Gomes: Naanza na Dodoma Jiji

KOCHA wa Dodoma Jiji, Mbwana Makata ameongeza dozi akijiandaa kupambana na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopangwa kufanyika kesho Uwanja wa Jamhuri, Dodoma lakini mwenzie, Didier Gomes ametamba anaanza nao.
Gomes amesisitiza hakuna kingine wanachotaka zaidi ya ushindi kwani itawarahisishia mechi ijayo ya Azam pamoja na michuano ya kimataifa.
Mchezo huo wa kiporo umepangwa kuanza saa 10 jioni na Makata amesema anatarajia matokeo mazuri ili kupanda nafasi ya tano katika msimamo wa ligi.
Dodoma Jiji FC kwa sasa ipo katika nafasi ya 10 kwa kujikusanyia pointi 22 zilizotokana na mechi 17 na ushindi itapanda mpaka nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo.
Simba ipo nafasi ya pili na kwa kuwa na pointi 35 zilizotokana na michezo 15.
Makata alisema kwa sasa wanaweza kukabiliana na Simba muda wote wa mchezo katika spidi na stamina ile ile kwani programu za mazoezi wameziboresha zaidi tofauti na mechi za nyuma kwani sasa hawako tayari kuangusha pointi yoyote.
“Kwa sasa tupo kambini Kondoa kujiandaa na mechi hiyo, wachezaji wawili, Seif Karie na Justine Omary hawatacheza mechi hiyo kutokana na kua majeruhi.
Ila kuna wachezaji wapa watatu, Manyika Junior, Erick Nkosi kutoka Mwadui na Omari Daga aliyekuwa timu ya Biashara nao wameingia katika timu. Naweza kusema tupo tayari kwa mapambano,” alisema Makata. Alisema ameiona Simba kwenye mashindano ya Super Cup na ina wachezaji wazuri, lakini wasitarajie mteremko.
“Simba ina heshima yake Ligi Kuu Bara kwani ndiyo mabingwa watetezi. Wameweza kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hapa tunazungumzia Ligi Kuu ambayo inamikiki mikiki yake, program yangu ya mazoezi imebadilika kabisa kwani na sisi tunahitaji matokeo mazuri,” alisema.
Alifafanua wamefanya mazoezi kwa malengo maalumu na wanaamini watafanikiwa kuisimamisha Simba kupata matokeo mazuri katika mechi hiyo.
MSIKIE GOMES
Kocha Gomes amesema baada ya kuchukua kombe la Simba Cup akili yake kwa sasa ameigeuzia Ligi Kuu.
“Nataka ubingwa wa Ligi Kuu hili ndio lengo kubwa, tukichukua ubingwa huo maana yake tutashiriki tena Ligi ya Mabingwa Afrika na hilo ndio lengo letu sisi,” alisema Gomes ambaye anasifika kwa kuusoma mchezo.
“Tunatakiwa kushinda katika mechi ya Dodoma na Azam, najua ni mechi ngumu kwetu lakini tunatakiwa tushinde ili kujiweka katika nafasi nzuri ya ubingwa,”alisema . Simba jana Jumanne waliingia kambini tayari kwa mchezo huo.