Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kisa cha Mwalimu Nyerere, Kenyatta kutolipenda soka

KATIKA miaka ya 1960 na 1970 ilikuwa kawaida kwenda kuangalia mchezo wa kandanda Zanzibar au Uganda na kuona viongozi wa nchi hizi, Rais Abeid Amani Karume (Zanzibar) na Rais Milton Obote (Uganda) wamefika uwanjani bila ya kutarajiwa.

Wakati Rais Obote alifika katika michezo ya klabu kubwa za nchi hiyo na ya kimataifa mzee Karume, alionekana uwanjani hata pale timu za madaraja ya chini au za watoto zilipocheza.

Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere alionekana mara chache kwenye michezo ya kandanda, lakini Rais wa Kenya, Jomo Kenyatta alikuwa haendi kabisa baada ya tukio lililomuudhi alipofika uwanjani siku moja timu ya Kenya ilipocheza.

Rais Kenneth Kaunda wa Zambia alifika uwanjani katika karibu kila mchezo wa kimataifa kuishangilia klabu au Timu ya Taifa ya Zambia.

Nilichogundua ni kuwapo sababu tofauti zilifanya mzee Kenyatta na Mwalimu kuwa na mtazamo huo kwa mchezo wa kandanda.

Mwalimu hakuwa akipenda sana kandanda kama alivyopenda bao, ijapokuwa alifuatilia maendeleo ya soka na mzee Kenyatta alikuwa akipenda sana riadha na mchezo wa ndondi.

Mzee alikuwa hapendi ndondi na mara nyingi alisema mtu hutakiwa kupigana dhidi ya njaa na sio kupigana na binaadamu mwenzake.

Siku moja nilipokuwa Tanga kama mwandishi mwanzoni mwa mwaka wa 1967 nilikwenda Mombasa kuangalia mchezo wa kandanda wawatani wa jadi wa mji huo, Feisal na Mwenge.

Nilipofika klabu ya Feisal nilikutana na marafiki zangu Ali Kajo, Ahmed Breik na Kadir Farah ambao walinielezea masikitiko yao kufuatia kuhama kwa golikipa waliyemtegemea sana, Mtanzania Kitwana Ramadhani Manara ‘Popat’.

Wakati ule Kitwana aliondoka Mombasa alikokuwa akichezea Timu ya Feisal nakurudi Dar es Salaam na kujiunga na klabu ya Cosmopolitan kabla ya kujiunga na Yanga huku akiwa golikipa namba moja wa timu ya taifa.

Katika mazungumzo yangu na wazee na wachezaji maarufu wa soka wa zamazile wa klabu ya Feisal, nilielezewa siri iliyokuwa imejificha ya mzee Kenyatta kukataa kwenda uwanjani hata timu za Kenya au ya taifa zilipocheza mashindano ya kimataifa.

Siku moja nikamuuliza rafiki yangu, Poly Fernandes, aliyekuwa Mhariri wa Michezo wa magazeti ya Daily Nation katika miaka ya 1970 kwa nini mzee Kenyatta alikuwa haendi kuangalia kandanda.

Jawabu yake ilikuwa: ”Eeh bhana wee, hii suala usiulize, mambo makubwasana. Mimi siwezi toa jibu”.

Wakati ule nilisikia mara nyingi mzee Kenyatta alialikwa kuwa mgeni wa heshima katika michezo mikubwa ya kandanda iliyofanyika Nairobi au Mombasa, lakini alikataa na kusema hataki mualiko wowote wa kwenda kwenye mchezo wa kandanda.

Uamuzi huo wa mzee Kennyatta ulitokana na hasira aliyoipata mwaka 1965 pale timu ya Taifa ya Ghana, Black Stars, ilipocheza dhidi ya Harambee Stars ya Kenya Nairobi wakati wa sherehe za mwaka mmoja za uhuru wa nchi hiyo.

Mzee Kenyatta alikuwa mgeni wa heshima katika mchezo ule ambapo Ghanailikuwa mabingwa wa soka wa Bara la Afrika.

Timu ya Kenya ilikuwa na wachezaji mashuhuri wa zama zile kamaJonathan Niva, Chege Ouma na Nicodemus Arudhi na Ghana ilikuwa nawachezaji waliosifika zama zile kama Frank Odoi, Kofi Pare na Mathew Amoah.

Katika mchezo ule Kenya ilielemewa vibaya sana na wakati wa mapumzikoGhana ilikuwa inaongoza 6-1.

Wakati wachezaji walipokwenda mapumziko mzee Kenyatta alisimama akiwa amekasirika na alipoulizwa alikuwa anakwenda wapi alisema: ”Na mimininakwenda kupumzika.”

