Prime
Barker ampa tano Keletso
KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker amesema licha ya kikosi chake kuhitimisha ushiriki wa Kombe la CECAFA Kagame kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars, bado hajaona sababu ya kuridhika kwani anaamini kuna mambo mengi yanapaswa kuboreshwa kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Simba iliaga mashindano hayo ikiwa na pointi tano baada ya suluhu mbili dhidi ya Mogadishu City na Jamus kabla ya kuibuka na ushindi dhidi ya Singida Black Stars, matokeo ambayo hayakutosha kuipeleka katika hatua ya nusu fainali.
Hata hivyo, Barker amesema pamoja na kuondolewa mapema, mashindano hayo yamempa majibu mengi aliyokuwa akiyatafuta kuhusu kikosi chake kipya na hatua ya maandalizi kuelekea Simba Day, Ngao ya Jamii na Ligi Kuu ya NBC.
GAME MBILI ZA KWANZA
Barker anasema jambo linalomuumiza zaidi si kuondolewa kwa Simba, bali namna ambavyo timu yake ilishindwa kutumia nafasi ilizozipata katika mechi mbili za mwanzo.
Kwa mujibu wa kocha huyo, Simba ilicheza vizuri dhidi ya Mogadishu City na Jamus, lakini ukosefu wa umakini ndani ya eneo la hatari uliigharimu timu hiyo pointi muhimu ambazo zingekuwa tiketi ya kucheza nusu fainali.
“Katika mechi mbili za kwanza tulijiumiza wenyewe kwa kushindwa kuwa makini mbele ya lango, tulitengeneza nafasi nyingi ambazo zilitosha kutupa ushindi, lakini hatukuzitumia. Kama tungezitumia, pengine leo tungekuwa tunazungumzia kufuzu badala ya kuaga mashindano,” anasema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.
Anasema tofauti kubwa kwenye mchezo dhidi ya Singida Black Stars ilikuwa ni uwezo wa wachezaji wake kutumia nafasi walizozitengeneza, jambo lililompa ushindi wa kwanza katika mashindano hayo.
USHINDI WAREJESHA IMANI
Licha ya kutofuzu hatua inayofuata, Barker anasema ushindi huo ulikuwa muhimu kwa upande wa kisaikolojia.
Kocha huyo anasema baada ya sare mbili za mwanzo kulikuwa na haja ya kumaliza mashindano kwa ushindi ili kurejesha hali ya kujiamini ndani ya kikosi kabla ya kuingia kwenye ratiba ngumu ya msimu mpya.
Anaeleza ushindi huo umeongeza morali ya wachezaji kuelekea Simba Day na baadaye mchezo wa Ngao ya Jamii, ambao utakuwa kipimo kingine muhimu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
“Nimefurahishwa na kiwango cha wachezaji, walijituma kwa kiwango kikubwa, walionyesha nguvu kubwa hasa kipindi cha kwanza na walipambana hadi dakika ya mwisho, huo ndio mtazamo ninaotaka kuuona ndani ya timu,” anasema.
Barker anakiri hali ya uwanja haikuwa rahisi kutokana na mvua iliyonyesha na kufanya sehemu kubwa ya uwanja kuwa na utelezi, lakini akawapongeza wachezaji wake kwa namna walivyokabiliana na mazingira hayo.
KAGAME IMEMPA MAJIBU?
Kwa Barker, CECAFA Kagame haikuwa mashindano ya kutafuta kombe pekee.
Kocha huyo anasema moja ya sababu zilizomfanya afanye mabadiliko makubwa ya kikosi katika kila mchezo ilikuwa kuwapa nafasi karibu wachezaji wote wapya na wa zamani ili kujua uwezo wao katika mazingira ya ushindani.
Anawataja Rushine De Reuck, Ismael Toure, Clatous Chama na Anicet Oura kuwa ni baadhi ya wachezaji waliopata muda wa kutosha wa kucheza, jambo lililompa nafasi ya kutathmini maendeleo yao.
“Pia ilikuwa muhimu kuona jinsi kila mmoja anavyoendana na mfumo wetu wa uchezaji, dakika walizopata zitatusaidia kufanya maamuzi sahihi kuelekea msimu mpya,” anasema.
DOUMBIA, KELETSO
Kocha huyo amesema moja ya mambo yaliyomfurahisha zaidi ni mshambuliaji Ibrahim Doumbia kufunga bao lake la kwanza akiwa Simba.
Kwa mujibu wa Barker, mabao huwa yanaongeza kujiamini kwa washambuliaji na anaamini Doumbia atakuwa bora zaidi kadri atakavyopata muda wa kucheza.
