Vigogo wanaopewa nafasi ya kupenya kwenye kila kundi Afcon 2025
Muktasari:
- Mashindano hayo yanayofahamika kama AFCON 2025 yatafanyika huko Morocco kuanzia Desemba 21 mwaka huu.
RABAT, MOROCCO: WIKI moja tu imebaki kabla ya kuanza kwa mchakamchaka wa mashindano ya soka ya kusaka ubingwa wa Afrika.
Mashindano hayo yanayofahamika kama AFCON 2025 yatafanyika huko Morocco kuanzia Desemba 21 mwaka huu.
Ni mikiki ya mwezi mmoja, ambayo itaanzia kwenye mshikemshike wa mechi za makundi, ambapo timu 24 zilizogawanywa kwenye makundi sita yenye timu nne zitachuana kuusaka ubingwa huo wa Bara la Afrika.
Katika makundi hayo sita (A hadi F) kwa kuzingatia ubora, ukubwa wa vikosi vyao na uzoefu wa mashindano ni timu gani zinazopewa nafasi kubwa ya kutoboa kutoka kwenye makundi yao na kutinga hatua ya mtoano?
Kwa kuzingatia vigezo hivyo, hizi hapa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutoboa kwenye makundi yao katika mashindano ya Afcon 2025. Hata hivyo, hii haina maana kwamba timu nyingine hazina uwezo au haziwezi kutoboa. Soka lina maajabu yake.
Kundi A – Morocco
Kundi hili linaundwa na timu za Morocco, Mali, Zambia na Comoros. Na ni suala lisilohitaji maelezo mengi, wenyeji ndiyo wanaopewa nafasi kubwa ya kupenya na hilo ni kwa sababu lukuki. Kwanza faida ya mashindano kufanyika nyumbani, kisha kwa timu zote zilizopo kwenye kundi hilo, Morocco ndiyo yenye kikosi chenye nguvu ukikitazama kwenye karatasi. Hivyo, kama watacheza kwa ubora wao, wana nafasi kubwa ya kuongoza kundi.
Kundi B – Misri
Misri inapewa nafasi kubwa kwenye kundi lenye timu za Afrika Kusini, Angola na Zimbabwe. Licha ya kwamba matarajio ni kuwapo na ushindani mkali kwenye kundi hilo, Misri inaondwa na kikosi chenye nguvu kubwa na kama kitacheza katika ubora wake, basi ni timu inayopewa nafasi kubwa ya kuongoza kundi. Afrika Kusini nao wanatazamwa kama wakali wengine ambao watasumbua kutoka kwenye kundi hilo, hivyo Misri isipokuwa makini, itakula kwao.
Kundi C – Nigeria
Nigeria inapewa nafasi kubwa ya kupenya kwenye Kundi C mbele ya Tunisia, Uganda na Tanzania. Kikosi hicho cha Super Eagles kina kila sababu ya kumaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi lao kutokana na kuwa na vikosi vyenye ubora mkubwa, benchi bora la ufundi. Kama utatazama wachezaji kwa kuangaliza ubora wa klabu zao wanazotoka, basi Nigeria anapewa nafasi kubwa ya kumaliza namba moja kwenye kundi hilo, huku Tunisia wakitazamwa kama wapinzani wakuu.
Kundi D – Senegal
Senegal inatazamwa kama timu itakayomaliza namba moja kwenye kundi lenye timu za DR Congo, Benin na Botswana. Timu hiyo imetengeneza kikosi matata kinachoundwa na wakali kama Sadio Mane, Nicolas Jackson, Mendy na wengineo, ambapo kama kila mmoja atacheza kwenye ubora wake, basi katika kundi hilo, hakuna timu wa kuizuia Senegal isipenye. Uzuri wa kikosi cha Senegal ni kwamba kimekuwa na uwiano mzuri katika kila idara, huku DR Congo ikitazama kama mshindani.
Kundi E – Algeria
Kama kila kitu kitakwenda kwenye uwiano unaostahili, Algeria inapewa nafasi kubwa ya kuongoza kwenye kundi lao lenye timu za Burkina Faso, Equatorial Guinea na Sudan. Kikosi cha Algeria kimesheheni wachezaji wenye uzoefu na damu changa ambao bila ya shaka watataka kwenda kuonyesha ubora mkubwa katika mchakamchaka huo wa kunyakua ubingwa wa Afrika. Burkina Faso inaweza kuwa mshindani mkubwa wa Algeria katika kundi hilo katika mapambano ya kutinga hatua ya mtoano.
Kundi F – Ivory Coast
Kwenye Kundi F vita itakuwa kali kati ya Ivory Coast na Cameroon, huko Gabon na Msumbiji nazo zikitarajia kuonyesha viwango ambavyo vitakuwa na mshangao kwa mashabiki wengi wa soka wakati wa mashindano hayo ya Afcon 2025. Hata hivyo, Ivory Coast ndiyo timu inayopewa nafasi kubwa ya kumaliza namba moja kwenye kundi hilo na hivyo kutinga hatua ya mtoano. Ivory Coast ndiyo mabingwa watetezi, hivyo bila shaka watapambana ili kuongoza kundi lao.