Wagosi wakubali, straika ajipanga upya Ligi Kuu
Muktasari:
- Wagosi hao hawajawa na mwanzo mzuri baada ya kucheza mechi nne wakiambulia sare moja na kupoteza tatu, huku wakiruhusu mabao saba na kufunga mawili wakishika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu kati ya timu 16.
MBEYA; COASTAL Union imesema kuanza vibaya Ligi Kuu Bara msimu huu si uwezo mdogo wa timu, bali ni sehemu ya matokeo ya mpira, ikieleza kuwa kwa sasa makosa yaliyoonekana yamefanyiwa kazi na mechi zinazofuata kwao itakuwa ni furaha.
Wagosi hao hawajawa na mwanzo mzuri baada ya kucheza mechi nne wakiambulia sare moja na kupoteza tatu, huku wakiruhusu mabao saba na kufunga mawili wakishika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu kati ya timu 16.
Straika wa timu hiyo, Maabad Maulid, amesema mwanzo huo si mzuri sana kwao, akieleza kuwa yapo makosa binafsi yaliyoonekana, lakini benchi la ufundi limeyafanyia kazi na matarajio mechi zijazo watafanya vizuri.
Amesema kuondoka kwa baadhi ya nyota kikosini hapo, imewatingisha kitimu kwani walikuwa na muunganiko mzuri hivyo mechi za mwanzo zimewapa ugumu kutokana na maingizo mapya japokuwa kwa sasa maelewano uwanjani yapo.
“Tulivyocheza dhidi ya Simba kuna utofauti mkubwa ukilinganisha na zile tatu za nyuma, maana yake tumeanza kuunganika na kujipata, matarajio yetu ni kuona mechi zinazofuata tunafanya vizuri.
“Siyo matokeo mazuri kwa timu kama hii yenye malengo makubwa, lakini naamini kuanzia mchezo dhidi ya Polisi Tanzania tuianze rasmi Ligi, hatujakata tamaa na nia yetu ni kuipa mafanikio timu,” amesema nyota huyo.
Kuhusu uhaba wa mabao haswa kwake, straika huyo amekiri kuanza vibaya akieleza kuwa mechi nne mfululizo bila bao si dalili nzuri kwake na badala yake anajipanga upya na michezo ijayo kurejesha kasi yake.
Straika huyo alijiunga na Coastal Union msimu wa 2022-2023 akitokea KVZ baada ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar kwa mabao 19.