Mbali na Doumbia, Barker anasema Nathan Chilambo ameanza kuonyesha utulivu mkubwa ndani ya kikosi, huku Keletso Makgalwa akionyesha uwezo mkubwa wa kasi na kucheza mmoja dhidi ya mmoja.
Hata hivyo, anasema Makgalwa bado hajafikia ubora wake; “Unaweza kuona uwezo wake wa kumkabili beki mmoja kwa mmoja na kasi yake lakini bado hajafikia kiwango chake bora kimwili, bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kuimarika,” anasema kocha huyo.
JABAAR AMETOA MATUMAINI
Kiungo Ibraheem Jabaar pia amemvutia Barker licha ya kucheza kwa muda mfupi.
Kocha huyo anasema kiungo huyo alikuwa hajacheza mechi za ushindani kwa takribani miezi minne baada ya kumaliza msimu nchini Afrika Kusini, hivyo kiwango alichoonyesha ndani ya dakika chache ni ishara nzuri.
“Nimefurahishwa naye, aliingia na kuonyesha nguvu na utulivu, huo ulikuwa mwanzo mzuri kwake,” anasema.
Barker anaamini kadri Jabaar atakavyoongeza utimamu wa mwili, atakuwa mmoja wa wachezaji muhimu ndani ya kikosi hicho.
KUHUSU KAPOMBE
Barker pia anazungumzia majeraha ya nahodha wa timu, akisema ni pigo kumpoteza mchezaji mwenye ushawishi mkubwa kama yeye.
Hata hivyo, anasema Simba ina kundi la viongozi wengine walioweza kubeba jukumu hilo wakati wa mashindano.
“Kukosa nahodha si jambo rahisi lakini tuna viongozi wengine kama Chama na wenzake ambao walisaidia kuhakikisha timu inaendelea vizuri,” anasema.
Anasema taarifa za kitabibu zinaonyesha majeraha hayo si makubwa kama ilivyohofiwa mwanzoni.
Kapombe alipata majeraha na kuugulia mkono baada ya kugongana na kipa Hussein Abel katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi dhidi ya Jamus.
Kwa mujibu wa Barker, nahodha huyo anatarajiwa kurejea mazoezini ndani ya wiki mbili na anaweza kuwa tayari kucheza ndani ya wiki tatu.
USAJILI UMEANZA KULIPA
Barker amesema ameridhishwa na kiwango cha wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba kuelekea msimu mpya.
Anasema kila mmoja ameonyesha dalili za kuendana na falsafa ya timu na anaamini kadri watakavyoendelea kufanya mazoezi pamoja, kiwango chao kitaongezeka.
“Nimefurahishwa na usajili tulioufanya, wachezaji wote wanaonyesha wana uwezo wa kutusaidia. Kadri tutakavyoendelea kukua kama timu, nao wataendelea kuwa bora zaidi,” anasema.
SIKIA ANACHOSEMA
Licha ya mambo yote mazuri aliyoyaona Kigali, Barker amesema hawezi kujipa alama za juu.
Amesisitiza kuwa hakuna kocha anayepaswa kuridhika kwa asilimia mia moja ikiwa bado anataka kuona maendeleo ya timu yake.
“Sidhani kama kuna kocha aliyewahi kuridhika kwa asilimia 100. Siku ukifikiri umefika hapo, labda ndiyo wakati wa kuacha ukocha, daima kuna kitu cha kuboresha,” anasema.
Anasema Simba imekuwa pamoja kwa muda mfupi tu tangu irejee kambini, hivyo bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kukifikisha kikosi kwenye kiwango anachokitaka.
SIMBA DAY, NGAO YA JAMII
Baada ya kumaliza safari ya Kagame, Barker anasema maandalizi sasa yanaelekezwa kwenye Simba Day na mchezo wa Ngao ya Jamii kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
Alifichua kuwa kikosi kitaendelea na mazoezi nchini Rwanda huku benchi la ufundi likipanga kucheza mchezo mwingine wa kirafiki kabla ya kurejea Tanzania.
Kwa Barker ambaye msimu ujao utakuwa wa pili kwake, CECAFA Kagame imekuwa sehemu ya mchakato wa kujeinga Simba ili kuwa bora zaidi.
Msimu uliopita aliisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Muungano visiwani Zanzibar, Kombea la CRDB huku wakimaliza nafasi ya pili kwenye Ligi ya NBC nyuma ya Yanga kwa tofuatu ya pointi mbili.
Ingawa matokeo hayakuipeleka timu hiyo nusu fainali, kocha huyo anaamini amepata kitu muhimu zaidi, picha halisi ya kikosi chake, maendeleo ya wachezaji wapya na maeneo yanayohitaji kuboreshwa kabla ya msimu mpya kuanza.