Prime
Sio mbaya Fadlu, Simba wakigawana mbao za mtumbwi
HAKUNA ubaya kama kila mtu akishika hamsini zake. Hakuna ubaya kama Fadlu Davids na klabu ya Simba kila mmoja akatembea katika njia yake. Sijaona kitu kikubwa sana cha kushinikiza uwepo wa uhusiano wao uwe imara zaidi na zaidi.
Nasikia Fadlu anataka kuondoka Simba. Na habari za kuaminika ni kwamba na Simba ipo tayari. Kilichobaki ni kutegeana tu nani aanze kuvunja mkataba kati ya kocha au klabu. Hizi ni habari za kuaminika kutoka katika moja ya vyanzo vyangu.
Chanzo changu kingine kimeniambia kwamba mara baada ya kumalizika kwa pambano la juzi Fadlu amebakia Afrika Kusini na hatakuwa tena kocha wa Simba. Kama atakuja nchini basi ni kwa ajili ya kufunga mizigo yake aliyoiacha katika makabati kisha atarudi tena uwanja wa ndege kwa ajili ya safari ya kwenda anakotakiwa.
Sidhani kama Simba wana kitu kikubwa cha kupoteza katika hili. Kuna kocha huwa anawaweka katika wakati mgumu akiamua kuondoka zake. Kuna aina ya mpira anaweza kuondoka nayo. Hadi sasa hatutajua mpira wa Fadlu ni upi hasa. Kuanzia pale alipoishika timu na mpaka pale alipokwenda likizo kisha akarudi, akahusika katika usajili na kisha kwenda na timu kambini Misri.
Simba iliweka kambi Misri ikacheza na mechi za kirafiki. Iliwakosa wachezaji waliokuwa katika kambi ya Taifa Stars tu ambayo ilikuwa inashiriki Chan. Wakati ikiwa pale Ismailia chini ya Fadlu sidhani kama Simba imetengeneza aina yoyote ya mpira ya kushtua chini ya Fadlu. Siku hizi makocha wanatengeneza falsafa zao.
Unaweza kuchagua kuwa bora katika kushambulia, au kukaa na mpira, au kujihami. Sijaona lolote ambalo Fadlu amelitengeneza kwa ufasaha wakati timu ikiwa kambini kule Misri. Tukianzia na mechi ya Gor Mahia katika siku ya Simba Day. Wageni waliwafundisha wenyeji namna ya kukaa na mpira kwa muda mrefu. Bahati mbaya tu wageni waliruhusu mabao mawili.
Halafu likaja pambano la Simba na Yanga. Simba walionekana kucheza vizuri. Sio kwamba walikuwa wazuri, hapana, ni vile tu Yanga walitarajiwa kuwa wazuri zaidi ya Simba lakini hawakucheza katika kiwango chao. Bado mwisho wa yote Fadlu aliendelea kuweka rekodi ya kupoteza pambano jingine la Dabi dhidi ya mtani kitu ambacho kimekuwa cha kawaida kwake.
Na Jumamosi jioni Simba ilikuwa Gaborone ikicheza pambano la kimataifa la ushindani dhidi ya Gaborone United. Simba haikuonyesha kama ilikuwa kambini Misri ikipika kitu. Ilicheza ovyo ingawa ilishinda 1-0. Sijakutana na shabiki wa Simba aliyeridhika na kiwango cha timu.
Nilijiuliza maswali mawili. Nasikia klabu za Kaizer Chiefs na Raja Casablanca zinamtaka Fadlu. Kwa kiwango kipi ambacho ameonyesha na timu kama hii Simba? Labda alikotoka aliwahi kuwa kocha mzuri lakini kwa kiwango cha Simba hii sijaona hasa ambacho kinazifanya Kaizer na Raja zimfukuzie. Sijaona falsafa ya mpira wake. Sijaona hata wachezaji wakijaribu kutimiza falsafa hiyo uwanjani.
