SportPesa yaimwagia Namungo Sh120m

Dar es Salaam. Kampuni ya michezo na burudani SportPesa, imeongeza mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya Namungo kutoka mkoani Lindi, Ruangwa.

Huu uni mjumuisho wa miaka miwili tangu kumalizika kwa mkataba wa kwanza.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Namungo, Hassan Zidadu alisema: “Ningependa kuwashukuru sana SportPesa kwa kutupokea kwa mikono miwili na kuendeleza mkataba wetu kwa mwaka mwingine tena.

“Hii ni ishara ya kutukubali sisi kama klabu na kujiunga katika maendeleo yetu ili kuboresha uendeshaji wa klabu.

“Kama klabu tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa kufanya vizuri.”

Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa, Tarimba Abbas aliwapongeza Namungo kwa kujiendesha vizuri na kuhakikisha timu inafanya vizuri barani Afrika na kuipa Tanzania na SportPesa sifa inayostahili.

“Hii ndiyo sababu iliyotufanya kuendelea kuwadhamini Namungo, ukiiangalia vizuri klabu hii tangu ianze hadi sasa unaweza kuona ni jinsi gani ilivyo na moyo wa kujituma na kuhakikisha wanafika mbali,” alisema Tarimba.

Namungo inashiriki mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.