20 wabeba matumaini ya KVZ Libya
Muktasari:
- KVZ, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, wapo Libya kukabiliana na wenyeji wao hao, mechi itakayopigwa kesho Ijumaa saa 2:00 usiku kisha kurudiana Septemba 13, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
KIKOSI cha wachezaji 20 cha KVZ kimebeba matumaini ya Zanzibar katika kuanza vizuri safari ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kinapojiandaa kuikabili Al Swehly SC ya Libya katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali.
KVZ, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, wapo Libya kukabiliana na wenyeji wao hao, mechi itakayopigwa kesho Ijumaa saa 2:00 usiku kisha kurudiana Septemba 13, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kocha Mkuu wa KVZ, Hababuu Ali amesema maandalizi ya timu hiyo yamejengwa kutokana na uzoefu wa mechi za kimataifa, zikiwemo tatu ilizochezwa kwenye mashindano ya Kagame Cup, Rwanda pamoja na mbili zilizochezwa Zanzibar ambazo ni Ngao ya Jamii na Ligi Kuu.
Hababuu amesema mechi hizo zimewapa wachezaji nafasi ya kuona na kuonja ushindani wa kimataifa, hivyo safari ya Libya si kwa ajili ya kushiriki pekee, bali kwenda kupambana.
"Kutopkana na mechi hizo tumepata uzoefu wa kimataifa. Tunaenda kushindana na siyo kushiriki,” amesema Hababuu na kuongeza, baada ya ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka, walipata nafasi ya kuwafuatilia na kuwachambua wapinzani wao, jambo alilodai limewasaidia kujiandaa vyema kwa mechi hiyo.
Amesema wanatambua ukubwa na uzoefu wa Al Swehly, lakini hawataki kuingia uwanjani wakiwa na hofu, wakiamini wana uwezo wa kupata matokeo mazuri ugenini.
“Tunajua tunaenda kucheza na timu kongwe, lakini si maarufu kama Al Ahli Tripoly. Hata hivyo, tunaamini mechi itakuwa ngumu kwa sababu tunacheza kwao,” amesema na kuongeza, lengo lao kubwa ni kufanya vizuri katika mechi ya kwanza ili kupata nafasi nzuri ya kumaliza kazi ya marudiano itakayochezwa Zanzibar.
Kwa mujibu wa kocha huyo, kuanza ugenini pia kunaweza kuwa faida kwao kwa kuwa matokeo mazuri watakayoyapata Libya yatawapa nafasi nzuri ya kutumia mechi ya nyumbani kuamua hatima yao.
Al Swehly inayofundishwa na kocha Hamadi Al-Qwiry, ndani ya kikosi hicho kuna kiungo wa zamani wa Simba, Débora Fernandes Mavambo aliyetua msimu uliopita.
KVZ iliyoondoka Zanzibar Septemba 1, 2026, ilikuwa na msafara wa watu 31, ambao unajumuisha wachezaji 20 na viongozi 11.
Msafara huo umeongozwa na Kanali Juma Hassan, Mkuu wa Utawala wa KVZ, huku benchi la ufundi likiongozwa na Hababuu Ali Omar.
Viongozi wengine ni Khalid Khalid, Meneja Abdi Mansour, Kocha Msaidizi Suleiman Abdi, Daktari Saleh Said, mtunza vifaa Ali Kimti na Ofisa Habari Abdul-Jalil Mohamed.
Wachezaji waliobeba matumaini ya KVZ katika safari hiyo ni Bashir Muslim Darwesh, Hamad Ubwa ‘Baro’, Idrisa Mgunya ‘Zungu’, Yakoub Said ‘Nkane Ally’, Mudrik Abdi ‘Gonda’, Munir Shafi ‘Mlipili’, Akram Muhina ‘Haaland’, Muhammed Mussa ‘Banega’, Mohamed Shaaban ‘Kwacha’, Hamid Bakar Omar ‘Gaucho’, Said Mussa ‘Mbeki’, Suleiman Kidawa ‘Pogba’, Mohammed Massoud ‘Dola’, Mussa Legeye ‘Jeba’, Hassan Kassim, Mukrimu Juma Madai, Salim Said Mgaya ‘Mbonde’, Ibrahim Sangula, Amour Kheir ‘Park’ na Majid Khamis Bakar.