Prime
Wadau wataka mkakati mpya kukomesha vurugu viwanjani – 3
Wadau wa soka Zanzibar wametaka hatua za kukomesha vurugu viwanjani zianze kabla ya mechi, zikihusisha tathmini ya hatari, ukaguzi wa viwanja, ulinzi wa kutosha na elimu kwa mashabiki, badala ya kusubiri matukio yatokee ndipo hatua zichukuliwe.
Wakizungumza kuhusu namna ya kurejesha usalama katika viwanja vya soka, wadau hao wamesema vurugu haziwezi kumalizwa kwa kutegemea polisi au adhabu pekee, bali zinahitaji mfumo unaoweka wajibu kwa waandaaji wa ligi, klabu, mashabiki, waamuzi na mamlaka za michezo.
Akizungumza na Mwananchi, mchezaji wa zamani Zanzibar, Suleiman Haroub Ali, amesema kila mchezo unapaswa kuanza baada ya kufanyika ukaguzi wa kiusalama wa uwanja.
“Huwezi kusubiri vurugu zitokee ndipo uanze kuangalia kama uwanja una usalama wa kutosha. Kabla ya mechi lazima kuwe na ukaguzi wa uzio, milango, njia za kuingia na kutoka na maeneo ambayo wachezaji na waamuzi wanatumia,” amesema.
Amesema endapo uwanja hautakidhi viwango vya msingi vya usalama, mchezo haupaswi kuendelea hadi upungufu uliobainika ushughulikiwe.
MPANGO WA USALAMA
Mdau wa soka, Rashid Juma, anapendekeza kila mchezo uwe na mpango maalumu wa usalama unaobainisha idadi ya walinzi wanaohitajika pamoja na majukumu ya kila upande wakati wa tukio la vurugu.
“Lazima ijulikane kuna walinzi wangapi, polisi wangapi na nani atafanya nini pale tatizo linapotokea. Huwezi kuwa na mashabiki elfu kadhaa halafu usalama ukaachwa kwa watu wachache bila mpango,” amesema.
Kwa mtazamo huo, mpango wa usalama unapaswa kutayarishwa kulingana na ukubwa na aina ya mchezo, badala ya kutumia utaratibu mmoja kwa kila mechi.
Kwa upande wake, Abdulrahman Sadick Mussa, mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya soka, amesema michezo yenye ushindani mkubwa au historia ya vurugu inapaswa kufanyiwa tathmini maalumu kabla ya siku ya mchezo.
“Mamlaka zisiwe zinakwenda uwanjani bila kutathmini hatari iliyopo. Kama kuna mchezo una historia ya ushindani mkubwa, lazima kuwe na kikao cha kiusalama kabla yake. Waandaaji wajue changamoto zinazoweza kutokea na waweke mpango wa kukabiliana nazo kabla hazijatokea,” amesema.
Pendekezo hilo linaweka mkazo kwenye kinga badala ya tiba, kwa kutaka taarifa kuhusu historia ya timu, mashabiki na matukio yaliyopita zitumike kuamua kiwango cha ulinzi kinachohitajika.
MIUNDOMBINU YA USALAMA
Mkongwe wa soka aliyewahi kucheza Kikwajuni FC, Ibrahim Said anasema kutenganisha mashabiki na eneo la kuchezea ni hatua muhimu ya kuzuia uvamizi wa uwanja.
“Mashabiki wanapaswa kuwa na eneo lao na wachezaji wawe na eneo lao. Kama hakuna kitu kinachotenganisha maeneo haya, inakuwa rahisi shabiki mwenye hasira kuingia uwanjani,” amesema.
Amesema miundombinu ya usalama isiangaliwe kama mapambo ya uwanja, bali kama sehemu ya mfumo wa kuzuia vurugu na kuwasaidia walinzi kudhibiti hali pale inapohitajika.
Mbali ya hayo, Kocha wa KVZ, Hababuu Ali amesema ulinzi wa waamuzi unatakiwa kuanzia wanapowasili uwanjani hadi wanapoondoka, kwa kuwa hatari inaweza kujitokeza hata baada ya mchezo kumalizika.
“Mwamuzi anatakiwa kulindwa kuanzia anapofika uwanjani mpaka anaondoka. Kuna wakati mwamuzi anaweza kuwa salama wakati wa mchezo, lakini akatishiwa au kushambuliwa baada ya mechi,” amesema.
Amependekeza kuwe na njia maalumu ya kuwaondoa waamuzi baada ya mchezo na kuhakikisha hawakutani na mashabiki wenye hasira.
