‘Shashaman’ aanza na moto Yanga
Muktasari:
- Shashaman aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea CBE ya Ethiopia aliandika bao lake katika mchezo huo wa raundi ya pili ya ligi, huku bao jingine la Yanga Princess likifungwa na Rehema Ramadhan ambaye naye alisajiliwa msimu huu akitokea Fountain Gate Princess, matokeo yaliyoifanya timu hiyo kuendelea kuonyesha makali yake katika mbio za kuwania ubingwa wa msimu wa 2026/27.
MSHAMBULIAJI wa Yanga Princess, Mesay Temsgen maarufu kama Shashaman, ameendelea kuonyesha ubora wake katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) baada ya kufunga bao lake la pili katika michezo miwili ya mwanzo ya msimu huu, akiisaidia timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Geita Queens leo jioni katika Uwanja wa Nyankumbu.
Shashaman aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea CBE ya Ethiopia aliandika bao lake katika mchezo huo wa raundi ya pili ya ligi, huku bao jingine la Yanga Princess likifungwa na Rehema Ramadhan ambaye naye alisajiliwa msimu huu akitokea Fountain Gate Princess, matokeo yaliyoifanya timu hiyo kuendelea kuonyesha makali yake katika mbio za kuwania ubingwa wa msimu wa 2026/27.
Kasi ya mshambuliaji huyo ilianza tangu mchezo wa ufunguzi wa ligi dhidi ya Bunda Girls, ambapo Yanga Princess ilipata ushindi wa mabao 3-0 na Shashaman alikuwa miongoni mwa wafungaji akiweka kambani bao moja.
Hata kabla ya kuanza kwa ligi, Shashaman alionyesha uwezo wake katika mashindano ya Ngao ya Jamii, kwenye mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya Mashujaa Queens. Katika mchezo huo, Yanga Princess ilitanguliwa kwa bao lililofungwa na Maimuna Hamis 'Mynaco', kabla ya kiungo huyo kusawazisha na kuipa timu nafasi ya kurejea mchezoni.
Wakati Yanga Princess ikipata ushindi huo, matokeo mengine ya raundi ya pili JKT Queens ikiichapa Bunda Girls mabao 2-0 kupitia Donisia Minja na Neema Issa, huku Simba Queens ikishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate Princess, bao lililotokana na kujifunga kwa beki wa Fountain.
Mashujaa ikiwa Uwanja wa Ushirika ilitembeza kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Kilimanjaro Wonders, Tausi nayo haijanza vyema msimu ikipoteza tena kwa mabao 2-1 dhidi ya Alliance Girls. Mechi ya raundi ya kwanza Tausi ilipoteza mabao 5-2 dhidi ya Bunda Queens.
Mechi nyingine iliyopigwa Uwanja wa Samora Iringa Ceasiaa ikiwa mwenyeji iliitandika mabao 4-2 Bunda Queens.