Prime
Vurugu zinavyotishia usalama wa soka Zanzibar
Muktasari:
- Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Juni, 2026 umebainika viwanja ambako mara kwa mara matukio hayo hutokea ni Mao A na Mao B, Unguja. Ndani ya mwaka mmoja kumeshuhudiwa matukio kadhaa ya vurugu yaliyoishia kwa baadhi ya wahusika kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
MATUKIO ya vurugu yanayojitokeza mara kwa mara katika viwanja vya mpira Zanzibar, yakiwamo mashabiki kuvamia uwanja, waamuzi kushambuliwa, wachezaji kupigana na mechi kuvunjika, yanaibua wasiwasi kuhusu usalama.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Juni, 2026 umebainika viwanja ambako mara kwa mara matukio hayo hutokea ni Mao A na Mao B, Unguja. Ndani ya mwaka mmoja kumeshuhudiwa matukio kadhaa ya vurugu yaliyoishia kwa baadhi ya wahusika kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Tatizo la miundombinu
Mfululizo huo wa matukio unaibua swali kuhusu mazingira ya viwanja vinavyotumika kwa mashindano.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, baadhi ya viwanja vya Zanzibar vinavyotumika kwa Ligi Kuu, Kombe la FA, Ligi Daraja la Kwanza na mashindano mengine yaliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) na Bodi ya Ligi Zanzibar (ZBL) vina changamoto za miundombinu zinazoweza kuchangia vurugu.
Uwanja wa Mao Zedong (Mao A na Mao B) ni miongoni mwa hivyo.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar (ZBL), Issa Kassim Ali, anakiri kuwepo kwa changamoto hiyo.
“Ni kweli matukio ya mashabiki kuingia uwanjani yamekuwa yakitokea. Changamoto kubwa ipo kwenye baadhi ya viwanja, hususan Mao, ambako wakati mwingine mashabiki hushindwa kudhibiti hisia zao. Hata hivyo, tunawashukuru wengi wao kwa kuwa wamekuwa wakijitahidi kujizuia, ingawa bado yapo matukio yanayotia dosari,” anasema.
Moja ya cha ngamoto kubwa anasema ni kukosekana kwa uzio unaotenganisha mashabiki na eneo la mchezo, hali inayowapa mianya mashabiki wenye jazba kuvamia uwanja na kuwafikia waamuzi na wachezaji.
Vievile, anasema kuna idadi ndogo ya walinzi katika Uwanja wa Mao ambao huwa takribani 15 kwa umati wa mamia ya mashabiki.
Issa anasema kuna mpango wa kuongeza idadi hiyo.
“Mbali na kuboresha kanuni zetu, tunataka pia kuimarisha kitengo cha ulinzi katika michezo yetu. Kwa sasa tunafikiria kuongeza idadi ya walinzi kutoka takribani 15 tulionao hadi kufikia 50, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama,” anasema.
Gharama yawapeleka Mao
Wakati Mao ikiwa na changamoto hizo, timu nyingi bado zinaendelea kuutumia kutokana na gharama zake kuwa ndogo.
New Amaan Complex, ambao umekidhi vigezo vya Shiri kisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hautumiki kwa mechi za Ligi Kuu Zanzibar kutokana na gharama zake kuwa kubwa.
Issa anasema klabu zinaangalia gharama kabla ya kuamua uwanja wa kutumia.
“Gharama za matumizi ya New Amaan Complex hazilingani na Mao, klabu zinaangalia wapi kuna nafuu ndiyo zinakwenda huko,” anasema akieleza kuwa kwa Mao gharama ni Sh200,000 kwa mechi za usiku na Sh150,000 za mchana, huku kwa Amaan usiku ni Sh6 milioni na mchana ni Sh5 milioni.
Mlolongo wa matukio ya vurugu
Aprili 18, 2026, baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Zanzibar kati ya Mlandege na Muembe Makumbi kwenye Uwanja wa Mao A, mshambuliaji wa Muembe Makumbi, Abdallah Iddi Mtumwa ‘Pina’, alionekana akipigana pembezoni mwa uwanja na shabiki wa Mlandege, Fahad Mohammed maarufu kwa jina la Mbaba. Mlandege ilishinda mchezo huo kwa mabao 2-1.
Ka mati ya Uen deshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Zanzibar (ZBL) ilimfungia Pina kucheza mechi tatu mfululizo, huku Mbaba akizuiwa kuhudhuria uwanjani na kutazama mechi zote zitakazoandaliwa na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Akizungumza na Mwananchi wakati wa uchunguzi huu, Mbaba anasema alikubali adhabu licha ya kuwa, kwa mtazamo wake hakuistahili.
“Nilipopata adhabu nilijifunza mambo matatu muhimu; kukubali, kusamehe na kuacha yaliyopita yapite. Naamini mtu akijifunza mambo hayo anaweza kufanikiwa katika maisha,” anasema na kuongeza:
“Nilikubali adhabu hiyo, ingawa kwa mtazamo wangu sikuistahili. Mimi ni shabiki wa mpira na kazi yangu ni kuitangaza timu yangu. Katika tukio lile, mchezaji ndiye aliyenifuata kutoka ndani ya uwanja, lakini pamoja na hayo nimeheshi mu uamuzi wa mamlaka za michezo,” anasema.
