UDANGANYIFU WA UMRI: Sumu inayolibomoa soka la Tanzania -2
Muktasari:
Mwanaspoti pia lilizungumza na baba mzazi wa Mrisho Ngassa, Khalfan Ngassa, mchezaji wa zamani wa Pamba, Simba na Taifa Stars ambaye hata hivyo alikataa kuzungumzia mambo ya mwanaye.
KATIKA toleo la Ijumaa iliopita tuliona jinsi tatizo la udanganyifu wa umri linavyoanza baada ya uchunguzi tulioufanya kwa wachezaji Nurdin Bakar na Mrisho Ngassa ambao wote wamewahi kuzichezea timu za Yanga, Simba na Taifa Stars. Endelea…
Mwanaspoti pia lilizungumza na baba mzazi wa Mrisho Ngassa, Khalfan Ngassa, mchezaji wa zamani wa Pamba, Simba na Taifa Stars ambaye hata hivyo alikataa kuzungumzia mambo ya mwanaye.
“Nina watoto wengi, wengine wanafanya shughuli zao, ni bora historia yake aizungumzie mwenyewe, kama atakosea sawa na akipatia sawa, hilo ni jukumu lake na si mimi,’’ anasema.
Ngassa mwenyewe alipoulizwa kuhusu hilo alionyesha kukerwa na jinsi Mwanaspoti lilivyozungumza na mzazi wake kuhusu mambo yake: “Yaani tunafuatiliana hadi kwa wazazi, mimi sipendi mambo hayo.”
Baada ya Ngassa na Nurdin, Mwanaspoti lilisafiri hadi mkoani Kigoma alikozaliwa kipa Juma Kaseja ambaye pia amewahi kuzichezea timu za Simba, Moro United na Taifa Stars na sasa ni mchezaji wa Yanga.
Umri wa Kaseja unaotambulika kwenye familia ya mpira ambao vielelezo vyake vipo TFF unaonyesha kwamba amezaliwa Aprili 20, 1985 na sasa ana umri wa miaka 29.
Hata hivyo, katika kujiridhisha na hilo, Mwanaspoti likiwa mkoani Kigoma lilipata taarifa zinazokinzana na umri sahihi wa kipa huyo maarufu na mwenye heshima kubwa nchini.
Utafiti wa Mwanaspoti unaonyesha kuwa Kaseja ana umri kati ya miaka 34 hadi 37 na si 29 kama inavyosomeka kwenye vielelezo vya TFF.
Kaseja alisoma katika Shule ya Msingi Karuta ambayo wenyeji wanasema zamani ilikuwa ikijulikana kwa jina la White Fathers.
Mwandishi wa Mwanaspoti alifika katika shule hiyo, utata wa kwanza alioukuta ni katika jina ambako vielelezo vinaonyesha kwamba Kaseja alikuwa akiitwa kwa jina la Juma Kaseija na Juma Kasheija.
Utata huo wa majina umeonekana katika orodha ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Karuta, katika wanafunzi waliotakiwa kufanya mtihani wa darasa la nne mwaka 1991 lipo jina la Juma Kaseija wakati kwa wanafunzi waliokuwa wakiandaliwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka 1994 lipo jina la Juma Kasheija.
Utafiti wa Mwanaspoti katika jina hilo ulibaini kuwa tatizo lipo katika matamshi au lafudhi na hivyo kusababisha kuandikwa lilivyoandikwa lakini kinachojionyesha ni kwamba Kasheija na Kaseija ni huyohuyo Kaseja.
Mwanaspoti halikufanikiwa kupata mwaka sahihi wa kuzaliwa wa Kaseja kwa sababu cheti chake hakikuwepo shuleni hapo lakini sehemu kubwa ya vielelezo vya wanafunzi aliosoma nao darasa moja, vinaonyesha kwamba walizaliwa kati ya miaka ya 1977 hadi 1980.
Kwa hiyo si sahihi kusema kwamba Kaseja ana umri wa miaka 29 badala yake umri wake sahihi ni kati ya miaka 34 hadi 37 na haiwezekani awe na miaka 29 halafu amalize darasa la saba mwaka 1994.