Ni kweli Simba wilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kama ilivyokuwa kwa watani wao lakini tunajua namna mapacha wa Kariakoo wanavyopambana sana nje ya uwanja katika michuano ya kimataifa. Ukipeleka sifa kwa kocha unaweza kujikuta unapotoka. Labda ndio maana makocha wao wakienda timu za nje huwa wanafukuzwa mapema.
Msimu uliopita ilionekana kama vile Fadlu hakuwa na tatizo isipokuwa wachezaji hawakuwa na ubora. Msimu huu mabosi waliongeza wachezaji 15 wapya huku wengine wakionekana kuwa bora na wengine walisajiliwa kwa maombi yake yeye mwenyewe. Hata hivyo, bado timu inacheza katika kiwango cha chini.
Hapo hapo linakuja swali jingine. Fadlu anapata wapi nguvu ya kuiringia Simba? Kuna wakati kocha anaringa baada ya kuwalambisha utamu mashabiki na mabosi wake. Lakini Fadlu atakuwa anaacha alama gani klabuni kama akiamua kufunga mabegi yake leo na kuondoka klabuni? Sishangai kusikia mabosi wa Simba wakiwa tayari kumuacha aondoke zake ili mradi tu yeye ndiye avunje mkataba.
Kama akiondoka sasa Simba watakuwa katika nafasi nzuri ya kuanza na kocha mpya kabla msimu haujachanganya. Labda wachezaji watamuelewa mapema kocha mpya wakati msimu angali ukiwa mchanga. Wakati mwingine inakuwa vigumu kama kocha akija wakati msimu ukiwa umechanganya. Ndio maana hata Fadlu mwenyewe hatukuweza kumchambua vema kuhusu falsafa zake kwa sababu aliwasili nchini wakati msimu ukiwa bado mchanga.
Kichekesho cha msako wa kocha mpya Simba kinakuja pale ninapoambiwa kwamba viongozi wa Simba hawataki kuwafikiria makocha waliopita kwa watani zao, Nasreddine Nabi na Manuel Gamondi. Kisa? Wanahofia hujuma mbele ya safari. Wenzetu huwa hawaangalii mambo hayo wakati wanapoweka majina mezani.
Jose Mourinho amewahi kufundisha Chelsea na Manchester United. Leo Manchester United wakipata nafasi ya kufundishwa na Pep Guardiola watakimbilia haraka kumpa peni na mkataba. Sisi hatujafikia dunia hiyo. Nasikia viongozi hawataki kusikia habari ya Nabi wala Gamondi.
Na sasa nasikia Fadlu anakaribia kuondoka Simba. Kama akiondoka bado timu inaweza kumshukuru kwa kuwaleta wachezaji wawili kutoka Afrika Kusini. Rushine De Rueck anayeonekana kuwa mlinzi mzuri na Simba inaweza kupambana abaki hata kama kaka yake ataamua kuondoka zake Msimbazi.
Halafu kuna Neo Maema. Binafsi bado sijamuelewa sana. Hajanishtua kama ilivyo kwa Rushine. Inawezekana ni mchezaji mzuri kwa sababu wachezaji hawafiki Mamelodi Sundowns kwa bahati mbaya. Lazima wawe na kitu. Labda tofauti na mwenzake kwamba yeye inamchukua muda kuzoeana na wenzake.
Halafu tutamshukuru Fadlu kwa kutuletea Antony Mligo katika timu kubwa. Ni mchezaji mzuri. Kinda mzuri. Imenikumbusha zama za Marcio Maximo wakati alipokuwa kocha wa Taifa Stars. Alikuwa ana uwezo wa kumjua mchezaji mzuri wa timu ndogo kisha akamuingiza katika kikosi chake na kutufanyia 'surprise'.
Wengi hatukumfahamu Mligo. Inawezekana tungemfahamu baadaye. Hata hivyo, shukrani kwa Fadlu ameharakisha tumfahamu na sasa kutakuwa na shinikizo hata kwa makocha wa timu ya taifa kumuita katika kikosi chao akapambane na kina Mohamed Hussein 'Tshabalala' na Pascal Msindo ambao wanachuana katika nafasi hiyo.