Aliondoka uwanjani na mchezo uliendelea na filimbi ya mwisho iliwakutaWakenya wamelala 13-2 wakati mzee Kenyatta akiwa amepumzika Ikulu ya Gatundu.

Kwa mujibu wa maelezo ya mchezaji maarufu wa Kenya, Joe Kadenge, Mzee Keyatta alipoona Timu ya Kenya inaendeshwa mchakamchaka nakuelemewa alitaka aingizwemwanariadha mashuhuri wa nchi hiyo, Kipchoge Keino kuokoa jahazi.

Alipoambiwa kwamba Keino alikuwa ni mwanariadha na siyo mchezajikandanda alikasirika na kusema alikuwa anaamini kama Keino angekuwemokatika kile kikosi cha Harambee Stars wachezaji wa Ghana wangeshikaadabu zao.

Tokea siku ile mzee kenyatta alifika katika uwanja kukagua gwaride au kuhutubia mkutano tu na siyo kuangalia mchezo wa kandanda.

Siku moja nilipomuuliza beki maarufu wa Kenya wa zama zile, Jonathan Niva, wakati akiwa mshauri wa timu ya taifa ya Kenya katika miaka ya 1980 hali ilikuwaje hatawakafungwa mabao 13 dhidi ya Ghana, aliniambia waljikuta wamezidiwa na kuchezeshwa kama watoto wadogo.

Aliniambia maumivu aliyoyapata kwa kile kipigo kile cha 13-2 alikuwa hawezi kuyasahau maishani mwake.

Vile vile nilipokuwepo Ghana mwaka 1975 kama mwandishi wa DailyNewsnilikutana na baadhi ya wachezaji wa kile kikosi cha Black Stars kilichofanya mauaji Kenya siku moja kabla ya Simba ya Dar es Salaam kufika Accra kucheza dhidi ya Hearts of Oak ya jiji la Accra.

Mathew Amoah, rafiki mkubwa wa Ken Bediako aliyekuwa Mhariri wa Michezowa gazeti niliokuwa ninalifanyia kazi la Daily Graphic aliniambia:

”Tulipunguza kasi ya mcheo kipindi cha pili kwa vile tulihisi kama tungelifunga mabao mengi zaidi tungeacha balaa kubwa zaidi kwa wenyeji baada ya kuondoka Kenya.”

Mwalimu Nyerere alikuwa siyo mshabiki sana wa kandanda, ijapokuwaalielewana sana na viongozi wa Yanga.

Mara chache alikubali kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa kandanda, lakini alikasirishwa siku alipokwenda Uwanja wa Taifa kama mgeni wa heshima na kuona timu ya Tanzania iliyokuwa inacheza na Sudan dhidi ya kuongozwa na nahodha marehemu Abrahman Juma ikiingia uwanjani na wachezaji wakiwa tumbo wazi kwa vile hapakuwepo na jezi.

Mzee Karume ambaye naye alikuwa shabiki mkubwa wa klabu za Kisimamajongo (Unguja), Yanga na Liverpool ya Uingereza alichukiamchezo wa rafu na hakupendamchezo wa ndondi ambao alisema ni wa kishenzi.

Siku moja aliamuru mchezo kati ya timu ya Mwadui na KMKM uvunjwe kwa vile aliona wachezaji wa Mwadui walikuwa wanacheza mchezo mchafu.

Alitoa amri kwa timu hiyo kupelekwa uwanja wa ndege na kundoka Zanzibarharaka.

Aliipiga marufuku Mwadui kutembelea Zanzibar na kwa kwelihaikufika Visiwani tena kucheza mpira wakati wa uhai wake.

Mara nyingi timu ya taifa ya Zanzibar ilipopiga kambi kama ilivyokuwamwenyeji wa michuano ya mwisho ya Kombe la Gossage mwaka 1966, aliwatembelea wachezaji asubuhi na jioni.

Alikuwa anaangalia mazoezi nakutoa ushauri kwa wachezaji na hata kuingia uwanjani kupiga danadana.

Kwa mujibu wa kumbukumbu Rais Obote mara nyingi alimaliza mapema aukuvunja mikutano yake muhimu kama ya baraza lake la mawaziri ili aendekuona mchezo wa kandanda.

Mara nyingi alifika uwanja wa Nakivubo, Kampala, kuangalia michezo ya kandanda bila ya kutarajiwa.

Hata alipofanya ziara za nchi za nje, kama Uingereza na Tanzania alipendelea kwenda kuona michezo mikubwa ya soka.