Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Azam shauri yenu

AZAM ikipoteza au kutoa sare nyumbani leo dhidi ya Simba itajiweka rehani kwenye mbio za nafasi tatu za juu. Lakini hata Simba ikipata matokeo kama hayo itairahisishia Yanga mbio za ubingwa.

Hivyo kulingana na mijadala ya mashabiki mitandaoni ni shauri ya kila timu kuamua kusuka au kunyoa ndani ya dakika 90 leo saa 1 usiku katika Uwanja wa Azam Complex.

Matokeo ya tofauti na ushindi katika mchezo wa leo, yatapokelewa kwa furaha zaidi na Namungo FC ambayo itazidiwa kwa pointi mbili au moja na Azam FC huku ikibakia na faida ya kuwa na mechi mbili mkononi ambazo ikipata ushindi, itasogea hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ambapo itafikisha pointi 36.

Simba wenyewe kama watapoteza au kutoka sare leo, watapunguza ugumu kwa vinara wa Ligi, Yanga katika mbio za ubingwa kwani yatawafanya watani wao hao wa jadi wanaoongoza msimamo wa ligi wakiwa na pointi 60, kuhitajika kupata pointi ushindi katika mechi tatu tu kati ya sita zilizobakia ili ijihakikishie ubingwa.

Simba ndio inahitaji zaidi ushindi ili iendelee kuipa presha Yanga katika mbio za ubingwa kwani itapunguza pengo la pointi kubakia nane, kutoka 11 ilizopitwa sasa.

Ushindi utaifanya Simba kufikisha pointi 52 ambazo zitaihakikishia kumaliza katika nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa ligi ambazo kikanuni, timu zitakazomaliza hapo, zitaungana na ile itakayotwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam kucheza mashindano ya kimataifa katika msimu wa 2022/2023.

Ni mechi ambayo huwa ya wazi pindi timu hizo zinapokutana na ndio maana imekuwa sio jambo la kushangaza kushuhudia kila moja ikifunga bao/mabao mara kwa mara.

Katika mechi 10 zilizopita baina ya timu hizo, jumla ya mabao 21 yamefungwa ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa kila mechi, ambapo Simba ndio timu iliyopachika idadi kubwa ya mabao ikifumania nyavu mara 13 huku Azam ikipachika mabao nane.

Safu ya ulinzi ya Azam FC, inapaswa kuonyesha kiwango bora leo dhidi ya Simba vinginevyo inaweza kuendelea kuigharimu timu hiyo kama ambavyo imekuwa ikifanya msimu huu.

Katika mechi tano zilizopita, timu hiyo imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane ikiwa ni wastani wa bao 1.6 kwa kila mechi. Simba wamekuwa na rekodi nzuri pindi wakutanapo na Azam FC kwenye Ligi Kuu na kuthibitisha hilo, katika mechi 10 zilizopita baina yao, Simba wameshinda tano, wakatoka sare nne Azam imepata ushindi katika mchezo mmoja.

Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema kikosi hicho kitakuwa na mabadiliko makubwa na wataanzisha sura zote zilizopumzishwa kwenye mechi iliyopita ambazo hazipungui tano.

“Ni mechi kubwa baina ya timu nzuri. Tutajitahidi kucheza kwa kiwango chetu bora ili tuweze kupata matokeo mazuri na naamini mechi tavutia kuitazama,” alisema Pablo.

Kocha msaidizi wa Azam, Iddi Abubakar alisema wamejiandaa vyema kuikabili Simba na wanaamini wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.

“Tunawaheshimu Simba ni mabingwa watetezi na wanshika nafasi ya pili wakiwa na kiwango kizuri lakini kwa maandalizi yetu sisi tuko tayari kupambana na Simba,” alisema Abubakar. Mechi hiyo imekuwa gumzo mitaani na kwenye mitandao ya kijamii ikifahamika zaidi kama dabi ya Mzizima. Timu hizo zimesajili wachezaji wenye majina makubwa na uzoefu ambao muda wowote unaweza kuamua mechi.