Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga ikiboresha haya mbona freshi

KUNA namna ambayo tumekuwa tukiishi na wachezaji (players management) panahitajika kuboreshwa.

Kwa misimu miwili Yanga imekuwa na wachezaji wengi kwenye vitabu vya usajili, lakini wapo walioshindwa kuonyesha ubora na wengine tulishindwa kuonyesha uzoefu na ubora wa kuishi na wachezaji bora.

Ujio wa GSM kupitia udhamini na baadaye kujitoa kwa Hersi Said kumesaidia kuboresha maslahi binafsi ya wachezaji.

Hata hivyo bado kuna maboresho yanahitajika hasa klabu katika kuheshimu na kutimiza matakwa ya kimkataba na kuangalia jinsi ya kuishi na wachezaji maisha ya kikazi, binafsi na kijamii.

Wachezaji wengi wa Kiafrika wanaocheza ligi za nyumbani wana mambo mengi nje ya uwanja na watu wengi waliowazunguka ambao ni virusi au baraka. Hii inategemea namna na jinsi mchezaji ana ufahamu gani.

Kwenye mpira wa kisasa, makocha wa kisasa wanajifunza mafunzo ya usimamizi wa utekelezaji majukumu, hivyo kuwa na uwezo wa kuwasiliana na wachezaji na wataalamu kiufundi katika kutengeneza muunganiko wa timu.

Wachezaji hawapaswi kuzungukwa na watu ambao majukumu yao hayaelezei moja kwa moja. Kwenye kambi ya timu wafuatao ndio wanapaswa kuwa sehemu ya wachezaji - kocha mkuu, kocha msaidizi, meneja wa timu, madaktari (wa kawaida na viungo), wataalamu wa masaji na lishe, mtunza vifaa na mlinzi wa kambi. Watu wengine hususan utawala hawapaswi kuwa na maingiliano ya moja kwa moja na timu.

Posho ni ziada ya mshahara kuleta hamasa kwa wachezaji. Hamasa hii ina pande mbili - moja ni kuwapa wachezaji motisha ya ushindi na pili klabu kufaidika na ushindi.

Mfumo mzuri wa bonasi sharti upendekezwe na kocha na ndiye atangaze kwa wachezaji. Viongozi na wadhamini hawapaswi kuwa sehemu ya majadiliano ya bonusi labda kama itakuwa sehemu ya mtu binafsi na mkataba wa wachezaji jambo ambalo si sahihi.

Yanga inahitaji kocha mwenye uwezo wa juu wa mbinu, lakini pia uelewa wa hali ya juu maana moja ya matatizo makubwa yanayosumbua ni majeraha ya muda mrefu. Upande wa tiba lazima paboreshwe kwa kiwango cha juu a na kuwa na wataalamu wabobevu wa michezo. Pamoja na vifaa tiba vya kisasa, mfano ‘portable ultrasonic machine’ kwa ajili ya tiba za papo kwa hapo.

Kwenye mpira wa kisasa vifaa ni vingi, lakini inategemea na matakwa ya kocha. Hata hivyo kama ni kupata matokeo chanya lazima twende dunia ilipo, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia. Siku hizi kuna programu za kufanya hata mazoezini na kiwango cha uchezaji wa mechi kwa wachezaji.Hapa sasa ni kuwa na kocha aliyezungukwa na watu wanaoweza kumsaidia kufanya hayo.

Kwenye mpira wa kisasa kamati ni wawezeshaji wa yale yanayohitajika kiutawala. Pia kwenye kamati hizo ndipo kuna watu wa kufanya kazi za nje ya uwanja hasa za mipango, siasa, ushawishi na upelelezi. Hawa wanapaswa kuwa watu wenye weledi wa kujua majukumu na mipaka yao.

Kamati ya Ufundi inapaswa kuwa na watu wenye uelewa wa kujua nini kitahitajika kwa makocha na ni namna gani kocha au wachezaji wanaweza kuathiri mwenendo wa timu. Pia watu wenye uwezo wa kuifahamisha klabu bila woga kama tatizo ni la kiutawala zaidi kuliko la kiufundi.

Watu hawa wanapaswa kuwa huru kimawazo na kimaadili. Kumekuwa na kamati nyingi ndani ya Yanga ambazo zipo kisiasa zaidi bila kuwa zimetafsiriwa majukumu yao. Mfano nashindwa kutofautisha kati ya Kamati ya Ufundi na Kamati ya Mashindano kwa kuwa kila mmoja anasema yeye hajahusika kusajili au anatakiwa kuonana na wachezaji ili wamjue na wamsikilize.

Kamati hizi zipo kikatiba sawa kabisa, lakini je zimeainishiwa majukumu yao? Nani afanye nini wakati gani kwa lengo lipi? Unapokuwa na mkurugenzi wa Ufundi halafu una Kamati ya Ufundi na una Kamati ya Mashindano hawa wote wanaonekana kama wanafanya kazi moja.

Ushauri wangu kama una mkurugenzi wa Mashindano kuna sababu gani ya kuwa na kamati hizi za ufundi na mashindano.

Nadhani hizi kamati ziwepo kwa ajili ya siasa za mpira wa Tanzania, lakini ziwe zimetafsiriwa majukumu yake kuondoa mwingiliano na kuja kushindwa kumpima mkurugenzi wa Mashindano na idara yake nzima.

Kwa sasa kumhukumu mkurugenzi wa Mashindano akiwa amezungukwa na utitiri wa kamati ya Utendaji, Mashindano, Ufundi, Wazee, Udhamini na chawa sio sawa.

Kwa Yanga ilivyo inahitaji maboresho kidogo kwenye baadhi ya nafasi, lakini maboresho hayo yafanyike kwa maelekezo ya kocha, ingawa kwa mtazamo wa jicho la tatu inahitaji yafuatayo msimu ujao ambao ni wachezaji wawili - mabeki wa kulia na kushoto, kiungo mkabaji mwenye uwezo wa kupandisha mashambulizi mbele na washambuliaji wawili bora zaidi ya waliopo.

Kuna uwezekano wa Yanga kucheza Ligi ya Mabingwa barani Afrika msimu ujao na kama hilo litatokea maandalizi yaanze hivi sasa. Yanga ina watu wengi ambao majukumu yao hayapo sawa.

Ni wakati sasa wa kuangalia ufanisi wa kila mmoja wetu - iwe kwenye kamati zetu au sekretarieti ama hata wale wengine wanaotokea kwa wafadhili ili kuleta ufanisi na mafanikio. Kama Simba inaweza kucheza robo fainali ya CAF, Yanga inaweza kucheza hata fainali kama tutafanya kazi kwa weledi.


Imeandikwa na Deo Mutta

Mwandishi wa makala haya ni mdau na mpenzi wa michezo nchini.