Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Karibu Dar Dimitar Pentev, staili ya Chikwende

JICHO Pict


JANUARI 2021 mchezaji anayeitwa Perfect Chikwende alitua zake Msimbazi akitokea klabu ya FC Platnumz ya Zimbabwe. Baada ya mechi mbili tu za hatua ya awali, Simba iliwatosha kushawishika kwamba walikuwa wamepata mchezaji wa maana kwa Chikwende.


Katika mechi mbili za awali za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, aliwasumbua Simba ugenini kule katika ardhi ya Robert Mugabe halafu akawasumbua tena Temeke kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Simba wakaona inatosha kwa walichokiona katika miguu ya Chikwende. Wakainasa saini yake wakati huo huo, ikisemekana kwamba watani wao Yanga na majirani Azam FC pia walikuwa wanamtolea macho Chikwende.


Imejirudia tena juzi Jumamosi. Simba wamemtangaza kocha wa Gaborone United, Dimitar Pentev kuwa kocha wao mpya. Hata hivyo, linatumika jina la "meneja" badala ya "kocha" kwa sababu kuna nyaraka za kumweka katika benchi zimekosekana. Inaonekana kuwa Suleiman Matola ana wasifu wa kuwa kocha mkuu kuliko yeye. Hii ni kwa mujibu wa kanuni zetu.

Imetuachia maswali kidogo. Namna ambavyo ghafla ghafla maisha yanaweza kubadilika katika mpira wetu. Nasikia hata watani wao Yanga waliingilia dili la kumtaka kocha huyu raia wa Bulgaria. Maswali ni mengi. Kwanza kabisa hatuna mipango ya muda mrefu. Ina maana bila ya Simba kucheza na Gaborone United basi leo Pentev asingekuwa kocha wa Wekundu wa Msimbazi.

JICH 01

Ina maana kwamba bila ya Simba kucheza na Gaborone United, basi Yanga nao wasingemuona Pentev. Kwanini hatukumuona huyu kocha kabla ya mechi ya Gaborone United? Hapa ndio tunapogundua kwamba mpira wetu ni bora liende tu. Hatuna mipango ya muda mrefu. Hatuandiki chini kinachopaswa kufanywa kwa msimu mzima. Kitu chochote kinaweza kutokea muda wowote.

Hatuna mpango A wala B. Kila kitu kinaweza kutokea ghafla ghafla tu. Simulizi ya namna ambavyo kuna wachezaji wengi wamesajiliwa na timu hizi kwa sababu waliwahi kuzifunga. Basi. Sio kwamba walimchunguza mchezaji hapo awali, hapana! Ni kwa sababu amewafunga tu, lakini hakukuwa na uchunguzi yakinifu kuhusu mchezaji mwenyewe kabla ya pambano dhidi yake.

Ni hadithi ya Ditram Nchimbi pia. Aliwafunga Yanga mabao matatu na hapo hapo Yanga wakaanza kukimbizana na saini yake bila ya kujali kwamba mchezaji mwenyewe alikuwa hajawahi kufunga mabao zaidi ya kumi katika msimu mmoja. Alipotua Yanga mabosi ndio wakaanza kugundua upungufu mwingi kwake. Kama wangekuwa wamemchunguza awali si ajabu wasingemchukua kwa sababu tu alikuwa amewafunga mabao matatu katika mechi moja.

JICH 02

Kingine katika hili la Pentev inatukumbusha kwamba kumbe pesa sio kila kitu. Hapa nchini kwa sasa klabu zetu zinatia pesa hasa. Kuanzia Simba, Yanga, Azam na ndugu yao Singida United. Hata hivyo, Simba wamehangaishwa vilivyo na Gaborone United ambayo haina uwekezaji mkubwa na wameamua kumchukua kocha wao.

Hii inanikumbusha kitu ambacho kinaendelea katika soka la kisasa. Kitu muhimu zaidi katika mpira kwa sasa ni ufundishaji. Nadhani ufundishaji umekwenda juu ya vipaji. Katika mechi mbili zilizopita Simba walikuwa na wachezaji wa bei mbaya na pengine wachezaji wenye majina makubwa kuliko Gaborone United, lakini walijikuta wakifundishwa mpira na timu ambayo imetengenezwa vema bila ya majina makubwa.

