Ukisikia wanacheza kamata rimoti yako
Muktasari:
- Kukiwa na takribani siku sita kabla ya Kombe la Dunia kuanza mjini Mexico City, ni wakati wa kuuliza, ni kina nani utafurahia kuwaona wakicheza.
WASHINGTON, MAREKANI: Kombe la Dunia la FIFA 2026 litakuwa na timu 48 na zaidi ya wachezaji 1,200. Ni kina nani wachezaji unaopaswa kuwaangalia katika Kombe la Dunia 2026? Hawa hapa mastaa 15 ambao unasubiri kuwaona wakicheza.
Kukiwa na takribani siku sita kabla ya Kombe la Dunia kuanza mjini Mexico City, ni wakati wa kuuliza, ni kina nani utafurahia kuwaona wakicheza.
Mashindano hayo yamepanuliwa kuwa na timu 48 kwa mara ya kwanza, na kwa wachezaji 26 katika kila kikosi, jumla ya wachezaji 1,248 wanakwenda Marekani, Mexico na Canada. Hao ni wengi mno kwa mtu yeyote kuelewa kwa urahisi, lakini hapo ndipo unapopaswa kusaidiwa kuwajua wachache utakaowafurahia uwanjani.
Kwa msaada wa wataalamu wa data na wachambuzi wa soka kutoka sehemu mbalimbali duniani ndani ya safu ya Opta wamechagulia idadi inayoweza kudhibitiwa ya wachezaji wa kuwaangalia. Hii siyo orodha ya wachezaji 26 bora wanaokwenda Kombe la Dunia, wala si orodha ya wachezaji ambao hujawahi kuwasikia. Kigezo pekee kilichotumiwa ni kwamba unapaswa kuwa na hamu ya kuwaona wakicheza.
Elliot Anderson (England)
England imejaa wachezaji wanaocheza katika klabu za Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini Elliot Anderson Anderson alikuwa na msimu mzuri katika kiungo cha Nottingham Forest akianzia mechi 37 kati ya 38 za Ligi Kuu England, huku akitokea benchi kipindi cha mapumziko katika mchezo mmoja.
Ni wachezaji watano pekee waliocheza dakika nyingi zaidi katika ligi hiyo msimu huu kuliko Anderson (3,334). Jamaa pia anakimbia balaa huku akiwa na mpira kwani ni James Garner pekee (kilomita 415.4) aliyekimbia zaidi yake huku yeye akifanya hivyo kwa kutimka kilomita 411.0. Anderson pia alishinda umiliki wa mpira mara 94 zaidi (306) kuliko mtu mwingine yeyote. Pia aliongoza ligi kwa kipimo cha kila dakika 90 katika kushinda mpira (8.3).
Donyell Malen (Uholanzi)
Donyell Malen tangu mechi yake ya kwanza AS Roma Januari 18, mwaka huu kafunga mabao mengi zaidi (14) katika ligi tano bora za Ulaya akizidiwa tu Harry Kane (16).
Malen alikuwa mchezaji wa tatu kufunga angalau mabao 14 Serie A akicheza chini ya mechi 20 katika msimu mmoja, baada ya Zlatan Ibrahimovic (15 katika mechi 19 msimu 2020-21) na Ronaldo de Lima (14 katika mechi 19 msimu wa 1998-99). Jumla yake ya mabao pia ilikuwa juu kuliko mchezaji yeyote aliyeingia Januari katika ligi ya Italia karne hii (rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Mario Balotelli, mabao 12 msimu 2012-13).
Callum McCowatt (New Zealand)
Chris Wood ndiye jina linalojulikana zaidi inapokuja timu ya taifa ya New Zealand akichezea klabu ya Superliga ya Silkeborg, Denmark.
McCowatt amekamilisha msimu wa sita Denmark tangu 2020, lakini msimu huu ulikuwa bora zaidi kwake akifunga mara 11 na asisti tano kuliko alivyowahi kufanya katika misimu yake miwili ya kwanza ya Superliga akiwa Silkeborg kwa pamoja (mabao 10, asisti nne).
