Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CHRISTOS; Fundi anayepeleka mabao, mipira ya kufa Arsenal

FUNDI Pict

Muktasari:

  • Moja ya maeneo ambayo ilitarajiwa Arsenal ingeimarisha ni nafasi ya winga wa kushoto na, baada ya kuondoka kwa Leandro Trossard kwenda Besiktas ya Uturuki kwa ada ya Pauni 15.3 milioni inaonekana tayari kocha Mikel Arteta amempata mbadala wake; Christos Tzolis.

BRUSSEL, UBELGIJI: HUENDA Arsenal ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20 msimu uliopita, lakini bado iliingia katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi ikiwa na kazi kubwa ya kufanya.

Moja ya maeneo ambayo ilitarajiwa Arsenal ingeimarisha ni nafasi ya winga wa kushoto na, baada ya kuondoka kwa Leandro Trossard kwenda Besiktas ya Uturuki kwa ada ya Pauni 15.3 milioni inaonekana tayari kocha Mikel Arteta amempata mbadala wake; Christos Tzolis.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ugiriki ameshaondoka Club Brugge kutua London kwa Pauni 34 milioni ambayo ni ada ya rekodi katika historia ya Ligi Kuu ya Ubelgiji. Tzolis ametumia misimu miwili akiwa na jezi ya Club Brugge, ambako alijiimarisha kama mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kuzalisha mabao na kusaidia timu kupata matokeo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alifunga mabao 33 kwa klabu hiyo tangu alipowasili akitokea Norwich City 2024, lakini ni msimu wa 2025-26 ambao huenda ulimvutia zaidi Arteta na viongozi wa Arsenal.

FUND 03

Msimu wake bora wa ndani ambao alifunga mabao 17 na kutoa asisti 23 katika mechi 36, uliisaidia Club Brugge kutwaa ubingwa wa 20 wa Ligi Kuu Ubelgiji. Jumla hiyo ya michango ya mabao 40 ilikuwa juu kwa tofauti ya mabao 16 dhidi ya mchezaji mwingine yeyote katika ligi hiyo, huku mshirika wake Nicolo Tresoldi akiwa nafasi ya pili kwa mchango wa mabao 24 msimu mzima.

Kama ilivyokuwa kwa Trossard, Tzolis anatumia zaidi mguu wake wa kulia na hucheza zaidi upande wa kushoto, lakini pia anaweza kutumika katikati kama mshambuliaji au kiungo mshambuliaji. Pia amewahi kucheza upande wa kulia akiwa Club Brugge, jambo linaloonyesha uwezo wake wa kubadilika sifa ambayo wachezaji wengi waliosajiliwa na Arteta wamekuwa nayo.

Takwimu za Tzolis katika msimu wa 2025-26 zilikuwa za kuvutia sana, lakini ni muhimu kukumbuka kwamba ushindani katika Ligi Kuu Ubelgiji ni wa kiwango cha chini ukilinganisha na Ligi Kuu England.

FUND 02

Kwa mujibu wa viwango vya sasa vya Opta Power Rankings, Ligi Kuu Ubelgiji ni ya nane kwa ugumu duniani ikiwa na wastani wa alama 81.8 kwa kila timu. Iko chini kidogo ya Championship ya England, ambayo ipo nafasi ya saba ikiwa na wastani wa alama 82.2.

Kwa kulinganisha, wastani wa alama 91.7 wa Ligi Kuu England unaifanya kuwa ligi bora zaidi duniani kwa viwango hivyo, ikiwa mbele ya Serie A ya Italia yenye wastani wa 86.2. Hii ina maana Tzolis atalazimika kufanya marekebisho makubwa kwa haraka kwani mashabiki wa soka England  wanaojulikana kwa kutokuwa na subira sana.

Hata hivyo, takwimu zake nchini Ubelgiji msimu uliopita haziwezi kupuuzwa. Alipolinganishwa na wachezaji wengine 12 waliomaliza msimu wakiwa na mabao 10 au zaidi katika ligi hiyo, Tzolis aliongoza pia katika vipengele vingine muhimu kama kutengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga (135), chenga nyingi zaidi kila mechi (40), na alifanya mikimbio mingi zaidi yenye kusogeza timu mbele akiwa na mpira (359) kwa tofauti kubwa. Thorgan Hazard alikuwa wa pili akiwa na mikimbio 215.

FUND 05

MIPIRA YA KUFA

Ufanisi wa Arsenal katika mipira ya kona umekuwa mjadala mkubwa katika misimu kadhaa iliyopita, lakini ni wazi kuwa klabu hiyo inalipa umuhimu mkubwa eneo hilo na imeanza kuvuna matunda.

