Prime
Bahati mbaya Folz hakuishi wanavyotaka Yanga
MPIRA miongoni mwa michezo ya kikatili duniani. Uwanjani na nje ya uwanja. Na ajira ya mpira nayo usiitilie maanani sana. Juzi jioni watu wawili wamefukuzwa kazi angali wakiwa wanatoa jasho uwanjani.
Kocha wa Nottingham Forest, Ange Postecoglu alipoteza kazi yake akiwa uwanjani kabla ya Basi la timu halijaondoka uwanjani baada ya Forest kuchapwa mabao 0-3 nyumbani na Chelsea. Ilitokana na mfululizo wa matokeo mabovu tangu airithi kazi hiyo kutoka kwa kocha Mreno, Nuno Santo. Tajiri alimpa mkono wa kwaheri pale pale uwanjani wakati Chelsea wakishangilia matokeo.
Maili nyingi kutoka Nottingham pale England mpaka Blantyre Malawi, Yanga nao walifanya hivyo hivyo. Walimpa mkono wa kwaheri kocha ambaye hawakuwahi kumuelewa. Roman Folz. Naye jasho lilikuwa linamtiririka baada ya Yanga kufungwa 1-0 na timu ndogo ya Malawi, Silver Stars. Ilikuwa mechi ya kijinga ya hatua za awali kuelekea makundi ya Ligi ya mabingwa.
Vitu viwili havikuona katika ndoa hii ya Yanga na Folz. Yanga hawasemi tu lakini ndoto yao kubwa ni kufika hata nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Na msimu huu Injinia Hersi Said alikuwa amepambana kuhakikisha anaziba nafasi za kina Aziz Ki kwa kuleta wachezaji wa maana kikosini ili kutimiza ndoto za Yanga.
Alileta kina Celestin Ecua, Lasine Kouma, Andy Boyeli, Mohammed Hussein Tshabalala, Momo Doumbia na wengineo. Kwa sifa ambazo tumesikia ni walikotoka walikuwa wachezaji bora. Kwa kuwaona kwa macho yetu bado ni wachezaji wazuri lakini wanacheza katika Yanga isiyo bora kuliko Yanga ambazo tumeziona kwa miaka minne iliyopita.
Hapo ndipo ndoa ya Yanga na Folz ilipofia. Niliwahi kuandika mahala Folz alikuwa na kazi nzito ya kufuata nyayo za makocha waliopita Yanga katika misimu minne iliyopita. Kufuata nyayo za Nasireddine Nabi, Miguel Gamondi, Saed Ramovic na Miloud Hamdi. Wote waliiweka Yanga katika mlengo wa kuutawala mpira uwanjani.
Bahati mbaya Folz hakuweza. Tulitazama mechi nyingi za Yanga uwanjani lakini haikuwa Yanga ile ambayo ilikuwa inakushambulia, inakufunga, halafu aliyefungwa anapoteza muda. Ilikuwa Yanga tofauti isiyo na makali. Kuanzia mechi dhidi ya Rayon Sports, Bandari katika wiki ya Mwananchi, dhidi ya mtani Simba, na nyinginezo mpaka juzi.
Kabla ya Folz Yanga walikuwa wanakufunga kadri wanavyojisikia. Kocha wao aliyepita, Hamdi aliishia pazuri. Ilikuwa ni katika pambano dhidi ya watani Simba. Clement Mzize akafunga bao la pili lililofunga msimu mzima wa ligi baada ya mabishano marefu kuhusu uwepo wa pambano lenyewe. Folz alipaswa kuanzia hapo lakini kadri dakika zilivyosogea alionekana hana maajabu.
Tatizo la Folz ni kama lile la mchezaji anayeitwa Jean Charles Ahoua. Uwanjani namba ni nzuri lakini mpira wake haukufurahishi. Ahoua anabebwa na namba zake ni kama Folz alivyokuwa anabebwa na namba zake. Mpira wake ulikuwa haufurahishi ingawa namba zake hazikupi sababu ya kumfukuza. Hata juzi wakati anafukuzwa Yanga hilo ndio lilikuwa pambano la kwanza kwa Folz kufungwa.