Sehemu kubwa ya hatari yake hutokea anapokimbia na mpira, huku wachezaji watatu pekee wa Superliga msimu 2025-26 wakiwa na mchango zaidi wa mashuti baada ya kubeba mpira angalau mita tano kuliko McCowatt (41 - mashuti 29, nafasi 12).
Lamine Yamal (Hispania)
Lamine Yamal alikuwa mchezaji mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika La Liga msimu huu; hakuna mwingine aliyefikia tarakimu mbili katika mabao 16 na asisti 11 katika ligi hiyo. Kwa kufanya hivyo, alikuwa mchezaji wa kwanza chini ya umri wa miaka 20 kufanya hivyo katika karne ya 21. Anajulikana kwa chenga na ubunifu. Ni VinÃcius Junior pekee aliyengeneza nafasi na mashuti zaidi yake (92 - mashuti 49 na nafasi 43) baada ya chenga kuliko Yamal (86, mashuti 50 na nafasi 36) katika ligi tano bora za Ulaya. Pia alikamilisha chenga nyingi zaidi (133) na alijaribu nyingi zaidi (265) kuliko mchezaji yeyote katika ligi hizo.
Willian Pacho (Ecuador)
Bado ana miaka 24 tu, beki wa kati wa Ecuador, Willian Pacho amekuwa na msimu mwingine wa kushangaza akiwa PSG, akishinda taji la Ligue 1 na kucheza kila dakika katika kampeni ya ushindi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2025-26. Baada ya hapo, anaonekana kuwa na jukumu muhimu katika safari ya Kombe la Dunia ya Ecuador, ambayo huenda ikajengwa zaidi na ulinzi, ikisaidiwa kwa kiasi kikubwa na beki huyo wa kati.
Mousa Al Tamari (Jordan)
Winga huyo wa kulia wa Rennes asiyechoka ni msumbufu sana uwanjani. Katika Ligue 1 msimu huu, alisababisha penalti nyingi zaidi kuliko mchezaji yeyote (nne), huku akiwa pia katika tano bora kwa chenga ndani ya boksi la wapinzani (mara 19).
Hata hivyo, mchango wake unaenda mbali zaidi ya kile anachofanya na mpira; alirudisha umiliki wa mpira katika eneo la mwisho mara nyingi zaidi kuliko mchezaji yeyote Ligue 1 2025-26 (33).
Anaweza kuwa na haraka kupita kiasi, akiwa ameotea zaidi kuliko mtu yeyote katika ligi ya Ufaransa (26, alitoa asisti sita za mipira 2025-26, wa pili kwa wingi Ligue 1.
Lamine Camara (Senegal)
Kama unavyoamini unachosoma, inaonekana kuna uwezekano mkubwa Lamine Camara akahamia Ligi kuu England baada ya fainali za Kombe la Dunia 2026 msimu ujao. Kiungo mkabaji na mbunifu mwenye nguvu na kipaji cha kiufundi. Tayari ana mengi ya kutoa baada ya baada ya klabu yake Monaco kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, na inaaminika Camara ni miongoni mwa wachezaji watakaouzwa. Kombe la Dunia litampa nafasi nyingine ya kuvutia klabu kubwa, akiwa tayari ana mechi 31 za kimataifa. Kwenye ulinzi, Camara alifanya kazi kubwa, akiwa na urejeshaji wa mpira mara 7.7 kwa kila 90 Ligue 1 msimu huu, wa pili kwa viungo wote (dakika 1,000+). Ni mzuri kwenye nafasi finyu na hutumia mwili wake vizuri, jambo linalomsaidia kujinasua kwenye presha. Usishangae akang’ara zaidi huko Amerika.
Besfort Zeneli (Sweden)
Kama ilivyokuwa miaka 32 iliyopita, wakati Sweden ilishangaza dunia kwa kumaliza nafasi ya tatu mara ya mwisho walipocheza Kombe la Dunia Marekani, Blagult wanaweza tena kutegemea washambuliaji wa kiwango cha juu, akiwemo Alexander Isak na Viktor Gyokeres.
