Pamba yataka kuzifuata Simba,Yanga
Muktasari:
- Timu hiyo imekamilisha maandalizi ya msimu mpya chini ya Kocha Francis Baraza, ikipita katika vituo mbalimbali kwa ajili ya kujenga kikosi, kuimarisha utimamu wa mwili na kuwapa wachezaji nafasi ya kuzoeana kabla ya kuanza kwa ligi.
PAMBA Jiji FC imeweka wazi azma yake ya msimu mpya kuwa si kushiriki tu Ligi Kuu Bara, bali kupambana na timu kubwa na kuhakikisha inajenga nafasi yake miongoni mwa vinara wa ligi hiyo, huku Simba na Yanga zikiwa sehemu ya timu zinazolengwa kushindaniwa kileleni.
Timu hiyo imekamilisha maandalizi ya msimu mpya chini ya Kocha Francis Baraza, ikipita katika vituo mbalimbali kwa ajili ya kujenga kikosi, kuimarisha utimamu wa mwili na kuwapa wachezaji nafasi ya kuzoeana kabla ya kuanza kwa ligi.
Ofisa Habari na Msemaji wa Pamba Jiji FC, Moses William, akizungumza na Mwanaspoti, ameeleza kwa kina maandalizi yaliyofanyika, usajili wa kikosi, wachezaji walioondoka pamoja na dhamira ya klabu hiyo ya kubadili sura yake katika ushindani wa Ligi Kuu Bara.
MALENGO NI NAFASI ZA JUU
Baada ya msimu uliopita kumalizia na Pamba kushika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi. Anasema timu imeweka wazi kuwa haitaki kurudia kiwango hicho bali inataka kuvuka mafanikio iliyoyapata.
Lengo kubwa ni kumaliza katika nafasi za juu na kuwa na uwezo wa kutoa ushindani wa asilimia 100 dhidi ya kila mpinzani.
“Lengo letu kubwa ni kuvuka tulipofikia msimu uliopita. Tunataka kuwa kwenye nafasi za juu isishuku ya nne na kuhakikisha tunatoa ushindani wa asilimia 100 kwa kila timu tutakayokutana nayo,” anasema.
Kuheshimika na kuogopwa na wapinzani wote ni sehemu nyingine ya malengo ya timu hiyo, huku matokeo mazuri yakitarajiwa kuwa msingi wa kujenga heshima hiyo.
“Tunahitaji timu iheshimike na iogopwe na kila mpinzani kwenye Ligi Kuu Bara, siyo kuonekana tunaweza kushindana na baadhi ya timu pekee,”anasema.
MAANDALIZI YA PRE-SEASON
Maandalizi yalianzia Mwanza kabla ya timu kuelekea Arusha ambako ilikaa kwa takriban siku 10 na kucheza michezo ya kirafiki dhidi ya timu za madaraja tofauti.
Baada ya Arusha, timu ilielekea Moshi kwa ajili ya kujenga umoja wa kikosi na kuimarisha utimamu wa mwili. Safari ya maandalizi iliendelea Bukombe, ambako ilialikwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Geita Gold, kabla ya kurejea Mwanza kukamilisha programu yake.
“Maandalizi tumeyafanya kwa kitalaamu, tumeanzia Mwanza, tukaenda Arusha kwa takriban siku 10, tukapitia Moshi kwa ajili ya bonding na fitness, kisha tukakwenda Bukombe kucheza na Geita Gold. Baada ya hapo tukarudi Mwanza kumalizia maandalizi,” anasema Moses.
USAJILI
Katika usajili, timu imezingatia mahitaji ya benchi la ufundi, ushindani wa ligi na ratiba inayotarajiwa kuwa na michezo mingi ndani ya muda mfupi. Mbali na uwezo wa mchezaji, vigezo vilivyopewa uzito ni kujituma, nidhamu ya kimbinu na nidhamu ya jumla.
“Zaidi ya uwezo wa mchezaji, tumeangalia commitment yake, tactical discipline na nidhamu yake kwa ujumla. Tumejaribu kupata wachezaji ambao wanaweza kuendana na mahitaji ya timu,” anasema.
"Timu imeongeza wachezaji wazawa pamoja na wageni kutoka Kenya, Burundi na Gabon. Hata hivyo, milango ya usajili bado haijafungwa rasmi na uwezekano wa kuongeza mchezaji mwingine bado upo."
WACHEZAJI WALIOONDOKA
Kikosi pia kimefanyiwa mabadiliko baada ya kuondoka kwa James Mwashinga, Keneth Kunambi, Yona Amosi, Kelvin Naftal, Peter Lwasa na Emmanuel Charles Lukinda.
"Uongozi wetu ukishirikiana na makocha unaamini mabadiliko hayo yamefanyika kwa kuzingatia mahitaji ya timu na mpango wa benchi la ufundi kuelekea msimu mpya."
MARA YA PILI UFUNGUZI
Msimu huu pia unaingia kwenye historia ya timu hiyo baada ya kuwa mara ya pili ndani ya misimu mitatu kucheza mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara.
Anasema kuwa, ubora wa kikosi na kazi ya benchi la ufundi vinaipa timu nafasi ya kuanza msimu kwa nguvu na kupigania alama tatu katika mchezo wa kwanza.
“Kwa maandalizi tuliyoyafanya na ubora wa kikosi tulichonacho, tunaamini tunaweza kuanza vizuri na kupata alama tatu kwenye mchezo wetu wa kwanza,” alisema.
REKODI ZA MSIMU ULIOPITA
Kwenye msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara msimu wa (2024/2025), klabu ya Pamba Jiji FC (ambayo ilikuwa ndio kwanza imepanda daraja baada ya miaka 23) ilicheza jumla ya mechi 30.
Kutokana na pointi 36 ilizopata, Pamba Jiji FC ilifanikiwa kumaliza katika nafasi ya 7 kwenye msimamo wa jumla wa ligi kuu yenye timu 16.