Kwa upande wake, Pina anasema: “Siwezi kumzungumzia vibaya Mbaba kwa sababu kwangu ni kama baba. Kilichotokea kilikuwa cha bahati mbaya. Ninaamini alikosea kwa namna yake, lakini bado ninaendelea kumheshimu.”
Shambulio kwa waamuzi
Mbali ya tukio hilo, Ali Mbwana ‘Kihonda’, mwamuzi wa soka Zanzibar amewahi kushambuliwa akiwa katika majukumu yake. Anasema usalama wa waamuzi umekuwa changamoto kutokana na baadhi ya wadau na mashabiki kutaka matokeo kwa nguvu badala ya kufuata sheria za mchezo.
Kihonda anakumbuka tukio ambalo alishambuliwa na mashabiki na habari hiyo kutangazwa katika kipindi cha redio cha Mawio. Kadhia hiyo ilimfika katika mchezo kati ya New King ya Kinyasini na Bweleo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mchangani.
“Marefarii wenzangu walikimbia, mimi nikakamatwa. Nilipigwa sana, mwisho wa siku nikapata nafasi ya kukimbia nikaingia kwenye nyumba ya watu, mama mmoja akanificha uvunguni mwa kitanda,” anasema.
Kwa mujibu wa Kihonda, changamoto hizo hutokana pia na tofauti ya uelewa kati ya waamuzi na mashabiki kuhusu sheria za mchezo.
Siyo Kihonda pekee, Aprili 15, 2026, vurugu nyingine zilitokea katika dakika za nyongeza za mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la FA Unguja kati ya Muembe Makumbi na JKU kwenye Uwanja wa Mao A. Mchezo huo ulivunjika, huku waamuzi wakitolewa uwanjani chini ya ulinzi mkali.
Vurugu hizo zilitokea baada ya wachezaji wa Muembe Makumbi kumvamia mwamuzi msaidizi, Abdallah Kombo, aliyenyanyua kibendera kuashiria kuwa bao lililofungwa na mchezaji wa timu hiyo lilikuwa la kuotea. Tukio hilo lilitokea katika dakika sita za nyongeza, huku JKU ikiwa mbele kwa mabao 2-1. Matukio hayo yanafuata mengine yaliyowahi kutokea katika uwanja huohuo.
Desemba Mosi 2025, katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza kati ya Kundemba na Black Sailors iliyochezwa Uwanja wa Mao A, Unguja, vurugu zilitokea baada ya dakika 90 kukamilika. Black Sailors ilitozwa faini, huku mashabiki wakiadhibiwa pia.
Novemba 14, 2025, Uwanja wa Mao ulirejea katika kumbukumbu za vurugu baada ya mashabiki wa Muembe Makumbi kufanya vurugu katika mechi ya Ligi Kuu Zanzibar dhidi ya KVZ, hali iliyosababisha mchezo kuvunjika kabla ya wakati. Muembe Makumbi ilitozwa faini ya Sh5 milioni na kutakiwa kulipa gharama zote za uharibifu wa miundombinu ya uwanja baada ya kukamilika kwa tathmini.
Miezi kadhaa kabla ya matukio hayo, Mei 12, 2025, Uwanja wa Mao B mjini Unguja ulitumika katika mchezo wa hatua ya mtoano wa kupanda daraja Ligi Kuu Zanzibar kati ya Polisi na Kundemba.
Polisi ilishinda kwa mabao 3-1 na kupanda daraja, lakini baada ya mchezo kulitokea hekaheka nje ya uwanja na kusababisha mwamuzi kutolewa uwanjani akiwa chini ya ulinzi mkali.
Juni 11, 2025, Uwanja wa Mao A uliibuka tena kuwa eneo la vurugu katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA kati ya Uhamiaji FC na KVZ FC. Katika mchezo huo KVZ ilishinda kwa mabao 2-1. Ilidaiwa kuwa kikosi maalumu cha ulinzi cha Valantia Zanzibar kilivamia uwanja na kusababisha vurugu hizo.
Ofisa Ulinzi wa ZFF, Ramadhan Abdalla Bakari, anasema kitendo hicho kilivunja Sheria 38 ya CAF, akieleza hakuna klabu iliyotoa taarifa ya kuhusika na ulinzi na usalama katika mchezo huo.
Pemba mambo tofauti
Wakati changamoto hizo zikiendelea Unguja, Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba umepitia maboresho makubwa yaliyolenga kuboresha usalama na miundombinu.
Kupitia mkataba na mkandarasi Reform Sports kutoka Uturuki, Serikali imefanya ukarabati uliowezesha, miongoni mwa mambo mengine, kujengwa kwa uzio unaozunguka eneo lote la uwanja. Vilevile, umewekwa nyasi bandia, ubao wa kielektroniki na vyumba vya kisasa vya kubadilishia nguo kwa wachezaji na waamuzi, jukwaa la VVIP na la waandishi wa habari, huku paa likiwekwa katika eneo la watazamaji.
Uwanja huo umeendelea kupokea mechi za mashindano ya Ligi Kuu Zanzibar, Kombe la FA Zanzibar, Kombe la Mapinduzi, Kombe la Muungano na Kombe la FA Tanzania Bara.
Itaendelea kesho…