Nilikiona kitu hiki hata katika pambano la Simba Day dhidi ya Gor Mahia. Pale ndipo nilipojua kwamba Simba wasingefika mbali na kocha, Fadlu Davis. Gor Mahia walikuwa vizuri zaidi katika kumiliki mpira, ingawa hawakuwa na wachezaji wa bei mbaya na wala hawakwenda kuweka kambi kwa wiki tatu pale Ismailia na Cairo kule Misri. Hii inatufundisha kwamba mabosi wa hizi timu pia wawekeze zaidi katika suala la benchi la ufundi na sio kukimbizana kuibiana wachezaji.

JICH 03

Na sasa Pentev amepewa jukumu la kuifundisha Simba. Bila ya kujali kwamba amefikaje Simba ukweli ni kwamba anakabiliwa na jukumu kubwa. Jukumu la kuifanya Simba wicheze kama Gaborone United inavyocheza. Tatizo hatutajua atatumia muda gani kuhakikisha hilo linatokea. Tunachojua ni kwamba kutakuwa na presha kubwa ambayo hajaizoea.

Kufundisha Gaborone United ambayo inacheza kwenye uwanja mtupu ni tofauti na kufundisha Simba ambayo ina mashabiki lukuki ndani na nje ya uwanja. Kuanzia kwa makocha hadi wachezaji, kuanzia Ulaya hadi Tanzania, kuna presha kubwa ukitoka katika klabu ndogo kwenda katika klabu kubwa. Maisha hayawi yale yale. Kuna namna tofauti ya kuhimili presha hiyo.

Mifano ni mingi. Hadi sasa tunaendelea kumuona Ruben Amorim akiwa katika hali mbaya pale Manchester United baada ya kutamba vilivyo na Sporting Lisbon. Hata David Moyes alikutana na jinamizi hilo baada ya kutamba vilivyo na Everton, lakini maisha yakawa magumu Manchester United. Mifano hii ipo kwa wachezaji pia. Hatumuombei mabaya Pentev nadhani anaonekana kuwa mwanaume mjuba mwenye uwezo wa kuhimili presha.

JICH 04

Na sasa ametua Simba. Kipi kinatazamiwa? Kwanza ni kuirudisha Simba katika njia yake ya kutawala mechi nyingi ambazo wanacheza. Simba wanaijua timu yao na inachosha kurudia mara kwa mara namna Simba ilivyokuwa katika utawala wa Clatous Chama, Jose Luis Miquissone, Larry Bwalya, John Bocco, Meddie Kagere na wengineo. Mashabiki wa Simba wanaitaka Simba ile.

Na kitu kikubwa wanaamini kwamba msimu huu wamesajili wachezaji wa kuwafanya warudi katika ubora ule. Na ndio maana mashabiki wengi wa Simba hawakusikitika sana wakati Fadlu alipoondoka, kwa sababu licha ya kununua wachezaji mastaa lakini hawakuona Simba ikiwa katika ubora ule licha ya kwamba ilikuwa imetoka kambini Misri.

Pentev ana kazi nzito ya kurudisha imani kwa mashabiki. Akiifanya kazi aliyoifanya na Gaborone United basi atakuwa ameishinda mioyo ya mashabiki wa Simba. Tatizo hatujui atafanya kazi katika mazingira gani ili afikie malengo. Hatujui akiwa na Gaborone United alitumia muda gani kufikia malengo yake. Hatujui alikuwa na uhuru kiasi gani kufikia malengo yake. Hatujui kama atakuwa katika nafasi hiyo hiyo pale Msimbazi.

JICH 05

Kitu kizuri kwa wachezaji ni kwamba wanaanza upya chini ya kocha huyu. Kila mchezaji analazimika kuipigania nafasi yake chini ya Pentev. Nawaona baadhi ya wachezaji ambao wanacheza kwa sababu ya ukubwa wa majina yao. Hata hivyo, viwango vyao vipo chini. Mfano ni Ellie Mpanzu. Kwa muda mrefu sasa yupo chini ya kiwango lakini inachoonekana ni kama vile makocha wanamuogopa.

Kuanzia Fadlu na hadi timu iliposhikwa na Suleiman Matola, Mpanzu ameonekana kuwa 'Mungu mtu' katika kikosi cha Simba. Hawataki kumweka benchi na wanahofia pia kumpiga 'sub'. Nadhani ni kwa sababu ya jina ambalo alilitengeneza msimu uliopita. Mambo kama haya wakati mwingine yanaondoka anapokuja kocha mpya klabuni.

Kila la kheri kwa kocha mpya Msimbazi. Kitu kizuri kwa Simba ni kwamba wamemchukua mapema kabla ya msimu haujachanganya na atakuwa na muda mrefu wa kuwajua wachezaji wake kabla mambo hayajafika mbali.