KLABU ZIWAJIBIKE
Ni mtazamo wa Saydee Saymir, shabiki wa Muembe Makumbi, kwamba jukumu la kuzuia vurugu haliwezi kuachwa kwa mamlaka za usalama pekee, akitaka klabu ziwajibike zaidi kwa tabia za mashabiki wao.
“Klabu lazima ziache kusema vurugu ni tatizo la mashabiki pekee. Mashabiki ni sehemu ya klabu na klabu zina wajibu wa kuwaelimisha,” amesema.
Amesema kila klabu inapaswa kuwa na utaratibu wa kuwaelimisha mashabiki wake kuhusu mwenendo unaokubalika uwanjani na madhara ya kuvamia uwanja, kumtishia mwamuzi au kushambulia wachezaji.
Katika hilo, Ibrahim Said amesema elimu kwa mashabiki isiwe kampeni inayofanyika baada ya vurugu kutokea, bali iwe sehemu ya maandalizi ya msimu na kila mchezo.
“Hatupaswi kusubiri mashabiki wafanye vurugu ndipo tuwakumbuke. Elimu inapaswa kuanza kabla ya msimu na kuendelea kila mchezo,” amesema.
Amesema mashabiki wanapaswa kufahamu kuwa kushangilia timu yao ni haki yao, lakini kuvamia uwanja, kumtishia mwamuzi au kumpiga mchezaji ni kuvuka mipaka ya ushabiki na kunapaswa kuchukuliwa kama kosa.
ADHABU PEKEE HAITOSHI
Wadau wameeleza pia kuwa kanuni na adhabu ni muhimu, lakini hazitoshi pekee kumaliza vurugu.
Badala ya kusubiri muhusika afanye kosa ndipo hatua zichukuliwe, wamependekeza waandaaji wa ligi wajenge mfumo wa kutambua mapema mashabiki wanaoweza kusababisha vurugu, kuwaondoa katika mazingira hatarishi na kuhakikisha taarifa zao zinawafikia wahusika wanaosimamia usalama.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa wadau, inapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa haki wa kanuni ili adhabu zisichukuliwe kwa upendeleo au kwa kuathiri mashabiki wasiohusika.
Suleiman Haroub Ali, amesema jukumu la usalama lisibebwe na polisi pekee, bali kila anayehusika na mchezo awe na wajibu unaotambulika.
“Usalama si kazi ya polisi pekee na si jambo la kuanza kulizungumzia baada ya mtu kupigwa. Ni sehemu ya mchezo. Kama tunataka soka letu likue na liheshimike, lazima tulinde wachezaji, waamuzi, viongozi na mashabiki kwa wakati mmoja,” amesema.
Mtazamo huo unaungwa mkono na Hababuu Ali, anayesema kuwa sheria, kanuni na vyombo vya ulinzi vilivyopo vinapaswa kufanya kazi kwa pamoja.
“Sheria zipo, kanuni zipo na vyombo vya ulinzi na usalama vipo. Kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake ili kuhakikisha michezo inafanyika kwa amani na utulivu,” amesema.
Vilevile, inapendekezwa kuimarishwa kwa mifumo ya kutatua migogoro ya michezo ili malalamiko kuhusu waamuzi, matokeo au uamuzi wa mashindano usiishie kwenye uwanja wa kuchezea.
Inapendekezwa kuanzishwa Mahakama ya Kitaifa ya Michezo kwa lengo la kuwezesha migogoro kushughulikiwa kwa haraka na kwa utaratibu maalumu badala ya mashabiki kuchukua sheria mkononi.
Kwa upande wa mashabiki, Fahad Mohammed, maarufu Mbaba, amesema mabadiliko hayo yanapaswa kuambatana na mabadiliko ya fikra za mashabiki wenyewe.
“Pale ambapo unahisi mwenzako amekufanyia vitendo ambavyo vinaweza kuzua vurugu kubwa, inabidi ujitafakari kwanza kisha uishi na hivi vitatu ambavyo ni kukubali, kusamehe na kuviacha vipite,” amesema.
Kwa ujumla, ili kukomesha vurugu viwanjani wadau wanasema kunahitaji mfumo wa hatua nyingi ambazo ni pamoja na ukaguzi wa viwanja kabla ya mechi, tathmini ya hatari, mpango maalumu wa usalama, kutenganisha mashabiki na eneo la kuchezea, ulinzi wa waamuzi, elimu ya mashabiki, uwajibikaji wa klabu na utekelezaji thabiti wa kanuni.