Mukrim aibukia kambini Dodoma
Muktasari:
- Inaelezwa timu hiyo imeongeza nguvu katika safu yake ya ulinzi baada ya kufikia makubaliano na Mukrim Issa ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili akitokea Singida.
DODOMA Jiji imekita kambi jijini Arusha ikijiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza Agosti 14 2026, sasa kwenye kambi hiyo ameonekana Mukrim Issa beki wa kati aliyemaliza mkabata na Singida Black Stars.
Inaelezwa timu hiyo imeongeza nguvu katika safu yake ya ulinzi baada ya kufikia makubaliano na Mukrim Issa ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili akitokea Singida.
Chanzo cha kuaminika kimeiambia Mwanaspoti kuwa nyota huyo tayari amejiunga na kambi ya timu hiyo iliyoweka makazi jijini Arusha.
“Kocha alihitaji beki mwenye uzoefu wa Ligi Kuu na michuano ya CAF ili kusaidiana na kina Abdi Banda, ndiyo akapendekezwa Mukrim amesaini mkataba wa miaka miwili na tayari yupo kambini na wenzake,” kimeongeza chanzo hicho.
Mukrim anawasili Dodoma Jiji akiwa na uzoefu wa kucheza Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na Singida Black Stars. Ujio wake unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Dodoma Jiji kuimarisha safu ya ulinzi kuelekea msimu wa 2026/27.
Msimu uliopita Mukrim hakupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Singida kutokana na ushindani mkubwa uliokuwapo, nafasi ambayo ilikuwa inatumiwa vizuri na Kennedy Juma, Abdallah Kheri ‘Sebo’na Abdulmalik Zakaria.
Takwimu zinaonyesha alicheza mechi 10 katika mashindano yote, akianza kikosini mara kadhaa na kucheza dakika 720 alianza kwenye mechi za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Otoho d’Oyo, CR Belouizdad na Stellenbosch.
Rekodi zinaonyesha beki huyo alianza msimu vizuri akicheza dakika zote 90 katika mechi dhidi ya KMC, JKT Tanzania na Fountain Gate.
Hata hivyo, kuanzia katikati ya msimu alianza kupoteza nafasi, mara nyingi akiishia benchi au kutokuwa kabisa kwenye kikosi kutokana na ushindani uliokuwepo ndani ya Singida.