Yanga ilivyovunja mwiko wa miaka 51
Muktasari:
- Ushindi huo muhimu umeifanya Yanga kufungua pazia la msimu kwa shangwe na hii ni mara ya pili kuchukua taji hilo ikiifunga Simba, ikifanya hivyo pia msimu uliopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa bao 1-0 pia.
YANGA jana Jumatano iliuanza vyema msimu wa 2026-2027 baada ya kubeba taji la tatu mfululizo la Ngao ya Jamii ilipoichapa Simba bao 1-0, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Ushindi huo muhimu umeifanya Yanga kufungua pazia la msimu kwa shangwe na hii ni mara ya pili kuchukua taji hilo ikiifunga Simba, ikifanya hivyo pia msimu uliopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa bao 1-0 pia.
MIAKA 51 YA USHINDI
Yanga imevunja mwiko wa kutoifunga Simba ndani ya dakika 90 zikikutana kwenye Uwanja wa Amaan na mara ya mwisho ilishinda mabao 2-0, Januari 1975 kwenye mechi ya Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
SIMBA YA MOTO 17 ZA KWANZA
Simba licha ya kupoteza mechi hiyo, lakini kama ukiangalia dakika 17 za kwanza kisha ukaambiwa walitoka kwa kipigo unaweza usiamini kutokana na namna walivyowabana Yanga, hata hivyo ikakosa hata kupata shuti lililolenga lango.
Ikitumia njia za pembeni, Simba ilipeleka presha kubwa kwa Yanga lakini ukuta wa mabingwa hao na viungo walimlinda vyema kipa wao, Djigui Diarra ambaye hakupata shida ya shuti lolote.
TATIZO SIMBA VIUNGO HAWA
Kama kuna wachezaji waliowapa wakati mgumu Simba kwenye mechi hiyo ni viungo watatu wa Yanga, Duke Abuya, Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya ambao walikuwa mithili ya mbweha wakiwabana wapinzani wao kutokamilisha hesabu zao.
Viungo hao watatu walifanya kazi kubwa kutibua hesabu za Simba na dakika 17 za kwanza walifanya kazi nzuri ya kuzuia lakini walishindwa kupiga pasi zilizofika, hatua ambayo iliwapa nguvu wapinzanio wao kwa kunufaika na mipira ya pili.
SIMBA VIUNGO WALIPOTEA
Viungo wa Simba, Clatous Chama, Anicet Ouara na Lebase Gueye hawakuwa kwenye ubora wao, nishati yao ya kukimbia sana haikuonekana kwa kiwango kikubwa, timu ilipokuwa chini nao walipotea na kuonekana wa kawaida katika mchezo huo.
YAO NI MMOJA TU
Beki wa kulia, Kouassi Attohoula Yao, juzi alikuwa kwenye kiwango kingine bora, aliwapa jeuri kubwa viongozi wake kwa uamuzi wa kuachana na Israel Mwenda kutokana na namna alivyojituma kwenye mchezo huo.
Yao alipotakiwa kupandisha mashambulizi alionekana, alipotakiwa kukaba alionekana, jamaa alikuwa kwenye kiwango bora kwenye mechi kubwa, kitu pekee ambacho kocha Manqoba Mngqithi alichoweza kufanya kwake wakati wa mchezo haikuwa kumuelekeza bali kumpigia makofi kwenye matukio mengi.
KANGWANDA FRESHI
Bao pekee lililoamua mchezo huo lilifungwa na winga mpya wa Yanga, Albert Kangwanda, ukiacha namna alivyomzidi akili beki wa Simba, Ismael Toure lakini jamaa ana uwezo mkubwa sana akiwa na mpira, anaweza kupenya kokote, kitu pekee kilichosalia ni kutulia kumalizia nafasi, alikuwa na uwezo wa kupiga hata Hat trick kwenye mchezo huo.
JABAAR KUNA MTU
Simba katika wachezaji wake ukiambiwa chagua mmoja ambaye alifanya kazi kubwa, jibu litakuwa rahisi ni kiungo wake mpya, Ibraheem Jabaar, jamaa hakuonyesha uoga kwenye mechi kubwa kama hiyo, alihaha uwanja mzima kuisaidia timu, unaweza kusema ni usajili bora wa Wekundu hao hadi sasa.
DOUMBIA APEWE MUDA
Siyo rahisi kumwambia shabiki wa Simba kwamba wampe muda mshambuliaji wao Ibrahim Doumbia lakini huo ndiyo ukweli halisi, alicheza dakika 45 za kwanza lakini ukitazama aliangushwa na anguko la viungo wa wekundu hao ambao walishindwa kumpa huduma stahiki.
Tazama namna viungo wa Yanga walivyojaribu kumtengenezea nafasi mshambuliaji wao Peter Shalulile lakini huduma kama hiyo hakuipata Doumbia, kuna kazi ambayo kocha wa Simba, Steve Barker anatakiwa kuenedelea kuifanya ili kutenegeneza kemia sasawasawa na raia huyo wa Mali na viungo wake.
UNAMDAI ARAJIGA?
Ilikuwa inazoeleka kwamba kila mchezo kama huo unapomalizika, lawama kubwa zinakuwa kwa waamuzi lakini sidhani kama atatokea mwenye lawama kwa waamuzi wa mchezo huo wakiongozwa na Ahmed Arajiga.
Jamaa alikuwa kwenye kiwango bora, alisimama imara kuamua matukio mengi kwa usawa lakini hata pale Simba ilipoomba msaada wa kurudiwa kwa tukio la mchezaji wake kuonekana kama amepigwa kichwani, alifanya uamuzi kwa usahihi
ARAFAT ZAIDI YA KIONGOZI
Kuna tukio lilitokea mwisho wa mchezo huo ambapo wakati wa kutoa zawadi, Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji alikuwa mbele ya rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said na ikaonekana kama medali ya ubingwa huo imesalia moja, jamaa akatumia busara sana iliyowashangaza wengi kwa kumtaka Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia kumvalisha Hersi, kisha yeye akakosa.