Kila la kheri Farid Mussa, Mkude
Muktasari:
- Tulishtuka kwa sababu katika wachezaji ambao hatukutegemea kama wangeichezea Coastal Union kwa msimu ujao, Farid ni mmojawapo lakini imekuwa kinyume.
JUZI hapa kijiweni wakati tumekaa tukitazama tamasha la Coastal Union, ghafla tukashuhudia utambulisho wa Farid Mussa.
Tulishtuka kwa sababu katika wachezaji ambao hatukutegemea kama wangeichezea Coastal Union kwa msimu ujao, Farid ni mmojawapo lakini imekuwa kinyume.
Baada ya kuitumikia Yanga kwa miaka sita tangu alipojiunga nayo mwaka 2020 akitokea Azam FC, Farid sasa anaenda kujaribu bahati yake ndani ya kikosi cha Coastal Union au Wana Mangushi.
Kijiwe kinaona Farid amefanya uamuzi mzuri na amechagua timu nzuri ya kujiunga nayo kwa faida ya kipaji chake baada ya kukaa muda mrefu bila kupata nafasi ya kutosha ya kucheza mechi za ushindani.
Kostali haina presha na mahitaji makubwa hivyo Farid atacheza bila hofu ya kukosea ambayo pengine ilimfanya ashindwe kuonyesha kiwango kikubwa ambacho kingempa nafasi katika kikosi cha Yanga.
Wakati Farid akitua Kostali, kuna taarifa tumeinasa pia hapa kijiweni Mashujaa FC inakaribia kukamilisha uhamisho wa kiungo wa mpira, Jonas Mkude.
Wengi tunaujua uwezo wa Mkude na kwa kipaji alichonacho, akiwa fiti, kijiwe kinaamini atakuwa ni mchezaji mwenye msaada mkubwa kwa Mashujaa FC katika msimu ujao.
Kijiwe kinatumia fursa hii kuwapongeza wachezaji hao wawili na kuwatakia kila la kheri katika timu zao mpya ambazo watazichezea 2026/2027 na kinaamini watarudi katika makali yao.
Miili yao bado inawaruhusu kucheza soka la ushindani hapa nchini hivyo bado wanahitajika ndani ya uwanja.