Simba: Kaenda Kaizer Chiefs itakuwa sisi!
MJUMBE wa Bodi ya Simba, Zakaria HansPope amesema kama Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini imecheza fainali ya Afrika msimu huu basi wao ni jambo la kuvuta muda tu msimu ujao.
Alisema kuwa kitendo cha timu mbili walizozifunga ambazo ni Kaizer Chiefs na Al Ahly kucheza fainali ya Afrika kimewapa mzuka mkubwa kwamba msimu ujao unaoanza Septemba wataingia na rekodi mpya ya zaidi ya robo fainali.
Hans Pope alisema kuwa kitendo cha kuchukua ubingwa wa Bara kwa timu hiyo kwa sasa kimekuwa ni kitu cha kawaida akili yao mpya ni kuweka nguvu zaidi kwenye michezo ya kimataifa walikoishia robo fainali kwa misimu miwili mfululizo.
“Simba ni timu kubwa kwa sasa na ndio mabingwa wa nchi kwa kuwa tumeshachukua makombe ya Ligi Kuu mara nne na sasa tumechukua Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kwa mara ya tatu tayari inatosha kuonyesha ukubwa wa klabu yetu kwenye soka la ndani hivyo nguvu ni kuwekeza kwenye michuano ya kimataifa ambayo tumekuwa tukifanya vizuri kiasi lakini sio kwa malengo ambayo tumekuwa tukijiwekea” alisema Hans Pope na kuongeza;
“Tunachohitaji kwa sasa ni kuvuka mipaka na kuchukua ubingwa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa tumeshachukua sana huku nyumbani na tumezoea ubingwa wa nyumbani hivyo kwa sasa ni levo nyingine za kimataifa na kuonyesha ukubwa wa Simba.”
Aidha alisema kuwa kutokana na ubora wa kikosi cha timu hiyo na maboresho watakayoyafanya kuelekea msimu ujao wanaamini yataleta tija katika kutimiza malengo yao ambayo wamekuwa wakiyatafuta kwa muda mrefu.
“Kaizer Chiefs walishiriki kwa mara ya kwanza katika michuano ile na alifanya vizuri sasa kwanini sisi tushindwe? tunajua michuano ni migumu kutokana na ubora wa timu ambazo tunashindana nazo lakini hilo kwetu sio tatizo kwa kuwa tumecheza na timu kubwa Afrika zenye bajeti kubwa zaidi yetu na tumeonesha ukubwa wa timu yetu,” alisisitiza.
Simba iliishia kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) walipotolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-3.
Hiyo ilikuwa ni mara ya pili ndani ya misimu mitatu.
IMEANDIKWA NA DAUDI ELIBAHATI