatta (nyota wa soka nchini) wetu kwenye ngumi kwa sasa,”.
Anasema hivi sasa ngumi za Tanzania zinakwenda juu, na ikifika Desemba kama mapambano yote ambayo yako kwenye ‘pipeline’ ya kuchezwa yatafanyika, Tanzania itakuwa na mabondia wengi wa nyota tatu hadi nne, ambao kidunia bondia wa nyota hizo si wa bei rahisi.
“Kuna vijana kama sita nawaandaa ili kuja kufuata nyayo za Hassan kwenye ngumi, mabondia wetu hadi Januari watakuwa wanauzika, tutaacha kucheza zile ngumi za nani ni nani bali za maslahi na biashara katika levo ya kidunia,” anasema.
SI MWAKINYO TU
Promota hiyo maarufu nchini anasema licha ya kupingwa vikali na familia yake, lakini hakuwasikiliza na kama angekuwa anawekeza kwenye miradi mingine pesa aliyoingiza kwenye ngumi, basi leo hii angekuwa ni mmiliki wa maghorofa makubwa mjini.
“Nikisema ni kiasi gani nimetumia katika ngumi, leo hii kuna watu wa familia yangu watasikitika, sababu ni fedha nyingi sana, ila nilifanya hivi sababu ya mapenzi yangu tu na huu mchezo,” anasema.
Anasema katika familia yake, kuanzia wazazi wake hadi watoto wake, hakuna hata mmoja aliyewahi kumsapoti kwenye harakati hizo za kusapoti ngumi na kuendeleza vipaji vya mabondia.
“Niliingia kwenye ngumi mwaka 1986, wakati huo nikiwa kama bondia,” anasimulia Mwazoa katika mahojiano hayo maalumu na gazeti hili mjini Tanga.
Mwanzoa anasema wakati huo alikuwa bondia wa klabu ya Bandari, mjini Tanga, ambayo ilikuwa na mabondia wakali na klabu iliwajali kwani wengi wao walipata ajira.
“Tanga klabu ya ngumi ilikuwa ni moja tu ya Bandari Tangamano, zikianza sparing (mazoezi ya kupigana ana kwa ana) ngumi zinapigwa sijapata kuona, kulikuwa na bondia pale anaitwa Abel Kisusi alikuwa moto licha ya umri wake mkubwa, Ramadhan Rashid ‘Sugar Ray’ na wengine wakali, kocha wetu alikuwa mzee Myeto (sasa ni marehemu) na mzee Jumbe.
Baada ya kizazi hicho kupita, kikaja kile cha kina Bonzo Mohammed, Mzee Mashango, Chaula, Mambeya Bakari, Hamis Tamimu, Said Mzenga, Nuru Stiba na Pama.
Familia
Mwazoa anasema familia yake haikuwa na mapenzi na ngumi, hasa baba yake, hivyo ili kumuondoa kwenye mstari huo, wakamtoa Tanga na kumhamishia shule Dar es Salaam.
“Mzee aliamini nikitoka Tanga, ngumi basi, lakini niliendelea kucheza, nilianza mazoezi kwenye klabu ya Bandari Dar es Salaam ambapo nilikuta pamesheheni, niliwakuta mabondia kama Tonge Nyama (sasa ni marehemu), Bruno Mwemezi na wengine wengi.
“Baada ya muda mzee akapata taarifa kuwa nacheza ngumi, nikahamishiwa Moshi, nikiwa kule nilikutana na afande anaitwa Yassin ni bondia nilifahamiana naye nikiwa Dar es Salaam, akanipeleka CCP nikaendelea na ngumi,” anasema.
Anasema mwaka 1989, mzee wake ambaye alikuwa mwanajeshi aligundua kwamba amerudi kwenye ngumi, akalazimika kumrejesha Tanga.
“Hakuna kitu kibaya kama kuwa na mapenzi na kitu, mimi nilikuwa kama ‘teja’ wa ngumi, sikuacha, niliendelea lakini wakati huunikiwasapoti mabondia wenzangu ambao walikuwa wakiendelea kucheza.
Miongoni mwa mabondia hao ni Fadhil Keya, Haji Pela, Mzonge Hassan, Jafar Bahatisha, Kidila, Kijiwe Halfani ambao wote ni wa Tanga.
“Baadaye ndipo ikaja ‘generation’ ya Magoma Shaban ambaye alikuwa na wenzake wengi, lakini wakati huo huo nilikuwa nikiwasapoti mabondia wa ridhaa Tanga.
“Kuna wakati nilikuwa nikiipeleka timu kwenye mashindano ya taifa hata mkoa haufahamu, ikawa hivyo si tu ngumi za kulipwa, hadi ngumi za ridhaa,”
Magoma amliza
Katika vitu ambavyo Mwazoa anasema hawezi kuvisahau ni kilichomtokea Magoma Shaban bondia aliyetamba kimataifa enzi za uhai wake.
Usikose kesho Oktoba 31, 2020 Mwazoa akizungumzia Magoma alivyoondoka mikononi mwake.