Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga na jiwe moja la manati lililoua njiwa wawili

JICHO Pict


NDANI ya saa chache kulikuwa na kazi mbili ambazo Yanga walilazimika kufanya juzi jioni. Pacome Zouzoua alilazimika kuipeleka Yanga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Injinia Hersi Said alimtangaza kocha mpya wa Yanga.


Hii kazi ya kwanza haikuwa ngumu sana ingawa bado ingeweza kufanywa kwa ukamilifu zaidi kuliko ilivyofanyika. Yanga waliingia uwanjani wakiwa na kocha msaidizi, Patrick Mabedi huku wakiwa wametanguliwa na kichapo cha bao 1-0 wiki moja iliyopita walichopokea kule Blantyre.


Kocha aliyefukuzwa, Roman Folz alikuwa ameiweka Yanga pabaya baada ya kuendelea kucheza mechi nyingine mbovu na akafukuzwa saa chache baada ya pambano hilo kumalizika. Na juzi Yanga walitarajiwa wacheze pambano safi kuwakumbusha Wanayanga kuhusu ubora wao.

Na kweli, ndani ya dakika 45 walikuwa wanakaribia kufunga hesabu. Mbao yao mawili yalitoka kwa watu muhimu. La kwanza lilifungwa na nahodha, Dickson Job. Alinikumbiusha nahodha mwingine wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Kwenda kufunga katika kona ya kwanza ya lango kutokana na mpira wa kona.

YAN 01

Katika mechi kama hizi nahodha inabidi acheze akionyesha mfano kwa wenzake. Bao la Job lilikuwa muhimu. Mechi ambayo lazima ushinde na kufanya ‘comeback’ nahodha anapaswa kusimama na kuhesabiwa. Job aliifanya kazi hiyo.

Bao la pili lilifungwa na staa wa timu, Pacome. Ukiachana na Djigui Diarra ambaye huwa anasimama umbali wa mita 100 kutoka lango la wapinzani, Pacome anabakia kuwa mchezaji staa zaidi wa Yanga uwanjani, hasa katika eneo la mwisho.

Mara nyingi Pacome anafanya mambo yatokee. Zaidi na zaidi ni kila siku anaendelea kuthibitisha yeye ni mchezaji wa mechi kubwa. Ndicho alichokifanya juzi. Namna ambavyo huwa hapotezi nafasi nyingi katika mechi.

YAN 02

Kwa jumla Yanga walipaswa kufunga hesabu zao kwa kufunga bao jingine kipindi cha pili. Hata hivyo, hawakufanya hivyo na matokeo yake waliendelea kushikilia roho zao kwa sababu kama Wamalawi wangefunga bao lolote basi Yanga wangekuwa wametolewa kwa bao la ugenini.

Lawama zinakwenda kwa wachache lakini hasa Prince Dube. Sijui ni kitu gani kimemkumba Jangwani. Alikosa mabao ya wazi na mwisho alitolewa nje huku akienda kumwaga machozi katika benchi. Dube anahitaji msaada.

Dube anahitaji faraja. Ni mchezaji ambaye tunajua ubora wake lakini hizi timu zetu kubwa zina mambo mengi ndani na nje ya uwanja. Tangu atue Yanga amekosa mwendelezo wa ubora. Na kitu kibaya zaidi ni anaonekana hana roho ngumu.

YAN 03

Kuna wachezaji wanapitia vipindi kama hivi lakini wanakombolewa kwa kuwa na roho ngumu. Dube anaonekana hana roho hiyo na anahitaji kusimamiwa kwa karibu kwa sababu kadri anavyojihisi hatia ndivyo ambavyo uwezo wake wa kujiamini unavyotoweka.

Tukiachana na Dube ukweli ni Yanga juzi walionekana walau wanatamani kufanya jambo. Walijaribu kwenda na kasi ambayo miaka ya karibuni iliwafanya mashabiki wao wajione wapo katika dunia nyingine. Hata hivyo, katika kipindi cha pili hawakuonekana kuwa na kasi kama ya kipindi cha kwanza.