Kama kweli Kaseja ana miaka 29 maana yake ni kwamba alizaliwa mwaka 1985 kama vielelezo vya TFF vinavyoonyesha lakini mtoto hawezi kuzaliwa mwaka 1985 halafu mwaka 1994 yaani akiwa na miaka tisa amalize darasa la saba. Hilo haliwezekani.
Au mtoto huyo aliyezaliwa 1985 afanye mtihani wa darasa la nne mwaka 1991 akiwa na miaka sita umri ambao ni wa mtoto kuanza darasa la kwanza na wakati mwingine hata la kwanza bado hajaanza.
Au kama kweli alizaliwa 1985 na akamaliza darasa la saba mwaka 1994 hiyo pia maana yake ni kwamba alianza darasa la kwanza mwaka 1986 wakati huo ana miaka miwili. Hilo haliwezekani.
Kwa hiyo ukweli ni kwamba suala la umri lina utata kwa Kaseja lakini jambo moja la kweli kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwanaspoti ni kwamba umri wake ni zaidi ya miaka 29.
Katika kuutafuta ukweli wa Kaseija na Kasheija kuwa ndiye Juma Kaseja, Mwanaspoti lilizungumza na baadhi ya wenyeji wa Ujiji ambao wanasema ndiye huyo huyo isipokuwa kilichojitokeza ni utata wa maandishi.
Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hussein, mfanyabiashara wa chipsi katika eneo la stendi ya mabasi ya Ujiji anasema anamtambua Kaseja kwa sababu alisoma naye Shule ya Msingi Karuta lakini walitofautiana madarasa.
Anasema, Kaseja alimaliza darasa la saba mapema na akamwacha shuleni, hata hivyo hakumbuki ni mwaka gani ambao mlinda mlango huyo aliyepata umaarufu tangu utotoni alimaliza darasa la saba.
Hussein anafafanua kuwa, yeye alimaliza masomo yake hapo Karuta mwaka 1998 na alimfahamu, Kaseja kwa sababu alikuwa maarufu sana shuleni hapo kutokana na kipaji chake katika soka.
Alifanya vizuri kwenye timu ya shule hadi akachaguliwa kwenye ngazi mbalimbali kuanzia wilaya hadi mkoa huku akisisitiza kwamba Kaseja ndiyo huyo huyo hakuna mwingine.
Kama hiyo haitoshi, Mwanaspoti lilipiga hodi nyumbani kwa Mwalimu Mkuu Mstaafu wa Shule ya Msingi Karuta, Zubeir Kisongo ili kumjulia hali na kupata ukweli kuhusu Kaseja.
Mwalimu huyo ambaye alifundisha shuleni hapo miaka ya 1990 anasema: “Namfahamu vizuri Kaseja nimemfundisha Karuta, ni miaka mingi sina kumbukumbu nzuri lakini ni miaka ya 1990.”
Anasema: “Baba yake mzazi alikuwa anafanya kazi katika Bandari ya Ziwa Tanganyika lakini naye pia alikuwa na kipaji cha kucheza mpira hivyo, Kaseja amerithi kwake.”
Akimzungumzia, Kaseja katika maisha yake ya shule anasema, alikuwa maarufu kwa sababu ya kipaji chake cha kucheza mpira kama mlinda mlango na kwa maisha ya nje alikuwa mchangamfu na mpenda watu wa rika zote.
Mwanaspoti pia lilizungumza na mwamuzi mstaafu, Nassoro Hamduni ambaye kwa sasa anaishi Ujiji mkoani Kigoma. Hamaduni aliyestaafu mwaka 2007 anasema: “Kaseja ni kijana wetu wa hapa hapa Ujiji, hilo halina shaka.
Anafafanua kuwa alimfahamu Kaseja tangu akiwa mtoto mdogo wakati akisoma Shule ya Msingi Karuta miaka ya 1990 lakini hana kumbukumbu juu ya mwaka sahihi aliomaliza masomo.
