Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VICENT: Mkali wa asisti Championship anayelizwa na jeraha lililomtibulia

Muktasari:

  • Geita Gold inaongoza msimamo wa Championship ikivuna alama 36 katika mechi 13, imeshinda 11 na sare tatu ikiwa haijapoteza mchezo. Imefunga mabao 27 na kuruhusu sita.

SAFARI ya Geita Gold kupanda Ligi Kuu msimu huu imekolea na gari lao limeshika kasi, lakini miongoni mwa wachezaji muhimu katika matokeo mazuri inayoendelea kuyapata timu hiyo ni Vicent Abubakar.

Geita Gold inaongoza msimamo wa Championship ikivuna alama 36 katika mechi 13, imeshinda 11 na sare tatu ikiwa haijapoteza mchezo. Imefunga mabao 27 na kuruhusu sita.

Katika takwimu hizo, Vicent amechangia mabao saba, akitoa pasi za mabao (assists) tano na kufunga mabao mawili.

Mabao yote mawili aliyafunga Novemba 26, 2025 katika ushindi wa 3-0 mbele ya Hausung FC katika Uwanja wa Amani mkoani Njombe.

Vicent anayemudu kucheza winga ya kulia na kushoto pamoja na mshambuliaji wa kati, amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Geita Gold akiaminiwa na Kocha Zuberi Katwila, akicheza mechi 13 kati ya 14 za ligi.

Mwanaspoti limepiga stori na winga huyo kuhusu kiwango chake, malengo, Geita Gold na simulizi ya safari yake kwenye soka ikiwemo ndoto ya kutamani kuwa mwanajeshi.

Akizungumzia kiwango, Vincent anasema kinachangiwa na kujituma na kufuata maelekezo anayopewa na benchi la ufundi kwenye uwanja wa mazoezi na kabla ya mechi.

“Kinachonifanya niwe vizuri mpaka sasa nafikiri ni kujituma sana, kujitunza tu na umakini ambao napewa na walimu kwa hiyo hicho kinanifanya niwe bora,” anasema.


LIGI NI TAMU

Winga huyo ana-amini Ligi ya Championship ina ushindani ambao timu zinapaswa kujidhatiti ili kufikia malengo, jambo ambalo linadhihirishwa na alama chache zinazotofautiana timu hizo kwenye msimamo.

“Ligi ni nzuri ina ushindani mzuri kulingana na pointi tunazotofautiana hazipishani sana kila mtu anapambana ili kujiweka vizuri katika msimamo,” anasema Vincent.


VITA YA GEITA GOLD,  KAGERA SUGAR

Kwenye mmsimamo wa Ligi ya Championship, Geita Gold na Kagera Sugar zina vita nzito zikikimbizana juu kwenye msimamo wa ligi, ambapo katika mechi nne zinalingana kila kitu.

Timu hizo zimecheza mechi 14 zikishinda 11, sare tatu na hazijapoteza mchezo, zimefunga mabao 27 na kuruhusu sita, huku zikivuna alama 36.

Akizungumzia ush-indani huo, Vincent anasema wanapaswa kucheza na kushinda mechi zao bila kumuangalia mpinzani wao anafanya nini, ili mwisho wa msimu matokeo yaamue nani anapanda daraja.

“Ushindani ni mkubwa, sisi kama wachezaji huwa tunahakikisha tunazicheza mechi zetu hatumuangalii mtu amefanya nini. Tunahakikisha tunapambana kupata matokeo katika mechi zetu na siyo Kagera tu, timu nyingi tunakaribiana pointi,” anasema Vincent.


MAJERAHA YATIBUA

Kabla ya kujiunga na Geita Gold msimu uliopita, winga huyo alikiwasha Ligi Kuu Bara akiwa na Coastal Union na baadaye KMC, lakini majeraha aliyopata mazoezini yalisababisha akose nafasi ndipo akatimikia Championship kujitafuta.

Akisimulia tukio hilo, Vincent anasema ilikuwa mwaka 2023 aliposajiliwa na KMC akitokea Coastal Union, ambapo timu hiyo ikiwa imeweka kambi Zanzibar alivunjika mguu na kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi 12.

“Kwenye pre- season (maandalizi ya msimu) pale Zanzibar mazoezini tu siku ya nne nikavunjika mguu nimekaa kama mwaka na nusu. Nilipopona nilicheza mechi chache tu mkataba ulivyoisha nikaja zangu Geita,” anasema.

