Wachezaji wetu wanafeli hapa tu, wala hawashtuki
ALINIKUMBUSHA kitu rafiki yangu Ricardo Momo tukiwa katika studio za Wasafi wiki iliyopita. Wachezaji wetu wanaamini katika mpira kitu muhimu ni kuwa fiti tu. Basi. Hawashughuliki na mapungufu yao mengine uwanjani. Nadhani alikuwa sahihi.
Wachezaji wetu wanabakia pale pale walipo. Viwango vyao vinabakia pale pale vilipo kwa sababu hawafanyii kazi mapungufu yao. Wenzetu wachezaji wao wanafanyia kazi mapungufu yao na kuimairsha ubora wao siku hadi siku. Ni tofauti na wachezaji wetu. Makosa yao ni yale yale na uwezo wao wa kuimarika umekuwa mdogo siku hadi siku.
Baada ya mazoezi wachezaji wote wanaondoka. Hakuna ambaye anashughulika na mapungufu yake. Hakuna anayeimarisha ubora wake. Sidhani kama kuna wachezaji huwa wanabakia uwanjani kwa ajili ya kuwa tofauti na wengine. Sidhani kama kuna mchezaji anabakia katika uwanja wa mazoezi na kufanya mazoezi ambayo yanaweza kusababisha akawa tofauti na wengine.
Mambo mengi ambayo yanatokea katika mechi huwa yanaanzia katika viwanja vya mazoezi. Ni kweli kuna baadhi ya wachezaji wana vipaji fulani lakini wengine wameimarisha kwa kufanyia kazi mazoezi kile ambacho wanataka kifanyike katika uwanja wa mechi. Huwa wanabakia mazoezini kufanyia kazi kile ambacho wanataka kujitofautisha na wengineo.
David Beckham alikuwa anawahi mazoezini kwa ajili ya kufanya mazoezi ya peke yake ya kupiga mipira ya faulo. Tulichokuwa tunakiona katika mechi nyakati zile kilitokana na na mazoezi aliyokuwa anafanya mara kwa mara katika uwanja wa mazoezi.
Labda ndiyo maana kuna wakati Sir Alex Ferguson alimchukia Beckham alipompata Posh Spice kwa sababu alianza kupoteza umakini na kuwa bize na mambo ya nje ya uwanja.
Wachezaji wetu wanaamini katika vipaji vyao. Hawaamini katika utundu mwingine ambao wanaweza kuufanyia katika viwanja vya mazoezi. Labda ndiyo maana siku hizi hatuna watu maalumu (specialists) katika kazi nyingi maalumu uwanjani. Leo ndiyo maana wachezaji wengi hawawezi kurudia mara kwa mara vitu wanavyofanya uwanjani.
Mfano, hatuna mchezaji ambaye ni hatari katika kupiga mipira ya frii kiki. Na hata katika msimu huu ulioanza hivi karibuni katika ligi kuu ya NBC hakuna mchezaji ambaye anaweza kukuhakikishia kufunga walau bao moja la mpira wa faulo nje ya boksi. Ambaye atafunga mabao manne ya mipira hiyo nampa Sh1 milioni mwishoni mwa msimu.
Hapa karibuni, Aziz Ki aliingia kwa mikwara katika ligi yetu kwa kupiga frii kiki nzuri aliyomfunga Aishi Manula katika dabi ya watani wa Kariakoo. Baada ya hapo kila alipokuwa anarudia alikuwa anapiga nje. Kumbe si ajabu kitu alichotufanyia katika pambano lile kilikuwa kitu cha mara moja tu. Hakuwa anakifanyia sana mazoezi katika uwanja wa mazoezi kule Kigamboni.
Kabla yake, Bernard Morrison naye aliwahi kutufungia bao zuri la frii kiki dhidi ya Simba akiwa na jezi ya Yanga. Baada ya hapo kila alipopata nafasi ya kupiga tena mipira hiyo alikuwa anageuka kichekesho. Hakuweza kurudia tena. Ni suala hili hili ambalo lilimkumba Aziz Ki. Labda bao alilofunga siku ile lilitokana na kazi nzuri kazini lakini hakuwa mtaalamu hasa wa mipira hiyo.
Naambiwa mchezaji aliyekuwa na mwendelezo wa ubora katika mipira hiyo alikuwa David Luhende wakati akiwa na Kagera Sugar. Kuna msimu alifunga mabao manne ya frii kiki. Labda mashabiki wengi hawakufahamu hili kwa sababu sio mchezaji wa Simba au Yanga. Timu ambazo wachezaji wake wanaimbwa zaidi kuliko timu nyingine nchini.
