Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jeshi la Kaze balaa jipya

KIKOSI kazi cha Kaze kina jambo lake msimu huu. Na katika kuthibitisha jeshi la Yanga linataka kurejesha utawala wa soka nchini mikononi mwa Wanajangwani, nyota wake wamebadilisha upepo wa mwenendo wao na takwimu zinathibitisha hilo.

Habari njema kwa Yanga ni kwamba tofauti na timu nyinginezo, wao mabao yanatokea pembe zote za uwanja, hamna mchezaji mmoja anayesubiriwa afunge.
Kufikia sasa nusu msimu, katika kikosi cha kwanza cha Yanga ni wachezaji watatu tu ambao hawajafunga bao ambao ni kipa Metacha Mnata, beki wa kulia Kibwana Shomari na beki wa kushoto, Yassin Mustafa. Hii ni habari mbaya kwa wapinzani.

Kubwa zaidi, Yanga imeonekana kuongezeka ubora katika siku za hivi karibuni tofauti ilivyokuwa mwanzo wa msimu.

Katika mechi tatu zilizopita, Yanga imefunga jumla ya.mabao 11 na kuruhusu bao moja tu. Hali hii ni tofauti kabisa na mwanzo wa msimu ambapo iliingia kweñye ligi kwa kuchechemea na ilihitaji mechi 7 ili kufikisha mabao 11.

Kutokana na kusajili nyota wapya wengi, Yanga ilitarajiwa ichukue muda kidogo kwa wachezaji wake kuzoeana na kocha kutengeneza pacha zake za uwanjani.

Hata hivyo, haikutarajiwa kama gari la Wananchi lingekuwa limeshawaka mapema kiasi hiki. Lakini huo ndio ukweli. Gari Yanga limeshawaka.

Mechi tatu zilizopita tena zote za nje ya Dar es Salaam, Yanga imeshinda kwa idadi kubwa ya mabao, 5-0 dhidi ya Mwadui, 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji na 3-0 dhidi ya Ihefu, matokeo ambayo ilikuwa ni vigumu kuyapata mwanzoni mwa msimu.

Ujio wa straika Saidi Ntibazonkiza raia wa Burundi umesaidia kufanya mpira kuwa rahisi pale mbele tofauti na ilivyokuwa mwanzo wa msimu.


Katika mechi tatu alizochezea Yanga (ukijumuisha ya kirafiki moja waliyoshinda 3-0 dhidi ya Singida United), Saido amehusika moja kwa moja katika mabao sita kati ya yote tisa jumla waliyofunga Yanga katika mechi hizo tatu.

Hii ni sawa na amehusika katika zaidi ya asilimia 66 ya mabao yote ya Yanga waliyofunga katika mechi hizo tatu.
Saido katika mechi hizo tatu kafunga mabao matatu na katoa asisti tatu, mbili za mguu wa kushoto na moja ya mguu wa kulia ambayo alipiga frii-kiki aliyoitumia beki wa kati wa Yanga, Bakari Mwamnyeto kufunga bao dhidi ya Dodoma Jiji.

Saido, nyota wa timu ya taifa ya Burundi aliyecheza soka katika Ligi Kuu kubwa duniani kama ya Uholanzi na Ufaransa, ana bao moja na asisti tatu katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara aliyotua katika dirisha hili dogo la uhamisho lililofunguliwa Desemba 16.

Habari njema zaidi kwa Yanga ni kwamba pacha za kocha Cedrick Kaze zinazidi kuiva kwenye kona zote za uwanja, tofauti na ilivyokuwa hapo mwanzo wakati wachezaji hao ambao wengi ni wapya kikosini walipokuwa wakijaribu kuzoea mazingira.
Langoni inaonekana Metacha ameanza kujihakikishia namba dhidi ya Mkenya Farouk Shikhalo lakini maeneo ambayo hayana maswali ni pacha ya mabeki wa kati inayoundwa na Mwamnyeto na nahodha Lamine Moro.

Pacha nyingine hatari Yanga ni ya viungo wa ulinzi Mukoko Tonombe na Feisal Salum ambao pamoja na kusaidia kuulinda ukuta wa Mwamnyeto na Lamine, pia wanapeleka mashambulizi mbele, wana asisti za mabao na kufunga wao wenyewe pia.
Yacouba Songne na Deus Kaseke ni pacha nyingine ya hatari sana Yanga.

Wawili hao mbali na kuelewana mikimbio yao uwanjani wana jicho la mabao. Wawili hawa wamehusika katika mabao zaidi ya 10 msimu huu. Kaseke amefunga mabao manne na ana asisti nne kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, huku pia Yacouba akifunga mabao manne na asisti nne.

Kasi ya winga Tuisila Kisinda katika kupandisha mashambulizi inawavuruga sana wapinzani na ushirikiano wake na pasi zenye macho za Saido, si ajabu Yanga ikizidi kuimarika kila uchao.

Kiungo wa zamani wa Simba, Amri Kiemba alisema kuwa mabadiliko ya Yanga chini ya Kaze ni zaidi ya kufunga mabao tu.

“Ukiitazama timu kwa sasa wachezaji wanacheza kwa umoja wa hali ya juu, hawamtegemei mshambuliaji pekee afunge hivyo hivyo hata kwenye kukaba wanakaba wote wakijua wanadaiwa kitu na mashabiki wa Yanga,” alisema Kiemba.

Mchambuzi wa soka na kocha Alex Kashasha alisema: “Mwalimu Kaze alichofanikiwa zaidi ni kuweza kubadili ujuzi wake alionao kutoka kichwani mwake kwenda kwenye miili ya wachezaji wa Yanga, aana talanta kubwa ya kufundisha.”