TRA United yakaribia kumnasa Pogba
Muktasari:
- Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, umeliambia Mwanaspoti mchezaji huyo amefika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha taratibu zote za kusaini mkataba wa kukichezea kikosi hicho, ili kuongezea nguvu katika eneo la kiungo.
KLABU ya TRA United iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo mkabaji, Venold Dzaba ‘Pogba’ kutokea Klabu ya AS Otoho d’Oyo ya Congo Brazzaville, baada ya pande mbili kufikia makubaliano ya kumsajili nyota huyo.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, umeliambia Mwanaspoti mchezaji huyo amefika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha taratibu zote za kusaini mkataba wa kukichezea kikosi hicho, ili kuongezea nguvu katika eneo la kiungo.
Nyota huyo aliyewahi kucheza Tongo FC, CARA Brazzaville, Inter Club de Brazzaville, AC Leopards de Dolisie kisha kutua AS Otoho d’Oyo zote za kwao Congo Brazzaville, ni pendekezo la kocha mkuu wa kikosi hicho, Mrundi Etienne Ndayiragije.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa TRA United, Christina Mwagala amesema timu hiyo imeingia kambini tangu Julai 15, 2026, kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2026-2027, japo suala la usajili bado linaendelea na halijakamilika.
“Tunaendelea na maandalizi yetu kwa ajili ya msimu ujao wa 2026-2027 na tutakapokamilisha taratibu zote za usajili mpya tutaanza rasmi kutangaza mmoja baada ya mwingine, mashabiki zetu wategemee kuwaona wachezaji wakubwa,” amesema Mwagala.
Pogba anaenda kuungana na wachezaji wengine wapya waliosajiliwa wakiwemo kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin aliyejiunga na timu hiyo baada ya kuachana na Simba aliyoitumikia kwa miaka 10, tangu aliposajiliwa mwaka 2016, akitokea Mtibwa Sugar.
Mwanaspoti linatambua nyota wengine waliokuwa katika hatua za mwisho za kujiunga na TRA United katika dirisha hili la usajili ni viungo pia wakabaji, Salmin Hoza kutoka Dodoma Jiji na Greyson Gerald Gwalala kutokea timu ya Coastal Union.
Mbali na usajili wa nyota hao wanaoenda kuongeza nguvu katika kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa 2026-2027, ila pia timu hiyo inakaribia kupata saini ya beki wa kati wa Geita Gold, Charles Komanya baada ya dili hilo kufikia hatua nzuri.