Prime
MZEE WA FACT: Julio alipoifaidisha Simba akiwa na jezi za wapinzani
Muktasari:
- Julio ambaye hivi karibuni alikuwa kocha wa Mashujaa FC ya Kigoma, alitoa kauli hizo wakati akiongea kama mgeni rasmi kwenye halfa ya ufunguzi wa tawi la mashabiki wa Simba la Mti Pesa jijini Dar es Salaam.
Wiki iliyopita kocha machachari Jamhuri Kihwelo 'Julio' aligonga vichwa vya habari kwa kauli zake tata kuhusu historia yake na klabu ya Simba.
Julio ambaye hivi karibuni alikuwa kocha wa Mashujaa FC ya Kigoma, alitoa kauli hizo wakati akiongea kama mgeni rasmi kwenye halfa ya ufunguzi wa tawi la mashabiki wa Simba la Mti Pesa jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa kauli tata alizotoa ni utumishi wake uliotukuka kama shabiki wa Simba wakati akizitumikia timu zingine kama mchezaji.
Watu wengi wanamfahamu Julio kama mchezaji wa zamani wa Simba, lakini hata hivyo hakucheza sana Simba.
Ushabiki wake kwa Simba ndio umemfanya kunasibishwa zaidi na Simba kuliko uchezaji wake.
Yaani Julio amekuwa mtumishi mwaminifu na wa muda mrefu zaidi kwa Simba akiwa nje ya Simba kuliko akiwa ndani.
Alicheza Simba kuanzia 1990 na 1991 akaondoka...lakini watu wanavyomtaja utadhani alicheza muda mrefu kama akina Jonas Mkude.
Hata hivyo, amekuwa mtumishi mwaminifu kwa Simba akiwa na timu zingine kuanzia wakati anacheza na bila shaka hata akiwa kocha baada ya kustaafu kucheza.
Katika kauli zake tata pale Mti Pesa, Julio alitaja mikasa miwili ya mwanzoni mwa miaka ya 1980 alipoitumikia Simba huku akiwa na jezi za timu nyingine.
Kupitia ukurasa huu najaribu kukuhadhithia kwa kina zaidi mikasa ile.
Ni hivi...
Miaka hiyo, wakati wa mwalimu (baba wa taifa), kulikuwa na timu nyingi sana za mashirika ya umma na taasisi za serikali zilizoshiriki ligi katika misimu tofauti.
Moja ya timu hizo ni Bora Dar es Salaam na CDA Dodoma, ambazo Jamhuri Kihwelo 'Julio' alizihujumu, kwa mujibu wa kauli zake mwenyewe.
BORA SC
Kulikuwa na kampuni ya viatu iliyoitwa Bora (Bora Shoes).
Pale Kijitonyama Dar es Salaam kuna uwanja maarufu unaitwa Bora, sasa pale kulikuwa nyumba za wafanyakazi wa kampuni hii.
Baada kampuni hii kufilisika, zile nyumba zikanunuliwa na idara ya uhamisho.
Hata Morogoro, pale stendi kuu ya zamani katikati ya mji kuna sehemu inaitwa Bora...kulikuwa na duka lao.
Kampuni hii ilianzishwa miaka ya 1950 kupitia uwekezaji wa kampuni ya kimataifa ya Bata eneo la Chang'ombe, Dar es Salaam.
Ilitengeneza viatu maarufu vya shule na kazi, Ilizalisha aina za viatu kama Twiga na Darlon, ikawa na maduka nchi nzima, na kushikilia soko kubwa tangu miaka ya 1970 hadi 1980.
Kiwanda chake kikuu kilikuwa Chang'ombe, Barabara ya Pugu, Dar es Salaam.
Sasa kampuni hii ilikuwa na timu ya mpira ambayo Jamhuri Kihwelo aliichezea mwaka 1982.
Kuanzia mwaka 1978, kulikuwa na mashindano yaliyoitwa Kombe la CCM yaliyoandaliwa na chama cha mapinduzi.
Yalikuwa maarufu sana, kama yalivyo mashindano ya Kombe la Mapinduzi au Kombe la Muungano kwa sasa.
Simba walitwaa Kombe la CCM mara mbili mfululizo, 1981 na 1982.
Huu mwaka 1982 ndio wa Julio akiwa na timu ya bora.
Fainali ilifanyika Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) na baada ya muda mwingi wa sare, Jamhuri Kihwelo akafungisha na kuigharimu Bora FC.
Na Bora wakagundua kwamba aliwachomesha, wakamfukuza.
CDA FC
Mwaka 1974 chama tawala cha TANU kiliazimia kuhamisha makao makuu ya nchi kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Wakati huo kulikuwa na msemo wa chama kushika hatamu, yaani kuwa juu ya serikali.
Hatamu ni kamba ya kuendeshea farasi, kwa hiyo mtu akishika hatamu maana yake anaamua uelekeo wa jambo kama muendesha farasi.
Kwa hiyo TANU ikiwa imeshika hatamu ikaimuru serikali kuhamishia serikali katika makao makuu mapya, Dodoma.
Serikali ikaitikia wito kwa kuunda chombo cha kuuandaa mji wa Dodoma uwe na hadhi ya mji mkuu.
Chombo hicho kikaitwa CDA (Capital Development Authority).
Chombo hicho kikaanzisha timu yake ya mpira iliyoitwa CDA aka watoto wa nyumbani,.na Jamhuri Kihwelo akaichezea timu hii baada ya kufukuzwa Bora FC.
Mwaka 1982 CDA FC iliifunga Simba mabao 6-1 kwenye ligi.
Mwaka 1984 Simba na CDA wakakutana tena kwenye ligi hatua za lala salama huku Simba wakipigania kumaliza katika nafasi ya pili ili washiriki mashindano ya kimataifa.
Mechi ikaisha 1-1 huku Jamhuri Kihwelo akisababisha penalti isiyoeleweka na Simba kusawazisha.
Simba wakamaliza nafasi ya pili kufuzu kushiriki Kombe la Washindi la Afrika.
Wakacheza na Al Ahly ya Misri, mechi iliyofanyika uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.
Simba wakashinda 2-1 kwa mabao ya Mtemi Ramadhani na Zamoyoni Mogella.
Lila Shonary, beki wa kati wa Simba aliumia kwenye mchezo huu na akakosa mchezo wa marudiano jijini Cairo ambapo Simba walifungwa 2-0.