Leo hatuna mchezaji ambaye anapiga kona za hatari kama ambavyo staa wa zamani wa timu ya Sigara na timu ya mkoa wa Dar es salaam, Ally Malilo alivyokuwa anafanya. Kila kona ambayo Malilo alikuwa anapiga ilikuwa ya hatari kama ambavyo Declan Rice wa Arsenal anafanya kwa sasa. Wachezaji hawafanyii kazi haya mambo. Nje ya uwanja wa mazoezi hakuna wanachoweza kufanya tofauti.
Huku katika ufungaji kuna matatizo mengi zaidi. Mshambuliaji akitazamana na lango anapaswa kufanya nini? Bukayo Saka amekuwa akirudia kufanya kile kile anachofanya kila wikiendi pindi anapotokea upande wa kushoto wa mashambulizi ya Arsenal. Anazungusha upande wa kulia wa golikipa na mara nyingi anafunga.
Mo Salah naye hivyo hivyo. Lionel Messi naye hivyo hivyo. Kuna sehemu ukiuzungusha mpira kipa hawezi kufika. Kila siku tunaona hivyo lakini kwa wachezaji wetu hatuoni hivyo. Nani ambaye anafanyia kazi hilo jambo. Nani anaweza kufunga walau mabao matatu kwa msimu kwa staili hii ya Saka? Hakuna. Walau nilimuona Clement Mzize akifanyia kazi jambo hilo akiwa mazoezini na timu ya taifa kule Morocco.
Wachezaji wetu hadi leo hawajui kama ukitazamana na kipa unapaswa kufanya na nini. Wakati wenzetu wanafanya kitu rahisi kuubetua mpira juu ya kipa sisi huwa tunapaparika na kuburuza mpira chini na kumuacha Djigui Diarra tukimuona kipa wa ajabu. Kumbe tatizo wachezaji wetu hawajifundishi kitu cha kufanya wakitazamana na makipa.
Siku hizi hata penalti huwa tunashika roho juu. Hatuna mtu ambaye tuna uhakika atakwenda kufunga penalti. Zamani walikuwepo wengi akiwepo Mao Mkami 'Ball dancer'. Labda mchezaji wa mwisho ambaye alikuwa anatuhakikishia kufunga penalti alikuwa ni Erasto Nyoni. Wengine ilikuwa maji kupwa maji kujaa.
Kuna mambo mengi binafsi ya kufanyia kazi. Hata mipira ya kichwa ni kitu cha kufanyia kazi. Hakuna kona ambayo tunaweza kuamini fulani anaweza kufanya jambo kama ilivyokuwa kwa Abeid Mziba au baadaye sana Mbwana Samatta. Hakuna kitu cha hatari sana kinachoweza kutokea katika kona au mpira wa krosi. Hakuna tunayeweza kumuamini kwamba anaweza kufanya kitu katika mpira wa kona au krosi.
Hapo hapo katika krosi kuna jambo pia. Walinzi wetu wa pembeni hawajui kupiga krosi. Hawatazami nani yupo wapi. Wengi wanapiga ili mradi mpira uende katika boksi. Na wengine huwa wanazidisha vipimo na mpira kwenda kurushwa katika upande mwingine wa uwanja. Hawafanyii kazi krosi zao.
Edibily Jonas Lunyamila staa wa zamani wa Yanga na taifa Stars aliwahi kuniambia krosi ni pasi kama pasi nyingine. Haupigi ili mradi ila unapaswa kumtazama ambaye unampelekea. Beki wa mwisho mzawa kupiga krosi vyema alikuwa ni Juma Abdul 'mnyamani'. Walinzi wetu wa pembeni wanapaswa kumtafuta na kumuuliza alikuwa anafanyaje.
Djuma Shaban pia alikuwa ni beki wa namna hii. Alikuwa hawezi kupiga krosi mpaka ajue anampelekea nani. Kuna marafiki watatu wanapaswa kubaki katika uwanja wa mazoezi kwa ajili ya kujiimarisha. Mlinzi wa pembeni, mshambuliaji na kipa. Wote wanahitaji kujua nini cha kufanya katika mipira ya namna hii. Hata hivyo wengi wanaondoka na basi la timu au magari yao binafsi pindi kocha anapomaliza mazoezi.
Matokeo yake leo hatuna watu maalumu katika maeneo maalumu. Wachezaji pekee ambao tunawasifia ni wale wanaoweza kupiga mashuti, kukimbia kwa kasi au kupiga chenga. Hatuna wataalamu wengine katika maeneo mengine. Kama wachezaji wetu wakiamua kuwa watu maalumu katika maeneo maalumu basi wanaweza kujitenga na wenzao.
Naweka ahadi ya shilingi milioni moja kwa mchezaji yeyote wa ligi kuu ya Tanzania ambaye atafunga mabao matatu au manne ya frii kiki katika msimu huu. Nadhani ifikapo Mei bado pesa yangu itakuwa salama kwa sababu sioni mchezaji ambaye anaweza kufanya hivyo kwa sasa.