Prime
Wanigeria wanavyoicheza ‘World Cup’ kimya kimya
WAPO Mexico. Wapo Canada. Wapo Marekani. Wapo kimya kimya. Jamaa nawakubali sana. Wanigeria. Wanacheza kombe la dunia kimya kimya ingawa hawakufuzu. Wapo sana. Wana kikosi kikali kuliko vikosi vingi vilivyoshiriki kombe la dunia mwaka huu.
Wenyewe wanaoweza kuimba wimbo wa taifa walishindwa kufuzu kombe la dunia kizembe. Walipigwa kwa penalti na wadogo zake Koffi Olomide. Congo. Lakini kuna Watoto na wajukuu wa Nigeria kibao ambao kama wangeunda timu yao kule Mexico, Canada na Marekani si ajabu wangefika mbali.
Huyu Bukayo Saka basi tu. Anatamba na England lakini alizaliwa na wazazi wa Kinigeria pale London. Hauhitaji kwenda mbali. Jina lake kamili ni Bukayo Ayoyinka Temidayo Moses Saka. Unahitaji nini zaidi ya hilo jina.
Basi tu kwa sababu ni mzuri ndio maana Wazungu wakaamua kuwa naye. Angekuwa mchezaji wa kawaida leo angekuwa katika kikosi cha Nigeria. Hatujui kama angekuwa amewawezesha Wanigeria kufuzu au na yeye angekuwa katika mkumbo wa kina Victor Osimihen.
Pale pale katika kikosi cha England kuna Waingereza wawili katika winga moja. Akitoka Saka anaingia Noni Madueke. Akitoka Madueke anaingia Saka. Wote haw ani Wanigeria. Noni Madueke pia alizaliwa London na wazazi wa Kinigeria.
Jina lake kamili ni Chukwunonso Azuka Tristan Madueke. Wote hawa wawili, Saka na Madueke kumbe wangeweza kuwa wanamsaidia Osimihen kufunga mabao katika kikosi cha Super Eagles. Wapo wengi.
Nusura nimsahau Eberechi Eze. Ni ndugu yao kabisa na jina lake linajieleza. Jina lake kamili ni Eberechi Oluchi Ebere. Kwa kifupi wanamuita Eze. Yeye kama wenzake amezaliwa London. Wanigeria wengi pale Uingereza wamezaliwa London.
Kule uswisi wana beki wao ambaye najua unamjua. Manuel Akanji. Baba yake ni Mnigeria na mama yake ni Mswisi. Unajua jina lake kamili ni nani? Anaitwa Manuel Obafemi Akanji. Basi tu anaungana na akina Granit Xhaka kukichezea kikosi cha Uswisi ambacho kina wachezaji wengi wahamiaji.
Pale pale katika kikosi cha Waswizi Akanji anacheza sambamba na mlinzi mwenzake wa Nigeria, Noah Okafor ambaye ni mchezaji wa Leeds United. Jina lake kamili ni Noah Arinzechukwu Okafor. Huyu ana damu za Afrika tupu kwa sababu mama yake anatoka Afrika Kusini ambako Waafrika sasa wanafukuzwa.
Halafu kuna huyu hapa. Michael Oliseh. Staa mpya katika soka letu. Alianza kama mzaha pale England na akawika na Crystal Palace kuzubaa na akajikuta akiishia Bayern Munich. Sasa hivi mstari wa mbele wa Ufaransa unatisha kwa sababu una Kylian Mbappe, Ousmane Dembele na Oliseh.
Hata hivyo Oliseh ni Wanigeria. Sawa, hawa wengine wawili wana Uafrika mwingi tu lakini Oliseh ana asili ya Nigeria. Baba yake ni Mnigeria aliyezamia Uingereza. Mama yake ana asilia ya Algeria lakini aliyezaliwa Ufaransa.
Ina maana Oliseh angeweza kucheza England, Ufaransa au Nigeria lakini alichagua kucheza Ufaransa. Ni mchezaji pekee wa kikosi cha Ufaransa ambaye anaongea Kifaransa cha kuibiaibia kwa sababu amezaliwa na kukulia London.
Wajerumani wameshatolewa katika kombe la dunia lakini wameondoka na mastaa wawili wa Kinigeri kikosini. Kuna huyu Jamal Musiala. Baba yake ni Mnigeria ambaye alikutana na mama yake Jamal rai awa Ujerumani wakati wakisoma katika chuo kikuu cha Southampton Uingereza.
Unajua jina kamili la Jamal Musiala? Anaitwa Jamal Daniel Richard Afouabi Musiala. Jina tu linakwambia ni raia wa Nigeria. Jamal alizaliwa Stuttgart Ujerumani ingawa pia alikulia Uingereza. Mnigeria mwingine huyu.
Mwingine ambaye wameondoka naye na ameanza katika mechi zote ni Felix Kalu Nmecha anayekipa katika klabu ya Borrusi Dortumund. Huyu mama yake ni Mjerumani. Mdogo wake anachezea Leeds United.
Wamarekani wana staa wao anaitwa Folarin Balogun. Bahati mbaya alipewa kadi nyekundu majuzi dhidi ya Paraguay. Huyu alizaliwa Brooklyin Marekani ingawa alikulia Uingereza. Utotoni alianzia Arsenal na mpaka leo anatamba Ligi kuu ya Ufaransa akiwa na Monaco.
Canada ina Wanigeria wanne. Kuna Samuel Adekugbe ambaye ni mlinzi wa kushoto, kipa Owen Goodman, mshambuliaji, Tani Oluwaseyi na mshambuliaji mwingine, Promise David. Ndugu zetu wa Canada hawajambo linapofika suala la kuhifadhi wakimbizi katika nchi yao. Labda ubaya wauanze sasa hivi.
Wajapana nao wanachekesha kidogo. Kipa wao namba moja, Zion Suzuki baba yake ni Mghana ingawa alizaliwa New Jersey pale Marekani, lakini kipa wao mwingine, Leo Kokuba baba yake ni Mnigeria wakati mama yake ni Mjapan.
Hapo hapo Japan Wanigeria wana damu yao nyingine. Kiungo wa ulinzi, Joel Chima Fujima ambaye anacheza katika ligi kuu ya Ujerumani katika klabu ya St Paul. Wanigeria hawana dogo. Wapo kila mahala. Ni kama maji tu. Kama hauwezi kuoga utayanywa.
Pale Austria kuna wawili na mmoja ndiye ambaye ameipa heshima zaidi Nigeria. David Alaba. Kwanini ameipa heshima? Kwa sababu inatajwa kwamba ndiye mchezaji maarufu zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Austria. Baba yake ni Mnigeria wakati mama yake ni Mfilipino. Lakini pia ndiye alikuwa nahodha wa kikosi cha Austria kilichotolewa juzi na Hispania.
Hapo hapo Austria Alaba anacheza pamoja na ‘ndugu yake’ Carney Chibueze Chukwuemeka. Staa wa Borussia Dortmund ya Ujerumani. Wanigeria wapo wengi. Wapo kila mahala. Hili kombe la dunia wameshiriki sana kimya kimya bila ya watu kuwa na habari.
Hawa ni wanasoka tu. Wapo pia wanamichezo mingine. Ndio hawa akina Anthony Joshua. Lakini wapo pia wanasheria, Madaktari, Waandishi na watu wa fani mbalimbali ambao babu zao walizamia Ulaya na Marekani tangu miaka ya 1930. Hauwezi kuwakosa kila mahala. Wapo kila mahala duniani.