Lakini ingawa kuna wingi wa machaguo mbele, kikosi bado kinatafuta mchezaji wa kuunganisha mchezo; mmoja atakayefurahia nafasi hiyo ni Besfort Zeneli. Mchezaji huyo alikuwa mhimili mkuu katika kiungo cha Elfsborg misimu kadhaa kabla ya kujiunga Union Saint-Gilloise. Zeneli alimaliza msimu wa Allsvenskan 2025 akiwa wa pili kwa kutengeneza nafasi (76) na wa pili kwa kurejesha mipira (mara 176), pamoja na nafasi tano bora kwa chenga (wa tano) na mipambano iliyofanikiwa (wa tatu).
Ricardo Pepi (Marekani)
Mshambuliaji huyo wa Marekani amecheza mechi 100 Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie) ikiwa ni 29 Groningen na 71 akiwa PSV, na amefunga bao moja kila dakika 75 kwa mabingwa hao. Hii ndiyo rekodi bora zaidi ya ufungaji katika historia ya PSV, akiwazidi mastaa kama Mateja Kezman, Ruud van Nistelrooy, Romário na Ronaldo. Pepi pia amefunga mabao sita katika dakika 442 za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Aleksandar Pavlovic (Ujerumani)
Kwa kuwa Joshua Kimmich, staa mwenzake wa Bayern Munich anatarajiwa kucheza beki wa kulia, timu itamtegemea zaidi Pavlovic kuendesha mchezo. Alionyesha umuhimu wake Ligi ya Mabingwa 2025-26 alipokuwa na miguso 100.4 kwa kila dakika 90; miongoni mwa wachezaji wote wenye dakika 500+ alikuwa wa pili nyuma ya Vitinha (111.6). Katika nusu fainali dhidi ya PSG, alikuwa na miguso mingi kuliko wote (72) na kiwango bora cha pasi kati ya waliocheza zaidi ya dakika 45. Kiwango chake cha pasi sahihi Ligi ya Mabingwa msimu huu kilikuwa asilimia 95.4 bora zaidi kati ya viungo na cha tatu kwa wachezaji wote wenye dakika 500+, nyuma ya mabeki wawili tu.
Luiz Henrique (Brazil)
Unapenda chenga za Brazil? Basi unapaswa kumwangalia Luiz Henrique, mmoja wa wachezaji wanaosisimua zaidi wanaokwenda Kombe la Dunia.
Mtindo wake wa mchezo unahusu kile ambacho Wabrazili wanapenda. Amepiga chenga 20 kati ya 33 alizojaribu katika dakika 548 akiwa na Brazil, wastani wa chenga moja kila dakika 27.4. Licha ya kuanza mechi tano tu na kuwa na jumla ya mechi 14 kwa Brazil, amechangia mabao matano (kafunga mawili na asisti tatu) tangu alipoanza Septemba 2024, wastani wa mchango wa bao kila dakika 109.6. Katika kipindi hicho, ni Estevao pekee (moja kila dakika 94) aliye na kiwango bora zaidi kwa wachezaji wenye mechi angalau tatu. Kwa wengi anafananishwa na Garrincha si tu kwa chenga, bali pia kwa mafanikio yake akiwa na jezi namba 7 ya Botafogo iliyowahi kuvaliwa na gwiji huyo.
Yan Diomande (Ivory Coast)
Akiwa amecheza mechi ya kwanza ya kulipwa Ulaya, Machi 2025 kwa Leganes, Yan Diomande aliitikisa Bundesliga katika msimu wake wa kwanza akiwa RB Leipzig akiwa na mabao 12 na asisti nane. Kati ya vijana wote chini ya miaka 20 katika ligi tano kubwa za Ulaya, ni Lamine Yamal pekee aliyehusika na mabao mengi zaidi 2025-26 (27). Na tangu 2004-05, ni Jadon Sancho pekee aliyekuwa na uhusikai zaidi wa mabao katika msimu mmoja Bundesliga akiwa mdogo (29 msimu wa 2019-20, 26 ule wa 2018-19) kuliko Diomande msimu huu (20).
