Arsenal yapewa Madrid, Bayern, PSG kuzifuata Man City, Aston Villa
Muktasari:
- Mabingwa wa Ligi Kuu England, Arsenal, ambao msimu uliopita walipoteza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya Paris Saint-Germain, pia watasafiri kwenda kucheza na Bayern Munich, wataikaribisha Borussia Dortmund na kusafiri kwenda Napoli katika kampeni yao.
BAADA ya kuchezeshwa kwa droo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2026-2027, Arsenal itakuwa mwenyeji wa Real Madrid, Aston Villa itacheza dhidi ya mabingwa watetezi Paris Saint-Germain, huku Manchester United ikirejea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kukutana na Bayern Munich.
Mabingwa wa Ligi Kuu England, Arsenal, ambao msimu uliopita walipoteza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya Paris Saint-Germain, pia watasafiri kwenda kucheza na Bayern Munich, wataikaribisha Borussia Dortmund na kusafiri kwenda Napoli katika kampeni yao.
The Gunners pia watacheza dhidi ya Real Betis, Lille, Sabah ya Azerbaijan ambayo itakuwa ikicheza Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza, pamoja na Slavia Prague.
Manchester United ya kocha Michael Carrick, katika kampeni yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa baada ya kupita miaka mitatu, itaikaribisha Bayern Munich na kusafiri kwenda kukutana na Atletico Madrid katika michezo yake minane ya hatua ya ligi. Pia itakutana na Roma, Sporting, RB Leipzig, Villarreal, Sabah na Como.
Liverpool kwa mara nyingine itasafiri kwenda Inter Milan na kuikaribisha Atletico Madrid, michezo miwili ambayo inarudia ratiba ya msimu uliopita, huku pia ikicheza dhidi ya Porto, Villarreal na kusafiri kwenda Uturuki kukutana na Fenerbahce. Timu hiyo ya Andoni Iraola pia itacheza dhidi ya Club Brugge, Lens na mabingwa wa Austria, LASK.
Manchester City itacheza dhidi ya mabingwa watetezi PSG na Barcelona katika kampeni ngumu ya kwanza kwa kocha Enzo Maresca, huku pia ikikutana tena na Kevin De Bruyne baada ya kupangiwa kucheza na Napoli nyumbani. Sporting, Porto, Leipzig, AEK Athens na Lens zitakamilisha ratiba yake.
Aston Villa, mabingwa wa Europa League, watasafiri kuifuata Barcelona, huku pia ikiwa mwenyeji wa mabingwa watetezi PSG katika marudiano ya pambano lao kali la robo fainali lililochezwa miaka miwili iliyopita. Borussia Dortmund, Club Brugge, Fenerbahce na Galatasaray, pamoja na Viking ya Norway na Slavia Prague, ndizo timu zitakazokutana na vijana hao wa Unai Emery.
Ratiba hiyo inaifanya bingwa mtetezi, PSG kuwa na safari mbili nchini England kukabiliana na Manchester City na Aston Villa, pia itaikaribisha Barcelona huko Parc des Princes.
Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu itachezwa kwenye Uwanja wa Estadio Metropolitano, ambao ni nyumbani kwa Atletico Madrid.
Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 70,000, ulipewa heshima ya kuandaa fainali hiyo mwaka 2025 baada ya Uwanja wa San Siro uliopo nchini Italia kuondolewa kwenye nafasi hiyo.
UEFA iliamua kufungua tena mchakato wa kuwania uenyeji wa fainali hiyo kutokana na wasiwasi kuhusu mipango ya ukarabati wa San Siro, hivyo mchezo huo sasa utafanyika katika mji mkuu wa Hispania, Madrid.
Mara ya mwisho uwanja huo uliandaa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa Juni 1, 2019, wakati Liverpool ilipoifunga Tottenham mabao 2-0.
MICHUANO ITAKAVYOKUWA
Katika mfumo huu mpya wa ligi, timu zote 36 zipo kwenye msimamo mmoja badala ya makundi ya zamani. Kila timu itacheza michezo minane.
Baada ya michezo hiyo, timu nane za juu zitaingia moja kwa moja hatua ya 16 bora, wakati zitakazomaliza nafasi ya tisa hadi 24 zitacheza mchujo wa kuwania nafasi zilizobaki. Timu zitakazomaliza nafasi ya 25 hadi 36 zitaaga mashindano ya Ulaya.
Michezo ya hatua ya ligi itaanza Septemba 8 hadi 10, 2026, huku raundi ya mwisho ikichezwa Januari 27, 2027. Fainali imepangwa kufanyika Juni 5, 2027, mjini Madrid.
Hata hivyo, UEFA imesema mpangilio kamili wa kila mchezo pamoja na tarehe na saa za kuanza utatolewa kabla ya Agosti 29, 2026.
TIMU ZA ENGLAND
Msimu uliopita, Arsenal waliopoteza fainali, waliongoza msimamo wa raundi ya ligi kwa pointi 24 baada ya kushinda mechi zote nane, huku Liverpool wakiwa wa tatu nyuma ya Bayern Munich walioshika nafasi ya pili kwa pointi 18, wakati Tottenham wakimaliza nafasi ya nne.
Chelsea na Manchester City pia walifuzu moja kwa moja kwa raundi ya 16 baada ya kumaliza katika nafasi ya sita na ya nane mtawalia huku Newcastle wakimaliza katika nafasi ya 12.
Chelsea, Manchester City, Newcastle na Spurs walitolewa katika raundi ya 16 msimu uliopita huku Liverpool wakishindwa katika robo fainali na PSG, ambao pia waliishinda Arsenal katika fainali na kubeba taji lao la pili mfululizo.
Safari hii hatua ya ligi, Liverpool itacheza dhidi ya Atletico Madrid (nyumbani), Inter Milan (ugenini), Porto (nyumbani), Club Brugge (ugenini), Villarreal (nyumbani), Fenerbahce (ugenini), Lens (nyumbani), LASK (ugenini).
Nayo Aston Villa itacheza dhidi ya PSG (nyumbani), Barcelona (ugenini), Borussia Dortmund (nyumbani), Club Brugge (ugenini), Fenerbahce (nyumbani), Galatasaray (ugenini), Viking (nyumbani), Slavia Prague (ugenini).
Huku Manchester City itacheza dhidi ya PSG (nyumbani), Barcelona (ugenini), Sporting Club (nyumbani), Porto (ugenini), Napoli (nyumbani), Leipzig (ugenini), AEK Athens (nyumbani), Lens (ugenini).
Kwa upande Manchester United itacheza dhidi ya Bayern Munich (nyumbani), Atletico Madrid (ugenini), Roma (nyumbani), Sporting Club (ugenini), Leipzig (nyumbani), Villarreal (ugenini), Sabah (nyumbani), Como (ugenini).
Pia Arsenal itacheza dhidi ya Real Madrid (nyumbani), Bayern Munich (ugenini), Borussia Dortmund (nyumbani), Real Betis (ugenini), Lille (nyumbani), Napoli (ugenini), Sabah (nyumbani), Slavia Prague (ugenini).
HATUA HII ITACHEZWA TAREHE HIZI
Mchezo wa kwanza: Septemba 8–10, 2026
Mchezo wa pili: Oktoba 13–14, 2026
Mchezo wa tatu: Oktoba 20–21, 2026
Mchezo wa nne: Novemba 3–4, 2026
Mchezo wa tano: Novemba 24–25, 2026
Mchezo wa sita: Desemba 8–9, 2026
Mchezo wa saba: Januari 19–20, 2027
Mchezo wa nane: Januari 27, 2027