Bahati nzuri pambano lenyewe lilikuwa likitazamwa na kocha mpya wa Yanga, Pedro Concalves na wasaidizi wake wawili katika makochi ya ofisi moja iliyo ndani ya jengo la Salamander pale Posta. Yanga walikuwa hawajui kama kocha wao amefika na angetambulishwa baada ya mechi.

YAN 04

Na kweli, muda mchache bada ya kuitoa Silver Stars, Concalves ambaye ni raia wa Ureno alitangazwa kocha mpya wa Yanga. Nadhani baada ya kuiona Yanga atakuwa anajua ugumu wa kazi inayomkabili mbele yake.

Lakini ingependezwa pia aonyeshwe ile Yanga ambayo ilikuwa inaziadhibu timu nyingi mabao matano matano, halafu aonyeshwe Yanga ya Roman Folz kabla ya kujua ugumu wa kazi iliyo mbele yake. watu wa Yanga wanataka Yanga yao irudi kama ilivyokuwa wakati wa Professa Nabi, kisha Manuel Gamond, halafu Saed Ramovic na kisha Miloud Hamdi.

Kama Pedro akiwarudisha huko basi Yanga watakuwa na uhakika wa kufanya kitu katika mechi za makundi. Kama hawatarudi huko basi Yanga hawatakuwa na uhakika na wanachokwenda kufanya katika hatua ya makundi.

YAN 05

Yanga hii imemfanya hata Djigui Diarra kupewa kadi ya njano kwa kupoteza muda katika pambano dhidi ya timu kutoka Malawi. Wameshuka chini kwa kiasi kikubwa. Hii sio Yanga ambayo iliwafanya Mamelodi Sundwons washike roho pale Pretoria, sio Yanga ambao waliitoa Club Africain kwao pale Tunisia, sio Yanga ambayo ilimchapa mtani mabao matano wakaweza mabango, sio Yanga ambayo ilishinda pambano la fainali za Shirikisho dhidi ya USM Alger pale Algiers ingawa hawakupewa kombe.

Pedro ana kazi ya kuwarudisha huko. Wasifu wake ni tofauti na Folz. Walau yeye ameshinda vitu mahala akiwa na timu kama kocha mkuu. Ametwaa mataji ya Cosafa na Angola mara mbili mfululizo. Unaweza kumshikia dhamana kwa wasifu wake kuliko ilivyokuwa kwa rafiki yetu Folz.

YAN 06

Hata hivyo, ana kazi ngumu ya kufanya kuanzia sasa hivi hadi mwishoni mwa msimu huu. Ana kazi tatu za msingi. Kwanza kabisa kuipeleka Yanga katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya mabingwa. Yanga huwa wanasuasua katika eneo hilo.

Pili ni kuipatia Yanga ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi kuu Bara. Makocha kadhaa waliifanya kazi hiyo katika misimu minne iliyopita. Folz hawezi kuhesabika katika kazi hii kwa sababu amedumu Yanga kwa wiki chache.

Pia Pedro ana kazi ya kuendeleza vichapo kwa mtani. Ni kazi ya kijinga lakini wenyewe wanaipa kipaumbele. Folz walau alipata bahati katika hilo katika ushindi dhaifu pengine kuliko ushindi mwingine wowote wakati wakiendeleza vichapo vya mfululizo.

Usishangae Pedro akahukumiwa kwa hilo. Kwamba makocha tofauti wameifunga Simba mara tano mfululizo lakini yeye akishindwa akahishia kulaumiwa. Nawajua mashabiki wanazi wa timu hizi namna walivyo na nongwa katika mambo haya.

Kila la kheri kwake. Hatujui kama amekuja na begi dogo au begi kubwa lakini Yanga wanatazamia makubwa kutoka kwake. Miaka ya karibuni wamedekezwa na mpira mzuri.