Anasema kwamba majeraha hayo yalimharibia mipango yake kwa kiasi kikubwa na kusababisha akose namba katika kikosi cha kwanza, jambo lililosababisha akimbilie Championship.

“Niliporudi kupambania nafasi yangu ilikua ngumu kuniamini tena kwa sababu nilikua nimetoka kwenye majeraha, sikupata muda wa kucheza kama unavyojua mpira wetu wa bongo usipocheza muda mrefu watu wanakusahau,” anasema winga huyo.



ANGEKUWA MWANAJESHI

Vicent ambaye ni mzaliwa wa Uyui mkoani Tabora anasema kama isingekuwa soka ndoto zake zilikuwa uanajeshi kwani ni kazi anayoipenda mpaka leo.

“Nje ya mpira mimi nilikuwa natamani sana kuwa mwanajeshi ila ilishindikana, lakini ni kazi ninayoipenda,” anasema.

ALIKOANZIA

Vincent ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Igalula wilayani Uyui, Tabora, ni mtoto wa pili katika familia ya watoto wanne, wakiwemo wawili wa kike na wawili wa kiume, ambapo, safari yake ya soka ilianzia shuleni kwenye mashindano ya kusaka vipaji ya Copa Coca cola kuanzia ngazi ya mkoa mpaka taifa.

“Baada ya kucheza ngazi ya taifa jijini Dar es Salaam nilijiunga na Kiluvya United, nikacheza Majimaji ya Songea baadaye nikaenda DTB (kwa sasa ni Singida Black Stars),” anasema Vincent.

Anaongeza: “Baadaye nikacheza Ligi Kuu na Coastal Union kisha nikaenda KMC na sasahivi niko Geita Gold. Familia yetu ni watu wa mpira, babu zangu walicheza mpira lakini siyo ngazi ya juu ila walikuwa ni watu wa mpira.”


CHRISTIANO RONALDO

Anasema wakati anaanza kucheza soka alikuwa anamtazama na kuvutiwa zaidi na nyota wa Manchester United, Real Madrid, Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno, Christiano Ronaldo ambaye pia anacheza nafasi ya winga na mshambuliaji wa kati.

“Mimi nampenda sana Christiano Ronaldo mpaka leo kwa sababu ya ile mikimbio yake na spirit (roho) yake uwanjani, ni mpambanaji sana asiyekata tama,” anasema Vincent.


AWATAJA SOPU, MTENJE ALBANO

Nyota huyo anasema katika soka la Tanzania anawakubali wachezaji wengi kutokana na uwezo wao, lakini miongoni mwao anawataja Miraji Abdallah, Abdul Suleman ‘Sopu’, na Mtenje Albano.

“Nawa-kubali wengi siwezi waorodhesha wote ni kwa sababu wana vipaji vikubwa ambavyo Mungu amewapa, lakini watano naoweza kuwataja ni Miraji Abdallah, Abdul Suleiman (Sopu), Gustapha Simon, Mtenje Albano, na Jackson Suluja,” anasema Vincent.

NENO KWA MASHABIKI

“Wasapoti tu vitu vya kwao, mashabiki wa Geita tunawapenda tunapambana tuwapandishie timu yao wawe na furaha kama zamani, Inshallah,” anasema.


MSIKIE KOCHA

Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zuberi Katwila anasema kikosi chake kina wachezaji waliokomaa, wenye uzoefu na wanaofuata maelekezo na kutekeleza vyema kazi anayowapa akiwemo Vicent  ambaye amekuwa mchezaji muhimu kwenye timu.

Katwila alimpongeza winga huyo kwa kazi nzuri anayoifanya, akitumia uzoefu alionao kuisaidia Geita Gold kutimiza malengo yake ya msimu huu kupanda Ligi Kuu Bara.

“Tumekuwa na michezo migumu lakini wachezaji wangu wanapambana na tunapata matokeo, ni ushindani tunaoutarajia kutoka kwa wapinzani lakini nina wachezaji waliokamaa kama huyu Vicent (Abubakar) wanatusaidia,” anasema Katwila.

Anaongeza: “Pia nimewaandaa kisaikolojia kwahiyo wanafanya vitu vya msingi, lakini hawapaswi kubweteka kwani safari bado inaendelea tunatakiwa kuendelea kushinda michezo yetu.”