Hata hivyo, Yanga wanaijua timu yao. Wanaijua vema. Kila wakiitazama Yanga yao walikuwa wanajua sio ile waliyokuwa wameizoea. Ile Yanga ya kupiga watu bao tano tano haikuwa hii. Ile Yanga ambayo mtani alichezea mabao matano na matokeo yakapelekwa katika mabango mitaa ya jiji la Dar es salaam.
Nani alaumiwe? Anaweza kuwa Injinia Hersi Said mwenyewe. Yanga ilifika fainali za Shirikisho miaka ya karibuni. Yanga ilitolewa robo fainali. Yanga ilitolewa pia makundi. Hersi anajua ndoto za Wanayanga. Huwa wananyanyasika kwa mashabiki wa mtani zao kwa kutofanya vizuri katika michuano ya CAF. Ligi ya mabingwa.
Wakati huu wakiwa wamesajili wachezaji wazuri huku akiendelea kumiliki wachezaji mafundi kama kina Pacome Zouzoua, Hersi akaitafutia Yanga kocha mwanafunzi. Ukitazama wasifu wa Folz, alikuwa amepita katika klabu kadhaa akiwa kama kocha msaidizi. Hajawahi kuwa kocha mkuu wala kutwaa taji lolote muhimu katika maisha yake ya mpira.
Unawezaje kutimiza ndoto zako ukiwa na kocha wa namna hii. Katika lugha ya mtaani ya Waingereza tunaweza kusema Hersi na wenzake walikuwa wamecheza kamari. 'Gambling'. Haukuwa muda wa Yanga kucheza bahati nasibu. Ulikuwa muda wa wao kuwa na kocha ambaye ana uzoefu na anaweza kuishi katika falsafa zao.
Matokeo yake Yanga wamejiweka katika hatari. Wameshafungwa ugenini na wageni wao wanaweza kuja na mbinu za ajabu. Injinia Hersi na masela wake ambao wanaongoza Yanga sasa hivi hawakufikiria kama wanaweza kuwa katika nafasi hii kwa sasa. Wakati wao wanaiwaza nusu fainali au fainali, tayari wapo hatarini kutofika hata makundi.
Hauwezi kumpa nafasi kocha ambaye unataka atafutie wasifu katika timu kubwa. Ni makocha wachache ambao wameweza kukulia katika timu wakafanya maajabu. Mfano ni Pep Guardiola ambaye alitolewa Barcelona ya vijana na kwenda kufanya makubwa katika timu ya wakubwa. Tena alicheza kamari kwa kuachana na Deco, Ronaldinho na Samuel Etoo baada ya kufika timu ya wakubwa.
Vinginevyo timu kubwa nyingi zimeachana na ujinga wa kujaribu kuwakuza makocha vijana. Wanahitaji makocha ambao tayari wana wasifu katika maisha yao ya soka. Wengine wanajaribu kuchukua wasifu mdogo lakini bado mambo yanawatokea puani. Mfano ni Manchester United. Walimchukua Erik Ten Hag akiwa kocha bingwa wa Ligi kuu ya Uholanzi pamoja na kufika nusu fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya lakini mambo yakawa magumu.
Walimchukua pia Ruben Amorim akiwa na ubingwa wake wa Ureno lakini maisha mpaka sasa ni magumu pale Old Trafford. Yanga ikaamua kujaribu maisha kwa kocha ambaye hakuwa na wasifu wowote katika soka la Afrika. Ni afadhali wangemchukua kocha mwenye uzoefu wa soka la Afrika kama Micho au Pitso Motsimane.
Sasa tusubiri kuona nini kitafuata baada ya Folz. Nadhani Yanga watakuwa wamejifunza kitu. Sidhani kama watakwenda kwa kocha mwanafunzi. Wanalazimika kwenda kwa kocha ambaye wana uhakika na wasifu wake. Bado ni suala la bahati nasibu lakini walau bahati nasibu iwe inaeleweka. Bahati nasibu ya Folz haikueleweka.