Walifunga mabao 19 kupitia mipira ya kona katika Ligi Kuu England 2025-26, rekodi mpya ya timu yoyote katika msimu mmoja wa mashindano hayo. Cha kuvutia ni kwamba hilo pia ni eneo ambalo Tzolis ana uwezo mkubwa, jambo ambalo bila shaka litamvutia Arteta.

Kati ya nafasi 135 alizotengeneza akiwa Club Brugge katika ligi msimu uliopita, nafasi 52 zilitokana na mipira ya kutenga (asilimia 38.5).

Kwa kulinganisha na wataalamu wa mipira iliyokufa wa Arsenal, asilimia 42.9 ya nafasi zilizotengenezwa na Declan Rice zilitokana na mipira hiyo wakati Bukayo Saka alikuwa na asilimia 19.7. Kutokana na Rice na Saka kuingia msimu wa 2026-27 wakiwa na changamoto za utimamu wa miili, Tzolis anaweza kuwa mtu muhimu kuchukua jukumu la kupiga mipira ya adhabu na kona wakati Arsenal itakapoanza kutetea taji.

FUND 04

VITA ULAYA

Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Tzolis alionyesha kwamba uwezo wake hauishii kwenye Ligi Kuu Ubelgiji pekee, bali anaweza pia kucheza kwa kiwango cha juu dhidi ya klabu bora zaidi Ulaya. Akilinganishwa na Trossard katika Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, inaonekana wazi kuwa Tzolis ni mbadala mwenye akili kwa Arsenal na anaweza kuingia kikosini na kutoa mchango wa haraka.

Kwa upande wa mchango wa mabao, Trossard alihusika kwenye mabao matano (bao 1 na asisti 4), wakati Tzolis alikuwa na mabao matatu (mabao 2 na asisti 1). Lakini katika vipengele vingine vya mchezo, Tzolis alionyesha uwezo mkubwa, ambapo mshambuliaji huyo alikamilisha mikimbio 59 ya kushambulia akiwa na mpira, 15 zaidi ya Trossard aliyekuwa na 44. Pia alifanikiwa kupiga pasi nyingi zaidi kwenda eneo la mwisho la mashambulizi (26 dhidi ya 16).

Zaidi ya hapo, licha ya kuwa na pasi moja tu ya mwisho ukilinganisha na nne za Trossard, Tzolis (13) alitengeneza karibu mara mbili ya nafasi ambazo Trossard alitengeneza (7). Inaweza pia kudaiwa kwamba kama angekuwa anacheza katika timu kubwa zaidi kama Arsenal, kiwango chake cha uzalishaji kingekuwa kikubwa zaidi.

Wachezaji hao wawili wana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi na kuchangia mabao, lakini kwa mtindo wa uchezaji Tzolis ataleta kitu tofauti zaidi upande wa kushoto wa Arsenal.

Yeye ni mchezaji anayependa kutembea na mpira, kuwafikia mabeki moja kwa moja na kutumia uwezo wake wa mmoja dhidi ya mmoja kutengeneza nafasi, wakati Trossard mara nyingi hupendelea kupunguza kasi ya mchezo na kutumia akili zaidi kutafuta nafasi.

Pia, ukweli kwamba Tzolis ni mdogo kwa miaka saba kuliko Trossard na bado ana nafasi ya kukua na kuendelezwa chini ya Arteta ni jambo ambalo litaongeza nguvu katika kikosi cha Arsenal.

FUND 01

Baada ya kujiunga na Arsenal Januari 2023, Trossard aligeuka kuwa mchezaji anayependwa sana na mashabiki, na huenda hata akawa mmoja wa wachezaji watakaokumbukwa katika historia ya klabu hiyo baada ya kufunga bao lililowapa ubingwa dhidi ya West Ham United.

Atakumbukwa kwa uwezo wake wa kutengeneza matukio makubwa katika mechi kubwa. Hivyo, itakuwa matarajio makubwa kumtegemea Tzolis aje mara moja na kutoa kiwango hicho hicho cha mafanikio katika mechi kubwa tangu siku ya kwanza.

Iwapo usajili huo utakamilika, huenda ikawa ndiyo nyongeza pekee ya Arsenal katika safu ya ushambuliaji, huku taarifa zikidai klabu hiyo bado itafanya pia usajili mkubwa wa nyota wa juu ili kuongeza nguvu zaidi kwenye safu hiyo.

Kuwasili kwa Tzolis huenda siyo aina ya usajili mkubwa wenye jina kubwa ambao baadhi ya mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakitamani, lakini unaweza kuwa usajili wa akili na wenye faida kubwa kwa klabu hiyo.