Kwa kasi yake ya ajabu, udhibiti wa hali ya juu wa mpira na kujiamini kupita kiasi, Muivory Coast huyo amejidhihirisha haraka kuwa winga hatari akijaribu chenga nyingi zaidi (213) katika ligi tano kubwa za Ulaya 2025-26, akiwa wa tatu nyuma ya Yamal (265) na Vinicius Junior (218). Hata hivyo, Diomande (55%) ana kiwango cha juu zaidi cha mafanikio ya chenga kati ya wachezaji wote wenye zaidi ya majaribio 100.
Vitinha (Ureno)
Akiwa katika kiwango bora PSG, Ureno wana kipaji cha kiwango cha dunia mikononi mwao. Nyota huyo akiwa na mpira anaweza kuamua kasi ya mchezo, kuleta utulivu unapohitajika na pia kusukuma timu mbele kwa pasi zake kali na za kuvunja safu za ulinzi. Alitoa asisti 11 msimu huu katika mashindano yote akiwa PSG, huku ni Kvicha Kvaratskhelia na Ousmane Dembele pekee waliozidi (12). Aidha, kati ya wachezaji wote katika ligi tano kubwa za Ulaya, Vitinha alitoa pasi nyingi zaidi (5,234), pasi nyingi zaidi katika eneo la wapinzani (3,001) na akashika nafasi ya saba kwa kukokota mpira mbele zaidi ya mita 10 (mara 277). Sio tu akiwa na mpira ambapo anang’ara, alishinda umiliki wa mpira mara 299 Ligue 1 msimu huu, akiwa wa tatu katika ligi zote tano kubwa za Ulaya. Vitinha anaipa Ureno ubunifu, akili ya mchezo na uwezo wa kuvunja mashambulizi ya wapinzani pamoja na nidhamu ya kiulinzi inayomwezesha kushinda mipira na kuzuia mashambulizi.
Luka Vuskovic (Croatia)
Beki huyo wa kati wa Croatia alijiunga na Hamburger SV kwa mkopo kutoka Tottenham Hotspur, Agosti mwaka jana na alicheza mechi 28 za Bundesliga, akimaliza dakika 90 katika 26 kati ya hizo.
Hamburg haikushinda hata mchezo mmoja kati ya sita alizokosekana (sare mbili, kupoteza nne), ikilinganishwa na ushindi wa asilimia 32 alipokuwapo (9/28). Alikuwa nguzo ya ulinzi akiwa na kiwango bora zaidi cha ushindi wa mipira ya juu kati ya wachezaji wote angalau dakika 1,000 (74.5%) na nafasi ya nne kwa ushindi wa mipambano (67.7%). Siyo ulinzi tu, pia alifunga mabao sita akiwa mfungaji wa pili kwa Hamburg na beki wa kati aliyefunga zaidi kuliko wote.
Michael Olise (Ufaransa)
Je, Michael Olise ndiye mshambuliaji hatari zaidi duniani kwa sasa? Mchezaji pekee katika ligi tano kubwa za Ulaya aliyefunga mabao 20+ (22) na kutoa asisti 20+ (26) katika mashindano yote 2025-26 akiwa na Bayern Munich. Pia alishika nafasi ya pili kwa kutengeneza nafasi (123), nyuma ya Bruno Fernandes (138), huku Kevin De Bruyne pekee 2022-23 akiwa na asisti nyingi zaidi katika misimu 10 iliyopita (28).
Kwa Ufaransa amejiimarisha katika kikosi chenye ushindani mkubwa. Tangu 2025, ameanza mechi nyingi zaidi chini ya Didier Deschamps (8) na ana mchango wa pili kwa mabao (6, nyuma ya Kylian Mbappe 13). Anakwenda Kombe la Dunia akiwa na malengo makubwa mawili; kuongoza Ufaransa na kuwa miongoni mwa wanaowania Ballon d’Or.