Naye, aligusia utata wa majina hayo ya Kaseija na Kasheija na kusema, tofauti hapo ni matamshi tu.
Kaseja azungumza
Mwanaspoti lilizungumza na Kaseja ili kujua ukweli wa majina yake na kuhusu Shule ya Msingi Karuta na mwaka alioanza masomo, naye akasisitiza kwamba jina analotumia sasa ndio sahihi.
Na hakupinga kuwa yeye ni mkazi wa Ujiji na amesoma Shule ya Msingi Karuta ingawa hakutaka kuweka wazi mwaka aliomaliza masomo katika shule hiyo.
“Nitamkie kwa herufi,” anahoji Kaseja na kufafanua: “Jina langu ni Kaseja, hakuna anayeweza kujua ukweli wa majina yangu hata kama tumesoma darasa moja na kuishi pamoja.”
Kwanini wanadanganya umri?
Boniface Pawasa ni mchezaji wa zamani wa Klabu ya Simba na Taifa Stars ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka, anasema kwamba tatizo la udanganyifu wa umri ni kubwa, si Tanzania tu bali lipo Afrika yote. Akizungumzia sababu za kudanganya umri Pawasa anasema: “Sababu kubwa ni mfumo wa maisha yetu ya Kitanzania au Afrika.”
“Maisha ya kazi ya mpira ni mafupi yakizidi sana ni miaka 15 hadi 20, lakini mara nyingi ni chini ya hapo, inaweza kuwa miaka mitano au saba, hatuna muendelezo wa malezi yatakayomfanya mchezaji akue katika msingi bora wa maisha ya soka kama wanavyofanya wenzetu wa nchi za Ulaya,” anasema Pawasa.
“Katika maisha yetu mchezaji anakuwa huku na kipaji chake kinakuja kutambulika kwenye jamii baadaye akiwa tayari na umri mkubwa,’’ anafafanua Pawasa.
“Na kwa sababu maisha ya mpira ni mafupi, ili mchezaji acheze kwa muda mrefu inambidi apunguze miaka mwenyewe, atakaposema miaka yake ya halali labda 25 au 28 soko lake litashuka tofauti na yule wanayefanana kiwango lakini amesema ana miaka 19 au 20,’’ anasema. “Lakini atakapotaja pia umri wake sahihi wa miaka 25 atashindwa kukamilisha malengo yake kwa sababu atakuwa na kipindi kidogo cha kucheza,’’ anasema. “Ukisema una miaka 25 baada ya miaka mitano tu utakuwa na miaka 30, hapo tayari utaanza kuandamwa na jamii hata klabu zitakunyima ulaji kwa sababu ya umri mkubwa na kuambiwa umeshakuwa mzee.”
Pawasa anafafanua sababu ya pili inayowafanya wachezaji kudanganya umri ni kupata fursa ya kushiriki mashindano ya vijana wa umri chini ya miaka 17, 20 kwa ngazi ya mkoa na hata taifa.
Anasema, anaweza kuwapo mchezaji mwenye umri mkubwa labda miaka 19 halafu kuna mashindano ya umri chini ya miaka 15 na timu inaamini mchezaji huyo atawasaidia.
Kitakachofanyika hapo ni viongozi, watazungumza naye ili abadili umri wake sahihi na kudanganya na kwa sababu soka ndiyo ajira ya mchezaji hatoweza kukataa.
Pawasa anatolea mfano wa mashindano ya vijana kama Copa Coca Cola (U-15), Uhai Cup (U-20 na Airtel Rising Stars (U-17) pamoja na timu za taifa za vijana wa umri mdogo.
“Uongozi wa timu unaweza kuwa haujafanya maandalizi vizuri na wanataka ushindi, watawachukua vijana wenye uwezo wa juu bila kujali umri sahihi wa mashindano na kuwatafutia vielelezo vya kufoji ili tu wawasaidie kupata ushindi,’’ anasema.
Itaendelea kesho Jumanne…